Sambaza....

TIMU ya Taifa ya Tanzania ‘ Taifa Stars’ ilichapwa 3-0 na Cape Verde Island katika mchezo wa kundi L kuwania nafasi ya kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika mwakani nchini Cameroon. Katika mchezo ulochezwa siku ya jana huko ugenini-Cape Verde wenyeji walitawala sana eneo la kati; kasi yao ikiwa tatizo kubwa kwa wachezaji wa Stars.

Kuna mambo nimeyaona katika uchezaji wa kikosi cha Mnigeria, Emmanuel Amunike. Mwezi uliopita wakati alipoisimamia Stars kwa mara ya kwanza vs Uganda pale Kampala mchezaji huyo wa zamani wa Super Eagle ambaye ni mshindi wa CAN 1994, anapenda soka la kushambulia. Si vibaya, lakini kwa nchi kama Tanzania inayosotea kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika kwa miaka 38 sasa bila shaka naamini ‘falsafa’ yake hiyo haitatufikisha popote.

UPANGAJI WA KIKOSI.


AMUNIKE alianza na wachezaji kumi kati ya 11 waliocheza katika suluhu-tasa dhidi ya Uganda katika mchezo wa jana na majeruhi Frank Domayo tu aliyekosekana. Himid Mao alianza sehemu ya kiungo kama mbadala wa Domayo aliyeumia siku chache kabla ya Stars kusafiri kwenda Cape Verde.

Amunike aliwapanga walinzi watatu nyuma- Agrey Morris, David Mwantika na Abdi Banda. Katika mfumo wa wa 3-5-2 kocha huyo aliwapanga, Mao, Mudathir Yahaya, na Saimon Msuva huku walinzi wa pembeni, Hassan Kessy na Gadiel Michael wakiongeza namba kati mwa uwanja, na mbele walisimama nahodha Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu.

Ilikuwa ni kikosi kizuri lakini kuwaacha nje ya kikosi kilichoanza walinzi wazoefu Shomari Kapombe ambaye aliingia dakika ya 37 kuchukua nafasi ya Gadiel, na Kelvin Yondan na aina ya uchezaji wa Kessy na Agrey bila shaka kocha Amunike alikosea sana na uchaguzi wake huo mbaya wa wachezaji na mfumo aliouchagu kumemponza.

Siku chache kabla ya mchezo huo nilijaribu kuitzama Stars na kufuatilia kuhusu wapinzani wetu na njia pekee ambayo ingetusaida ilikuwa ni kwenda kucheza mchezo mzuri wa kujilinda na kushambulia kwa kushtukiza. Kutumia 4-5-1 ilikuwa njia bora mno na kwa aina ya wachezaji aliokuwa nao kikosini, Amunike hawezi kukwepa lawama.

Kapombe, Gadiel, Mwantika na Kelvin wangefaa mno kucheza katika mfumo wa 4-4-2. Simaaminishi kwamba, Kessy na Agrrey si wazuri lakini tangu vs Uganda mwezi uliopita wachezaji hao walionyesha wasio na umakini na nidhamu ya kimchezo pindi timu inaposhambuliwa. Matatizo yote ya jana katika ngome yalisababishwa na wawili hao.

Gaiel si mzuri katika uchezaji wa wing-back lakini ni mtu anayezalisha magoli mengi klabuni kwake Yanga kutokana upigaji wake wa krosi za mbali, jana na hata dhidi ya Uganda alionekana kushindwa kucheza vizuri katika mfumo wa Amunike, na wakati alipopotea huku Kessy akipoteza umakini, nilidhana Amunike angemtoa mlinzi huyo wa Nkana FC ya Zambia na kumpa nafasi Kapombe ili kubadili mfumo na kutumia walinzi wane nyuma.

Kwa mchezo kama ule ambao unakwenda kuwakabili wapinzani waliocheza fainali mbili kati tatu zilizopita za CAN tena wakiwa nyumbani kwao, Amunike alipaswa kumtumia John Bocco kama mshambulizi huru na nyuma yake kuwapanga viungo watano –akiwemo nahodha, Samatta.

KUTOHESHIMU WAPINZANI-MAZINGIRA.


Miaka miwili iliyopita Visiwa vya Cape Verde vilikuwa juunamba moja kwa ubora wa soka barani Afrika. Hili lilipaswa kutazamwa kwa umakini mkubwa na kulitafutia mikakati ya kupambana. Lakini suluhu ya Kampala ilituvimbisha kichwa na kusahau kutoa heshima kwa Taifa hili dogo la Kaskazini Magharibi mwa Afrika na kichapo cha jana ni fuzo linguine kuwa tunapaswa kujitazama upya na kuachana na siasa katika mambo muhimu.

Kupoteza kwa Cape Verde nyumbani dhidi ya Uganda, Juni mwaka jana na Stars kulazimisha suluhu-tasa Namboole Stadimu mwezi uliopita kulifanya wengi kuichukulia Cape Verde kama ngazi tu ya plastic lakini sasa wametuadhiri.

MIKAKATI


Timu mbili za juu katika kundi zitafuzu kwa fainali za Cameroon mwakani na wakati Uganda na Lesotho wakitaraji kukamilisha mzunguko wa kwanza leo Jumamosi katika kundi, Stars inapaswa kujaribu tena kupanga ‘mikakati ya zima-moto’ kama ilivyo kawaida yetu.

Kesho Jumapili ndugu na majirani zetu Wakenya wataingia bure ili kuujaza uwanja wa Kasarani pale Nairobi kuipa sapoti timu yao ya Taifa itakapokuwa ikiikabili Ethiopia. Kenya walilazimisha suluhu Adid Ababa katikati ya wiki hii na ushindi kesho ubnaweza kuwafanya kufikisha alama saba na huku wakiwa na mchezo mwingine nyumbani ushindi dhidi Ethiopia utawapaisha zaidi.

Si hivyo tu, wachezaji wameahidi Ksh. 250, 000 kama watapata ushindi. Hii ni mikakati ‘hai’ ambayo wenzetu wamekuwa wakiifanya. Stars inawezekana wakawa na nafasi kubwa ya kufuzu kama tutazishinda Cape Verde na Uganda katika michezo miwili ya nyumbani.

Labda, TFF nao wanatakiwa kusahau kuhusu mapato ya mlangoni na kuweka mikakati ya kuingiza mashabiki bure ili kuujaza uwanja wa Taifa. Hili linawezekana na lipo ndani ya uwezo wao kwani mara kadhaa wamekuwa wakifanya hivyo kwa michezo ya timu za Taifa za Vijana.

Sambaza....