Kombe la Dunia

Ghiggia, ‘Jini’ aliyepeleka balaa Maracana 1950

Sambaza....

Sehemu ya Makala hii kwa mara ya kwanza ilitoka katika gazeti la Mwananchi-Spoti Mikiki mwaka 2013. Patrick Mwasomola, wa FQ Hotel Airport Dar es salaam, Tanzania ameirudia tena kwa wakati wa sasa na kuiongezea vitu, karibu uisome ndani ya kandanda.co.tz.


Mechi ya fainali ya Kombe la Dunia 1950 kati ya Brazil na Uruguay ndiyo inayokumbukwa sana na mashabiki wa soka nchini Brazil.

Ni miaka 63 (2013) tangu Alcides Ghiggia alipofunga bao la ushindi la Uruguay dhidi ya Brazil kwenye uwanja wa Maracana mjini Rio De Janeiro, Brazil na kuhatarisha maisha ya mashabiki 200,000.

Ghiggia akifunga bao lake pale Maracana

“Wote walikuwa kimya. Umati ulizizima. Ilikuwa Kama ni watu waliokuwa hawapumui,” alisema Ghiggia akikumbuka mechi ya fainali ya kombe la dunia dhidi ya Brazil mwaka 1950 ambayo iliisha kwa Uruguay kushinda 2-1, akiwa amefunga bao la ushindi.

Ghiggia, nyota wa zamani ambaye sasa ana miaka 86, (2013 ni mchezaji pekee aliye hai kati ya wachezaji wa kikosi kilichotwaa ubingwa mwaka huo. (Ghiggia alifariki mwaka 2015).
Bado anakumbukwa kama mtu mashuhuri ambaye aliudhi mashabiki wengi zaidi katika historia ya kombe la Dunia.

Wachache waliamini Uruguay itashinda, lakini hakukuwa na raia yeyote wa Brazil aliyeamini katika hilo.
Siku moja kabla, gazeti la mji wa Sao Paulo, Gazeta Esportiva liliandika: “Kesho tutaifunga Uruguay!”
Gazeti la Rio De Janeiro la O Mundo lilichapisha na kuweka picha kubwa ya kikosi cha Brazil ikiwa na maelezo yaliyosomeka: “Hawa ndio mabingwa wa dunia.”

Maracana miaka hiyo

Baada ya kipindi cha kwanza kumalizika kwa suluhu, dakika ya kwanza ya kipindi cha pili, Brazil ilipata bao la kuongoza lililofungwa na Friaça, lakini dakika ya 66, Juan Alberto Schiaffino aliisawazishia Uruguay baada ya kuunganisha krosi safi ya Ghiggia katika eneo la hatari.
Bao hilo lilinyamazisha sehemu kubwa ya mashabiki. Lakini wakati michuano ya wakati huo ikiwa inaendeshwa kwa mtindo wa ligi, sare ya aina yoyote ingeipa ubingwa Brazil.

TAARIFA:

Michuano ya Kombe la Dunia haikumpa utajiri wowote Ghiggia, lakini siku zote bado anakumbukwa. Sura yake ilikuwa ikitumika katika stempu alipotimiza miaka 80 ikiwa imeandikwa “Ghiggia nos hizo llorar”
(Ghiggia Umetutoa Machozi), na nyayo ya mguu wake imewekwa katika kumbukumbu ya wanasoka wakubwa duniani kwenye Uwanja wa Maracana. Wengine ni Pele, Eusebio na Franz Beckenbauer.

Ghiggia, ambaye alikuwa winga tishio wakati huo na mwenye uwezo wa kukimbia na mpira kwa kasi, anasema: Nilichukua mpira wingi ya kulia, nilimpita Bigode (aliyekuwa beki wa kushoto wa Brazil) na kuingia katika boksi.
“Mlinda mlango (Moacyr Barbosa) alidhani kwamba ningepiga krosi, kama ambavyo nilifanya katika bao la kwanza, hivyo aliacha nafasi kati yake na nguzo ya kwanza. Nami niliona ni nafasi, na nikapiga shuti hafifu kuupenyeza mpira na kuwa goli.”
Tukio hilo lilitokea dakika 11 kabla ya kipenga cha mwisho, bado linakumbukwa hadi leo katika ardhi ya Brazil.

Ghiggia akifanya yake

Kwa Brazil, matokeo hayo yalichukuliwa kama janga la kitaifa. Mechi hiyo inabaki kuwa huzuni kwa taifa zima na ilipewa jina la “Maracanazo” kwa Kireno cha Brazil na “Maracanaco”, kwa Kireno lenye maana “Balaa la Maracana”.

Kutokana na kipigo hicho mwandishi mmoja wa Brazil, Nelson Rodrigues, aliandika katika gazeti kuwa hilo lilikuwa janga lao na kulipa jina la “Hiroshima yetu”.

Kwa kujiona wakosaji mbele ya mashabiki wao, nyota wengi waliokuwa katika kikosi cha Brazil wakati huo waliamua kustaafu soka, wakati wengine hawakuitwa tena timu ya taifa.

Wakati huo wakitumia jezi za nyumbani zenye rangi nyeupe na bluu, Brazil waliamua kubadilisha haraka rangi yao na sasa wanatumia njano na kijani.

Brazil kamwe hawawezi kusahau kipigo hicho cha fedheha nyumbani.

