Kombe la Dunia

Bravoo Serengetii Girls!

Sambaza....

Allez Allez Serengeti Girl

‘’Mon équipe mon choix ‘’

Najua wenzangu nami watataka kujua mwalimu amechanganyikiwa kwanini aandika lugha tusivyo ijua kwa walio wengi!

Yawezekana ni kilele cha furaha yangu kuona timu yetu ya Taifa kwa wasichana wa chini ya umri wa miaka 17 wamefuzu kushiriki kombe la Dunia kule India.

Siku zote mimi binafsi hujivunia timu zetu za Taifa maana ndiyo utambulisho wangu wa kwanza kabla ya vilabu vyenu hivi.

‘’Mon équipe mon choix ‘’ ni lugha ya kifaransa yenye maana ‘timu yangu chaguo langu’ na “Allez Allez” ni kama kuhimiza vile ‘nenda nenda ‘ mkafanye yenu.

Kwa heshima na taadhima nitapenda kuchukua nafasi hii kulipongeza benchi la ufundi chini ya ‘Mchawi Mweusi ‘ Bakari Shime na mwanadada Edna Lema ‘Mourinho’ wachezaji, madaktari na benchi la ufundi kiujumla kwa kufanikisha hili ikiwemo Watanzania wote kwa ushiriki wao kwa maana moja au nyingine kwa kuwa naamini wapo waliowaombea vijana hawa watoboe na wakatoboa.

Bakari Shime.

Najua haikuwa jambo jepesi kufuzu kwa aina ya machakato tuliopitia
lakini hatimaye imekuwa hivyo.

Binafsi nami nastahili pongezi zangu kwa kugundua vipaji vya mabinti wawili waliomo kwenye kikosi hichi wakicheza kama’ key players” Nahodha Noela Luhala na Clara Luvanga kifupi wamenitendea haki na sikuyadanganya macho yangu nilipo waona wakiwa wadogo zaidi miaka kadha iliyopita kabla ya kuingia kwenye mfumo wa kutambulika kwa kupitia timu ya Mapinduzi Queen’s ya Njombe.

Nataka nitumie nafasi hii kuwapongeza pia wazazi wao wachezaji wote na walimu /makocha waliowafanya wakafikia hatua hii na leo kuwa mashujaa wa Taifa si jambo dogo hata kidogo.

Lakini sasa nakwenda kutizama ugumu wa hatua tunayoenda kushiriki, michuano itakayofanyika kwa wiki 3 nchini India kwa kuanza tarehe 11/ 10/2022 na kutamatika 30/10/2022.

Ikiwa na mfumo wa makundi 4 toka kwa timu shiriki ambazo kila bara au shirikisho husika kama AFC, CONMEBOL, CONCACAF, UEFA na CAF ikitoa timu 3 kasoro OFC ikitoa timu moja pekee.

Nilikuwa najaribu kuangalia kila bara Taifa gani na gani ililokwisha kukata tiketi nikaona ni mataifa shindani na makubwa sana linapokuja soka la wanawake kwa mfano Brazil, USA, Germany,  France na Spain.

Licha ya kwamba makundi bado hayajapangwa lakini naona ushindani na ugumu wa hatua iliyoko mbele yetu kutokana na nguvu za mataifa tuliyofuzu nayo.

Hivyo basi katika kipindi hichi kilichobaki ushauri wangu ni kufanya maandalizi ya kina ikiwemo kambi ya nje kwa mataifa yaliyofanikiwa kwenye soka la wanawake kukubali kubadilishana na kushare uzoefu kwenye eneo la kiufundi pia.

Mfano mataifa kama Netherlands na Sweden ambayo hayajapata nafasi ya kufuzu wenzetu wamepiga hatua kubwa sana linapokuja suala la soka la Wanawake hivyo ingewezekana kuweka Kambi huko kwa muda kwa sababu za kiufundi /kitaalam kushare maarifa na wabobezi wa soka la wanawake kwenye sehemu hii kubwa.

Pia eneo la mwisho kama litakuwa na ulazima ni kuweka kambi kwenye miji au Taifa linalofanana na hali ya hewa ya India mazingira na tamaduni  muda mchache kabla ya mashindano kuanza.

Kwa kufanya hivi yawezekana tukafanya vyema zaidi na kutengeneza masoko ya wachezaji wengi wa Tanzania kwa kuifanya nchi iwe inasikika mara kwa mara kupitia ushiriki wa timu zetu za Taifa katika mashindano makubwa kama haya.


Sambaza....
Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.