Sambaza....

Timu ya Mtibwa sugar imetinga hatua ya nusu fainali ya michuano ya Azam ya michuano ya Azam Sports Federation Cup, baada ya kupata ushindi wa penati 9-8 dhidi ya Azam FC kufuatia sare 0-0 katika dakika 90 za mchezo.

Mara baada ya dakika 90, kukamilika ndipo changamoto ya mikwaju ya penati ikatumika kwa kila timu kupiga penati 10, ambapo Mtibwa sugar walikosa penati moja huku Azam FC wakikosa mbili.

Frank Domayo aligongesha nguzo penati yake, huku ile ya mwisho iliyopigwa na beki Abdallah Heri ikipanguliwa na kipa wa Mtibwa Benedict Tinocco, naye kipa wa Azam FC akipangua mkwaju wa kiungo mkongwe Henry Joseph Shindika.

Waliofunga penati za Mtibwa ni Hassan Dilunga, Ismaily Muhesa, Stamili Mbonde, Hassan Isihaka, Shabani Nditi, Hassan Mganga, Salim Kihimbwa, Cassian Ponera na Dickson Daud.

Kwa upande wa Azam FC ni Himid Mao, Yahya Zayed, Bruce Kangwa, Agrey Morris, Joseph Kimwaga, Joseph Mahundi, Saleh Abdallah na Salum Abubakary.

JKT Tanzania, nayo imetinga hatua hiyo ya nusu fainali mara baada ya kuichapa Tanzania Prisons kwa mabao 2-0 katika mchezo ulifanyika kunako dimba la kumbukumbu ya Sokoine mjini Mbeya.

Mchezo mwingine wa robo fainali unataraji kupigwa kesho kunako dimba Namfua mjini Singida, ambapo wenyeji Singida United wataikairibisha Yanga sc.

Sambaza....