MABINGWA mara 27 wa kihistoria wa ligi kuu Tanzania bara, Yanga SC kwa mara ya pili mfululizo wanashinda mechi ambayo hadi wakati wa mapumziko walikuwa nyuma.
Jumatatu iliyopita kikosi hicho cha koch Mcongo, Zahera Mwinyi kilipambana ´kufa na kupona´na kutumia robo saa ya mwisho ya mchezo kurudisha goli la Tanzania Prisons na kushinda 3-1 katika uwanja wa Sokoine, Mbeya.
YANGA 2-1 BIASHARA UNITED
Usiku uliopita Yanga ilikuwa hatarini kuangusha pointi katikauwanja wa Taifa, Dar es Salaam mbele ya timu iliyo mkiani Biashara United FC kutoka Mara baada ya timu hiyo ngeni katika ligi kuu kutangulia kufunga dakika ya 38 kupitia kwa Abdulmajidi Mangalo na ´kupaki basi´ kwa dakika 37.
Mlinzi wa kati Abdallah Haji ´Ninja´ akimalizia vizuri pasi ya mshambulizi Mrundi, Amis Tambwe dakika ya 70, haitoshi mfungaji namba moja Mcongo, Heritier Makambo alitumia uwezo wake binafsi na kufunga goli lake la nane katika ligi dakika kumi kabla ya kumalizika kwa mchezo na kuirudisha kileleni mwa msimamo timu yake.
ZAHERA…
Kocha huyo bora wa ligi kuu mwezi November ameendeleza kiwango chake bora msimu huu. Zahera ´mtaalam wa sub´ alilazimika kufanya mabadiliko yasiyo ya kiufundi dakika ya mwisho kipindi cha kwanza kwa kumtoa kiungo aliyeumia Rafael Daud ambaye nafasi yake ilichukuliwa na raia wa DR Congo, Papy Tshishimbi.
Ndani ya dakika kumi mara baada ya kuanza kwa kipindi cha pili, Zahera alifanya mabadiliko mengine Lakini safari hii yalikuwa ya kiufundi zaidi. Zahera aliamua kumpumzisha kiungo wake bora tangu kuanza kwa msimu, Feisal Salum ´Fei Toto´ na kwa mara ya kwanza Pius Buswita alipewa nafasi msimu huu.
Biashara waliendelea kucheza mchezo wa kujihami na kubaki wengi katika eneeo lao la ulinzi. Zahera aliona njia pekee ya kuupita msitu wa wapinzani wake ni kuendelea kuwaongezea washambuliaji na ndipo akamuingiza uwanjani, Tambwe wakati mchezo ukielekea nusu saa ya mwisho.
Kama alivyofanya vs Prisons, Tambwe akatengeneza goli la kusawazisha ambalo sasa liliwafanya Biashara United kufunguka katika ngome yao hali iliyo sababisha Makambo kufunga goli la ushindi dakika ya 80.
Ushindi huo umewafanya mabingwa hao mara tatu mfululizo wa zamani kufikisha alama 41 baada ya michezo 15. Kwa timu iliyodharauliwa chini ya kocha aliyebezwa kabla ya kuanza kwa msimu- kukusanya pointi 41 kati ya 45 walizopaswa katika michezo 15 ni mafanikio makubwa, pia ni ´onyo´ kwa wale wote waliokuwa wakiwadharau.
Zahera anaendelea kuweka alama yake ya kimapinduzi katika soka la Tanzania. Uaminifu wake imekuwa silaha kubwa mno kwa mwenendo huu ambao haukutarajiwa. Mbinu zake, hamasa na uwezo wa kuusoma mchezo ni wa kipekee, Lakini hii tabia ya kutangulia kufungwa kisha kupindua matokeo anapaswa kushughulika nayo kabla ya kuzivaa Mbeya City FC na Azam FC wiki hii.
Inapendeza na kudhihirisha uwezo wa timu pale inaposawazisha na kushinda mechi, lakini si rahisi kufanya hivyo ( kuongozwa) hadi kipindi cha kwanza na kushinda mechi. Morali yao imewabeba vs Tanzania Prisons na Biashara United. Watapoteza dhidi ya City na Azam FC kama wataendelea kuruhusu kuongozwa mchezoni kwa kipindi cha kwanza.