Naisubiri kesho ndipo nimsifu Karia.
Ligi Kuu

Naisubiri kesho ndipo nimsifu Karia.

Sambaza....

Wallance Karia ndilo jina ambalo wazazi wake waliamua kumpatia, sijui kichwani mwa wazazi wao walikuwa wana waza nini kuhusu maisha ya baadaye ya mtoto wake.

Kama ilivyo kwa wazazi bora bila shaka picha ya maisha mazuri ya mtoto wao kwa siku za baadaye ilikuwepo kichwani mwao.

Hiyo ndiyo fahari ya mzazi yoyote kumuona mwanae akifanikiwa kwenye maisha yake ndiyo maana maombi huwa ni makubwa sana na yenye nguvu sana kutoka kwa wazazi wetu.

Maombi haya ndiyo yaliyomfanya Wallance Karia awepo sehemu ambayo alipo kwa sasa.

Sehemu ambayo imebeba hisia za watu wengi, kwa kifupi ndiyo sehemu ambayo inafuatiliwa na watu wengi hapa Tanzania.

Hapana shaka hakuna mchezo unaofuatiliwa kwa ukubwa kama mchezo wa mpira wa miguu hapa Tanzania.

Na Wallance Karia amepewa dhamana hiyo. Dhamana ya kuweka tabasamu kwenye mioyo yetu.

Yeye ndiye ameshikiria maono ya mpira wetu, kwa kifupi yeye ndiye mwenye maamuzi ya kuukuza na kuudumaza mpira wetu.

Tumekuwa tukilia kila siku kuhusu maendeleo mabovu ya mpira wetu kwa sababu hatuna viongozi wenye maono makubwa.

Hatuna viongozi wa kuufanya mpira wetu uwe wa weledi yani kwa kifupi hatuna viongozi wa kuufanya mpira wetu wa kulipwa.

Mazingira hayo hatuna!. Ndiyo maana ninaweza kuwa sahihi nitakaposema Tanzania nzima hatuna kituo cha kuibua, kulea na kukuza vipaji ila tuna vituo vya timu za vijana.

Mpira wetu hauanzwi kufundishwa katika ngazi za chini yani kuanzia miaka (0-5). Mara nyingi tumekuwa tukichukua watoto wenye miaka zaidi ya mitano na kuanza kuwafundisha.

Vijana hawa hukosa misingi ya mwanzo ya mpira na huanza kufundisha wakiwa katika umri mkubwa kitu ambacho hakina tija kubwa.

Hapa ndipo umuhimu wa Wallance Karia unapoanzia. Simaanishi yeye ndiye anayetakiwa kutujengea vituo hivi vya kuibua, kulea na kukuza vipaji ila maono yake yanatakiwa kutuletea vituo hivi.

Yeye ni Raisi wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF), ngazi ambayo inaushawishi mkubwa kwa watu mbalimbali. Ni rahisi kwake kuanzisha mazungumzo yenye faida kibiashara kwa viongozi wa timu mbalimbali duniani kuja kuweka kituo cha vipaji hapa (academy) au watu wenye pesa kuwekeza kwenye biashara hii ya mpira.

Inawezekana hawa watu hawajaambiwa vizuri faida ambayo inapatikana kwa kuwauza wachezaji ambayo kituo fulani kiliwaibua , kuwalea na kuwakuza wachezaji hao.

Kukuwepo na nguvu ya ushawishi hakuna mfanyabiashara asiyependa kuwekeza sehemu yenye faida kwake.

Imekosekana nguvu ya ushawishi pekee kutoka kwenye shirikisho letu la mpira, nguvu ambayo ingetumika hata kuvishawishi vilabu mbalimbali barani ulaya kuleta wakufunzi bora wa masuala ya ukocha kwa ajili ya kuwafundisha makocha wetu.

Tuna idadi ndogo sana ya makocha, na mpira wetu hauwezi kuendelea bila kuwa na watu ambao wanaufundisha mpira.

Leo hii Ujerumani tunaiongelea kama nchi yenye wachezaji wengi kwa sababu ilianza kuzalisha makocha wengi ambao walikuja kuzalisha hao wachezaji.

Baba bora ni yule anayetoka kwenda kutafuta, hakuna baba aliyebora anayekaa ndani masaa 24 akitegemea atabapa pesa ya mahitaji ya familia yake akiwa amekaa.

Ndipo hapo hata akili yangu inapouma inapofikiria kuwa mpaka muda huu tuna wadhamini wawili kwenye ligi yetu.

Logo ya Ligi Kuu

Ligi ambayo itakuwa na timu 20, najaribu kujiuliza ni kwa jinsi gani hii ligi ikaweza kujiendesha kwa kujimudu ikiwa na wadhamini wawili pekee?

Chapa ya ligi yetu haijatosha kushawishi wafanyabiashara kuja kuwekeza katika ligi yetu? Au sisi watu wa masoko na masuala ya chapa ya ligi yetu tuliokabidhiwa dhamana hiyo tumeshindwa kuwashawishi wafanyabiashara kuja kuwekeza kwenye ligi yetu.

Tuna subiri watu watufuate bila wao kuwashawishi kuingia ndani kwetu?, kwanini tusitengeneze mazingira ya kuwashawishi kipindi hiki tukiwa na shida?

Ligi yetu inafuatiliwa kwa kiasi kikubwa sana, kwa kifupi ligi yetu ni nembo kubwa sana, nembo ambayo ilitakiwa kupambwa na makaratasi ya wadhamini wengi tu.

Kitu ambacho kingepunguza hata njaa kwa vilabu vyetu. Hata waamuzi wetu wangelipwa vizuri na kuepukana na vishawishi vya kuuza mechi.

Ndiyo maana hata nikiangalia viwanja vinavyotumika kwenye ligi kuu huwa naumia sana. Wallance Karia ana nguvu kubwa sana ya kuwashawishi wamiliki wa viwanja hivi kuvikarabati.

Ndipo hapo nafsi yangu inaposita kumsifia Wallance Karia leo hii labda nisubiri mpaka kesho atakapoamka vizuri.


Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x