Sambaza....

Naam joto la Watani wa Jadi linazidi kufukuta kuelekea Novemba tano Jumapili ambapo Simba atakua mwenyeji wa Yanga katika mchezo wa mzunguko wakwanza wa Ligi Kuu ya NBC.

Licha ya mvua kubwa inayonyesha mjini Dar es salaam lakini vilabu hivyp na mashabiki wao ni kama hawana habari nayo wakiendelea na maandalizi wa mchezo huo ambao kwa kiasi kikubwa una nafasi yake katika alama za ubingwa wa Ligi msimu huu.

Tayari Yanga wameshapoteza mchezo mmoja wa Ligi na hivyo kuiacha Simba pekee ikiwa haijapoteza mchezo mpaka sasa “unbeaten” licha yakwamba Yanga wapo kileleni mwa Ligi na alama 18 sawa na Simba lakini wao wakiwa na magoli mengi zaidi.

Kiungo wa Yanga Khalid Aucho akimuacha Clatous Chama wa Simba.

Kuelekea mchezo huo ambao upo ndani ya tano bora kwa “Derby” kubwa Barani Afrika si tu kwamba unafwatiliwa nchini Tanzania pekee bali ni kama Afrika nzima sasa unaifwatilia na kuutilia maanani mchezo huo wa Derby ya Kariakoo.

Tovuti yako pendwa ya Kandanda.co.tz inakuletea nchi ambazo mchezo huo umepata mashabiki na kufwatiliwa zaidi kutokana na sababu mbalimbali za Kikandanda:

Mali

Magharibi mwa Afrika kuna nchi inaitwa Mali ambapo kuna raia wake watakutana siku hiyo ya Jumapili, kwanza kuna mlinda mlango wao  wa timu ya Taifa ya Mali Djigui Diara atakua katika lango la Yanga halafu pia kuna Sadio Kanoute kwa upande wa Simba kwenye eneo la kiungo. Wawili hao watawafanya watu wa Mali kufwatilia mchezo huo.

Djigui Diarra.

Zambia

Kuna Jenerali Moses Phiri na Clatous Chama kwa upande wa Simba halafu kuna Kenedy Musonda wa Yanga wote kwa nyakati tofauti wamepita timu ya Taifa ya Zambia “Chipolopolo” ukiachana na Chama ambae mpaka sasa anaitumikia timu hiyo inayojiandaa kushiriki Afcon huku ikiwa kundi moja na Tanzania.

Afrika Mashariki

Hapa kuna Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda majirani hawa siku hizi wamekua wakiitolea macho Ligi yetu kutokana na maendeleo makubwa na hatua kubwa tuliyoipiga katika mpira wetu. Uwepo wa uwekezaji mkubwa katika Ligi yetu umewavutia wachezaji wao ambao wapo nchini lakini pia sababu za kifedha. Kuna kina Khalid Aucho na Gift Fred (Uganda), Said Ntibazonkiza (Burundi) wakati Rwanda wao watataka kumfwatilia MVP wao wa Ligi msimu uliopita Willy Esomba Onana.

Congo Napo Balaa

Miongoni mwa nchi zenye wachezaji wengi katika Ligi ya NBC ni Congo DR, ina idadi kubwa ya wachezaji wanaocheza hapa lakini pia wamefanikiwa haswa kwa timu hizi mbili za Kariakoo. Kuelekea mchezo huo nchi hiyo imetoa wachezaji wengi si tu wapo katika timu hizo lakini pia ni wachezaji muhimu na wanategemewa kuanza katika mchezo huo.

Mlinzi wa Simba Henock Inonga Baka akishangilia bao la kwanza la Simba katika mchezo dhidi ya Yanga walipokutana mara ya mwisho katika Ligi.

Kutoka Congo kuna Max Nzengeli, Jesus Moloko na Lomalisa Mutambala hawa watakua upande wa Wananchi, wakati kwa Simba kuna Henock Inonga, Fabrice Ngoma na Jean Baleke huku wote hao wakiwa nyota muhimu katika timu zao.

Misri Nao Wapo

Wababe wa Misri Al Ahly watakua na kibarua kizito dhidi ya Yanga Disemba mwaka huu katika Ligi ya mabingwa Afrika hivyo ni wazi benchi la ufundi litautumia mchezo huo kutazama mambo ya kiufundi ili waweze kujiandaa kukabiliana nao mapema.

Skudu Makudubela

Afrika Kusini Pia

Skudu Makudubela atakua uwanjani kucheza Derby kwa mara ya kwanza tangu ajiunge na Wananchi akitokea nchini Afrika Kusini katika klabu ya Marumo Gallants hivyo ni wazi mashabiki wa soka kutoka nchini humo watataka kumuona Skudu atafanya nini na timu yake ya Yanga.

Ukiachana na hao pia kuna baadhi ya nchi kama Cameroon anapotoka Esomba Onana na Che Malone, Ivory Coast kuna Pacome Zouazoua watakua wakoufwatilia mchezo huo ili kuwaona nyota hao.

 

Sambaza....