Barbosa akiwa kwenye goli lililohusika na Ghiggia

Kipigo hicho hakikumtoka akilini Barbosa, aliyekuwa kipa wa Brazil. Licha ya kuwa na maisha marefu ya soka katika klabu ya Vasco da Gama ya Rio de Janeiro, alicheza tena mara moja katika timu ya taifa. Wenzake walimsafisha.
Baada ya kuzuiwa kukiona kikosi cha Brazil kilichokuwa kikijiandaa kwa michuano ya Kombe la Dunia1994, aliwaambia waandishi wa habari: “Nchini Brazil adhabu ya juu ya kifungo ni miaka 30; nimetumia miaka 44 kutumikia adhabu bila ya kufanya kosa.”

Ghiggia alisema anafikiri Barbosa analaumiwa kimakosa. “Nilizungumza naye miaka michache baada ya kombe la Dunia. Nilimwambia soka ni wachezaji 11 kwa 11.
“Makipa siku zote wanakuwa hawathaminiki. Unaweza kucheza vizuri katika dakika zote, ukifungwa unaingia matatizoni kwa bao moja. Beki hakunikaba sasa kwa nini analaumiwa yeye?”.

Barbosa alifariki mwaka 2000.

Hakuna mechi inayozungumziwa zaidi nchini Brazil kama ya Maracanazo. Kila siku ya Julai 16 inakuwa siku ya kukumbuka na kuvuta hisia za nyuma.
Mwaka jana (2012) kumbukumbu ya kutimiza miaka 62 ilikumbukwa kwa machapisho yaliyosomeka “Dossier 50,” ikiwa ni kumbukumbu ya kipigo cha nyumbani miaka hiyo.

Ghiggia anazungumzia hilo kwa kusema kuwa kuna wakati anajihisi kama ni “jini wa watu wa Brazil.”
Siku zote nakuwa pamoja nao katika kumbukumbu.” alisema.

Licha ya kuwapa machungu yasiyosahaulika, raia wa Brazil bado wanamuona shujaa huyo wa zamani kama mtu maarufu duniani na kumheshimu siku zote.

ALIKOTOKEA:

Alcides Edgardo Ghiggia Pereyra alizaliwa tarehe 22 Desemba mwaka 1926 na kufariki tarehe 16 Julai mwaka 2015.

Ghiggia kwa nyakati tofauti alizichezea timu za Taifa za Uruguay na Italia kama winga wa kulia.

Klabu alizopata kuchezea ni pamoja na Peñarol na Danubio za nchini kwao Uruguay na A.S. Roma na A.C. Milan za nchini Italia.
Mwaka 1952, Ghiggia aliondoka klabu ya Penarol na kuwa mchezaji wa kwanza kutoka Bara la Amerika kucheza Ulaya aliposajiliwa na AS Roma ya Italia.

Ghiggia aliamua kuwa raia wa Italia mwaka 1957, ambapo mwaka 1963 alirudi Uruguay.

Kama tulivyoona hapo juu kuwa mwaka 1950, Ghiggia, wakati huo akiichezea Uruguay, alifunga bao la ushindi dhidi ya Brazil katika mechi ya fainali ya mwaka huo maarufu kama ( Maracanazo).

Roberto Muylaert analifananisha goli hilo katika sinema yake ya Black and White na sinema ya Abraham Zapruder ya Chance Images katika mauaji ya Rais Kennedy wa Marekani jijini Dallas: anasema kwamba goli na risasi iliyomuua Rais wa Marekani “vilikuwa na uelekeo mmoja, mwendo unaofanana na kasi isiyosimamishika. Hata vumbi lake lilifanana liliporuka juu, hapa kwa bunduki aina ya rifle na kule kwa mguu wa kushoto wa Ghiggia.”

Kama tulivyokwishasema kuwa mechi ile ya fainali inachukuliwa kama mojawapo ya jambo lililowasikitisha na kuwanyong’onyesha mamilioni ya Wabrazi katika historia ya mchezo wa mpira wa miguu; Ghiggia alikuja kusema baadaye kuwa “ni watu watatu tu ndiyo waliweza kuinyamazisha Maracana. Watu hao ni Mwanamuziki wa Kimarekani Frank Sinatra, Papa, na mimi.”

MIAKA YAKE YA BAADAYE:
Familia ya Ghiggia ilikuwa ni ya kizazi cha Ticinese kwa asili wakitokea Sonvico.
Miaka yake ya mwisho, Ghiggia aliishi nyumbani kwake huko Las Piedras, Uruguay. Alifariki tarehe 16 Julai mwaka 2015 katika hospitali moja binafsi jijini Montevideo akiwa na umri wa miaka 88. Coincidentally, miaka 65 ya kumbukumbu ya Maracanazo toka tarehe ile ya 16 Julai mwaka 1950 alipofunga bao la ushindi dhidi ya Brazil.

Wakati anafariki, yeye ndiye aliyekuwa mchezaji pekee wa zamani wa mabingwa hao wa Kombe la Dunia aliyekuwa amebakia.
Vilevile Ghiggia ndiye mchezaji wa mwisho aliyekuwa amebakia wa vikosi vya pande zote mbili vya Brazil na Uruguay vilivyoshiriki katika fainali ile ya kihistoria ya mchezo wa Kombe la Dunia mwaka 1950.


Sambaza....
Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.