Sambaza....

Mabingwa wa soka Tanzania bara Yanga sc, watavaana na klabu ya Walayta Dicha ya Ethiopia katika mchezo wa mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la barani Afrika.

Hiyo itakuwa ni mara ya pili kwa klabu hiyo ya Ethiopia kuja nchini, ambapo mwezi Februari walikuja visiwani Zanzibar kuumana na Zimamoto FC ikapata ushindi wa jumla wa mabao 2-1 baada ya kulazimisha sare ya 1-1 kunako uwanja wa Aman, kabla ya kupata ushindi wa bao 1-0 kule Ethiopia.

Hiyo ni kwa mujibu wa droo iliyopangwa leo Cairo,Misri huku Yanga wakianzia nyumbani kati ya Aprili 6-8 kabla kurejeana kati Aprili 17 na 18 mwaka huu.

Welayta Dicha imefikia hatua hiyo, baada kuwaondosha Zamalek ya Misri kwa mikwaju ya penati 4-3 hiyo ikiwa ni baada kwenda ya 3-3 kwa kila moja ikipata ushindi nyumbani kwake.

Yanga sc, imefikia hatua hiyo baada ya kuondolewa kunako michuano ya Ligi mabingwa Afrika, kwa kukubali kichapo cha mabao 2-1 katika mchezo wa kwanza uliopigwa Dar es salaam, kabla kwenda kulazimisha sare ya 0-0 katika mchezo wa marejeano dhidi ya Township Rollers kunako uwanja wa taifa wa Gaborone, Botswana.

Huu unakuwa ni mwaka wa tatu mfululizo kwa Yanga, kuangukia kunako hatua ya mchujo wa kuwania kucheza hatua ya makundi ya Shirikisho, huku rekodi nzuri kwao ikiwa ni mwaka 2016 ambapo walipoitoa Esperanca Sagrada kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-1 ikishinda 2-0 Dar es salaam, kabla ya kufungwa bao 1-0 kule Angola.

Sambaza....