Sambaza....

Klabu ya Yanga kutoka Tanzania imeanza msimu wa ligi vyema baada ya kucheza mechi saba na kushinda sita na kupoteza moja na anaongoza ligi akiwa na alama 18 akimtangulia Simba mwenye alama 18 wakitofautishwa na idadi ya magoli ya kufunga na kufungwa, Yanga akiwa na idadi kubwa ya mabao kuliko Simba.

Yanga ya msimu huu ni tofauti kwani wanasifika kwa kucheza soka la kasi na pasi nyingi na kuutawala mchezo kwa kiasi kikubwa kiasi cha kumnyima adui nafasi hata ya kuuchezea.

Kumekuwa na uwiano sawa katika idara zote kiwanjani kuanzia idara ya ulinzi, kiungo na ushambuliaji.

Dickson Job na Mudathir Yahya.

Idara ya kiungo ya Yanga ndiyo idara muhimu zaidi kwani ushindi na mipango yote hupangwa hapo. Asilimia kubwa ya magoli yao yamefungwa na viungo wao mafundi, Aziz Ki mwenye mabao 6, Max Nzengeli mwenye mabao 5 na Pacome Zouzoua magoli 3 pamoja na Mudathir Yahya mwenye mabao 2.

Safu ushambuliaji ya Yanga haina magoli mengi kama ilivyo kiuongo. Kiungo cha Yanga kimegawanyika mara mbili ambapo kuna kiungo cha chini (uzuiaji) na kiungo cha juu (ushambuliaji). Kiungo cha chini cha Yanga kinaundwa na Khalid Aucho pamoja na Mudathir Yahya huku kiungo cha juu kinaundwa na Aziz Ki, Pacome na Max Nzengeli. viungo hawa washambuliaji wamekuwa ndio muhimili wa mashambulizi ya Yanga, Aziz Ki, Pacome pamoja na Max wamekuwa wakicheza kwa kupishana na kulizunguka eneo la kiungo huku Max akiwa na jukumu huru kiwanjani la kuunganisha timu na kushambulia maeneo yote yenye uwazi na kumfanya kuwa mchezaji hatari zaidi kwa timu pinzani.

Max Nzengeli na Hafiz Konkoni

Aziz Ki amekuwa na uwiano mzuri wa kupiga mashuti nje ya lango na kuitumia vema mipira iliyokufa kama vile faulo na kona na kumfanya kupata nafasi nyingi za kufunga magoli kiasi cha kupachika goli sita mpaka sasa huku akiwa kinara wa ufungaji.

Kwa kiasi kikubwa Yanga imepunguza matumizi ya mawinga huku ikiamini katika matumizi makubwa ya viungo. Washambuliaji wa Yanga wakiongozwa na Kenedy Musonda, Clement Mzize, na Hafiz Konkon hwajaanza msimu vema kwani wamekuwa na uwiano mdogo sana wa kufunga. Hata hivyo Yanga ya sasa haitegemei washambuliaji kufunga.

Aziz Ki na Konkoni

Mechi inayofuata kwa Yanga ni dabi dhidi ya Simba Novemba 5 Jumapili, mara ya mwisho walipokutana katika ligi Yanga alipoteza kwa bao mbili bila. Inafahamika wazi kuwa roho ya Simba iko katika kiungo chao ambacho kinaundwa na mafundi wa soka na watukutu kwelikweli wawapo kiwanjani, Je Simba wataweza kukizuia kiuongo cha Yanga kisitimize majukumu yake? Je Yanga wataendeleza ushindi na kuwafanya waongoze ligi mbele ya Simba?
Basi baki na Kandanda.co.tz kwani wanakupa nafasi ya kujadili na kutoa maoni, karibu utoea maoni yako hapa chini.

NB: KARIBU KWENYE ULIMWENGU WA KANDANDA

Sambaza....