Blog

David Silva mtoto wa Polisi anaepigiwa salute Uingereza

Sambaza....

Ilikua tarehe nane mwezi wa kwanza mwaka 1986 ambapo mama mwenye asili ya Kijapani aliyeolewa nchini Hispania Bi Eva alitabasamu baada ya kujifungua mtoto wa kiume mwenye furaha na kumkabidhi kwa babaye Mr.Jeminez aliyekua ofisa wa polisi nchini humo.

Ni zaidi ya kilometa 3,975.6, kutoka Arguineguin nchini Hispania alikozaliwa kiungo wa mpira David Josua Jimanez Silva mpaka mjini Manchester kule Uingereza iliko klabu tajiri ya Manchester City anakoheshimishwa sasa mwanasoka huyo.

Haikuwa rahisi kwa fundi huyo wa mpira kupaa umbali mrefu namna hio bali juhudi, Uwezo na imani ndivyo vilimuongoza mpaka kutua pale Manchester city.

David Silva akiwa Valencia

Ilimchukua miaka 24 kufika hapo huku jasho, pumzi na nguvu vikipambania safari hio katikakati mwa viwanja mbali mbali nchini Hispania alipokuwa akiitumikia Klabu ya Valencia toka timu za vijana mpaka ile ya wakubwa.

Hayawi hayawi yakawa, mwaka 2010 Silva akamuaga baba yake kwa kumpigia saluti na kumuahidi kwenda kupambania timu na familia yake, Baba akajibu na kutoa baraka zote kwa Silva na fundi huyo rasmi akajiunga na Wananchi hao wa jijini Manchester ‘The Cityzen’.

Jezi namba 21, mgongoni akaanza kupambana kiasikari, kila alipojaribu kukata tamaa aliiona sura ya mama yake ikimwambia wewe ndiye shujaa wetu huku akikumbuka maneno ya baba yake siku wanaagana.

Akajawa na hasira zisizoumiza, nguvu ya kupambana ikatawala misuli yake, akili na ubunifu wa kusakata kandanda ukajaa akilini kwake, kilichofuata hapo ni historia.

Miaka 10 ndani ya Machester City Silva anatangaza kukivua kitambaa cha unahodha na jezi ile ya bluu bahari anakwenda kutafuta maisha mengine, mkono wa kwa heri anaunyosha juu pale Etihad mashabiki wanaumia lakini muda huo huo wanatoa chozi la furaha na heshima kwake.

Mguu pande mguu sawa saluti inapigwa amri inatolewa lijengwe sanamu la Silva nje ya uwanja wa Etihad kama ishala ya kumbukumbu kwa kiunga huyo machachari aliyeishi na City kwenye shida na raha zote pasi kuiacha.

Kapunguze majukumu ‘ankoo’ tutakukumbuka kwa pasi zako za mwisho, uongozi kwa wachezaji wenzako pasi kusahau upendo na kiwango chako bora uwanjani.

Sambaza....