Shirikisho Afrika

Giza la Yanga ni mwanga wa Simba

Sambaza....

Jana giza liliingia mapema sana hapa nchini, giza ambalo lilikuja na majonzi makubwa sana kwa Watanzania wengi

Muambatano huu wa giza na majonzi umedumu kwa muda mrefu bila mwanga kuonekana mbele ya mboni za macho yetu.

Usiku umekuwa mrefu sana kwetu na kibaya zaidi usiku wetu ulianza mapema sana. Jua la saa kumi na mbili lilizama jana na kukaribisha giza la usiku wa tarehe 07/03/2017.

Giza ambalo mpaka sasa limekuwa totoro, hakuna mwanga tena unaoonekana kwa sasa. Hata vibatari tulivyokuwa tunavitegemea Wabotswana wameenda navyo.

Wamevichukua kipindi ambacho hata jua limependa kukaa magharibi, mashariki pameonekana siyo mahali pazuri kwake.

Halitaki tena kuanza safari ya kwenda mashariki, kitanda cha magharibi kimekuwa adhabu kwetu maana hatuoni tena kwa ufasaha kwa sababu ya giza hili totoro.

Giza ambalo lilisababishwa na Yanga. Yanga ambayo ilikuwa tegemeo kwetu kama mwakilishi wetu wa michuano ya kimataifa.

Michuano ambayo kwa mwaka huu mwanzo wao ulionesha mwisho wa mji ambao watafikia.

Haukuwa mwanzo mzuri wa kutia matumaini. Mwanzo ambao tulitegemea kuiona Yanga iliyokuwa katili kwa vilabu vinavyotoka kwenye visiwa kama Sherisheri na Comoro.

Ilikuwa kawaida sana kusikia kelele za watu mtaani wakisifia mauaji ya ƙkikatili yaliyokuwa yanayofanywa na Yanga dhidi ya vilabu vinavyotoka nchi hizi.

Ungeshangaa kukuta gazeti limeandika “Yanga yawaua Wacomoro kwa risasi saba”? Hapana shaka halikuwa jambo la kushangaza.

Ukawaida wa jambo hili ulikuwa unatengenezwa na Yanga kuwa na wachezaji wanishandani na wanaoendana na michuano hii, wachezaji ambao walikuwa wanajua kutumia ipasavyo uwanja wao wa nyumbani.

Wachezaji ambao walikuwa na hasira, hasira ambayo iliwafanikisha kufika robo fainali ya michuano ya kombe la shirikisho misimu miwili iliyopita.

Hii ndiyo ilikuwa Yanga ambayo ilikuwa na wauaji wengi ndani ya kikosi, kipindi Amis Tambwe alipokuwa anazembea kuua, Donald Ngoma alikuwa anakuja na kitako cha bunduki yake na kumpiga adui kisogoni.

Kuna kipindi Simon Msuva alikuwa haridhiki na vifaru alivyokuwa anamiliki mpaka alikuwa na mabomu ya nyuklia, mabomu ambayo yalikuwa yanarahisisha kuua adui ambaye alionekana msumbufu mbele ya kina Donald Ngoma na Amis Tambwe.

Hata wanajeshi wa nyuma walikuwa na nguvu na hawakuwa na masihara walipokuwa kwenye uwanja wa vita.

Haruna Niyonzima na Kamusoko walikuwa thabiti kutengeneza njia nzuri za kumuua adui, hata kipindi kazi ilipokuwa inawashinda nje kwenye benchi kulikuwa na wanaume ambao wangeweza kubadili upepo wa vita, ilikuwa jambo la kawaida kwa Obrey Chirwa kutokea benchini .

Leo imekuwa hadithi tofauti kabisa, hadithi yenye kutia huruma kabisa moyoni kipindi unapoisoma, huruma ambayo inaenda na riwaya ya “simu ya kifo” ya Ben Mtobwa.

Inawezekana Ben Mtobwa alikuwa ni mmoja waandishi mahiri hapa nchini waliowahi kutokea, mwandishi ambaye aliacha alama yake ya maandishi kwenye karatasi zenye pumzi iliyohai mpaka muda huu.

Uhai wa pumzi yake upo kwenye kila kurasa ya vitabu vyake alivyowahi kuandika hata ukifunua kurasa za riwaya yake ya “msako wa hayawani” yaweza kukupa picha tosha ya mechi ya jana ya Yanga na Township rollers ilivyokuwa.

Ni mara chache sana kuiona Yanga ikikimbia chumba chake kwa kuogopa kelele za mgeni wake.

 

Misimu mitatu iliyopita Yanga ilikuwa jabali la kila timu iliyokuwa inakanyaga hapa, ardhi ambayo ilikuwa ngumu hata kwa Al Ahly ya misiri.

Lakini jana ilishangaza kushuhudia msako wa hayawani, hayawani ambaye aliogopa hata nyumba yake na kuamua kutumia muda mwingi akikimkimbia mgeni ambaye aliweka makazi bila shaka yoyote.

Ilikuwa ni aibu, aibu ambayo imelifanya jua mpaka muda huu ling’ang’anie magharibi, linasubiri mtu mmoja tu aje kulishawishi, Simba ndiye anayeweza kusababisha mwanga kumulika tena kwetu.

Wanasilaha ambazo zinaweza kuingia vitani na kutupa ushindi, ushindi ambao utatupa mwanga mzuri ndani yetu. Kikosi chao kinachoanza kina watu ambao walikuwa wanapatikana ƙkipindi ambacho Yanga ilikuwa inafanya vizuri misimu miwili iliyopita.

Hata benchi lao lina silaha za akiba, silaha ambazo zinaweza kugeuza usiku kuwa mchana wenye mwanga angavu.

Ukubwa huu wa benchi ndiyo mwanga ambao wanao Simba, mwanga ambao haupo kwa kaka yake Yanga, mwanga ambao wanaweza kuutumia kuliondoa giza ambalo Yanga jana aliliweka na halijaondoka mpaka muda huu

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x