Blog

Tuikumbuke Kesho tuliyoisahau kwa Goli la Ajib.

Sambaza....

Jana ambayo ilitengenezwa na juzi mbovu, juzi ambayo hatukuruhusu akili zetu kuwaza vyema. Hatukuipa nafasi akili yetu kufikiria maisha ya baadaye ndiyo maana jana tuliishi kwenye nyumba mbaya na leo tunazidi kukaa kwenye nyumba mbovu.

Nyumba isiyokuwa na msingi imara, msingi ambao hufanya ukuta wetu uanguke mara kwa mara na bila kufikiria kutibu tatizo akili zetu huziaminisha katika kuziba nyufa za kuta zetu kwa kutumia mifuko ya rambo!.

Bado hatujaamua kuwaza sawa kabisa kwa sababu tulipata akili ya kutowaza sawa kutoka kwa watangulizi wetu ndiyo maana tunaishi maisha ya shida sana, maisha ya kuomba omba kila uchwao.

Tuna umri mkubwa lakini bado hatujapata uwezo wa kujitegemea sisi kama sisi. Na bado hatujafikiria hata siku moja kuwa kuna mawio yatatukuta tukiwa kwetu ambako hakuna mateso makubwa, hata machweo yatakapofika usingizi wetu utatunukiwa na sehemu nzuri ya kuweka ubavu wetu.

Kwa kifupi hatujatamani kuishi maisha mazuri na bora yenye furaha ambayo inaendana na wakati wa sasa. Wakati ambao unahitaji kila kitu kifanyike kwa jicho la biashara ili kipate kufanikiwa kwa kiwango kikubwa sana!.

Tumekataa kuishi kwenye nadharia hii ndiyo maana hatuna hata uwanja wa mazoezi ambao tungejivunia kama sisi kuwa ni wamiliki halali wa uwanja huo na kuepusha gharama za kwenda kukodi viwanja vya mazoezi na wakati mwingine havina hadhi kubwa kwa mchezaji wa daraja la ligi kuu kufanya mazoezi.

Hatujali kuhusu hilo, ndiyo maana hata wachezaji wetu tulionao hatuwatunzi kama wachezaji wa kulipwa. Ni kawaida sana kwetu sisi kumfanya mchezaji akae miezi minne bila kupata mshahara wa aina yoyote ile.

Ni kitu cha kawaida sana kwa sababu tumezoea kufanya vitu katika ukawaida usio wa kawaida, na kibaya zaidi tumezoea kabisa kuishi ndani ya uchafu.

Tunafurahia sana kuona uchafu, kuishi nao hata tunapokula milo yetu ya kila siku hula ndani ya huo uchafu. Hatujali kabisa afya zetu, kitendo ambacho kimesababisha tusiwaze kabisa kuwa afya za wachezaji wetu.

Wachezaji ambao wanatutumikia sisi kama sisi, wachezaji ambao wanatupa furaha lakini kipindi wanapopatwa na majeraha hakuna anayejumuika naye kwenye maumivu yake.

Matibabu yao huwa ya hali ya chini sana, ndiyo maana kuna wakati mchezaji huchelewa kurudi uwanjani kutokana na kutopata matibabu mazuri. Kwa kifupi eneo hili la matibabu hatujawahi kulifikiria katika uzito wa hali ya juu.

Tunaliona la kawaida sana na kusahau kuwa eneo la matibabu kwa wachezaji ni eneo muhimu sana ndani ya timu. Eneo ambalo linahitaji uwekezaji wa hali ya juu. Hata kama ukishindwa kujenga Kliniki za matibabu kwa wachezaji kama kiongozi mwenye maono una nafasi kubwa sana ya kuingia ubia wa kibiashara na hospitali kubwa ambayo itahusika na matibabu ya wachezaji kibiashara.

Tumeamua kuweka giza kwenye akili zetu na kuamua kutupa tochi ndani ya bahari,  hatutaki mtu yeyote atokee wa kuichukua hiyo tochi na kumulika akili zetu.

Mtu ambaye atakuwa na tochi ya kumulika giza letu la kukosa hata Gym kwa ajili ya wachezaji wetu. Hatujafikiria kuingia ubia kabisa na Gym ambayo inaweza kutusababisha sisi kama sisi kuwapeleka wachezaji kufanya mazoezi kwa makubaliano ya kibiashara.

Makubaliano ambayo yanaweza kufanyika hata kwenye usafiri, kuna mechi nyingi sana za mikoani. Mechi ambazo zinachosha sana kama ukitumia usafiri wa basi. Tuna makampuni kadhaa ya ndege, ambayo yanafanya biashara.

Hakuna mfanyabiashara asiyependa kupata sehemu ya kutangaza bidhaa yake. Klabu yetu ni kubwa sana na inamshabiki wengi sana. Kwa kifupi inaweza kutumika kama sehemu sahihi ya kutangaza bidhaa ya mfanyabiashara husika.

Hivo, ni vigumu kwa mfanyabiashara kukataa klabu husika kugharamikia nusu bei ya ticketi za ndege kwa akili ya kwenda mikoani. Hii inatengeneza mazingira mazuri kwa wachezaji kucheza bila mawazo na uchovu wa aina yoyote.

Ndiyo maana tumeridhika na udhamini wa wadhamini wachache tulionao , sehemu ambayo inaweza kuwa na wadhamini wengi na klabu ikaishi bila kuomba omba.

Sehemu ambayo inaweza kuingia mkataba na mfuko wa jamii wowote kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa timu husika kwa makubaliano maalumu na uwanja huo ukaitwa jina la mfumo huo wa jamii mfano, NSSF Stadium, PPF Stadium n.k.Na timu ikanufaika kwa kiwango kikubwa na kiwanja husika.

Ila matatizo yote haya tunayasahau na kujifariji kwa furaha ya muda mfupi. Furaha ambayo haina maisha marefu, furaha ambayo siyo imara. Leo hii goli la Ajib linatupa furaha na kuyasahau matatizo yetu lakini baada ya wiki moja tutarudi kwenye uhalisia wetu na kubaki tunalia na matatizo yetu kwa sababu hatujaamua kutoka kwenye hayo matatizo.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x