EPL

Guardiola anapotuumbua wanafiki wake

Sambaza....

Mbele ya hadhara Pep Guardiola ameamua kutuumbua wanafiki wake. Ametuumbua
na kutuziba midomo kwa vitendo uwanjani sio kwenye ndimi kama sisi tulivyomuhukumu awali. Najisikia aibu kuwa mmoja wao.

Pep na Manchester City yake wanafanya vyema. Pep mwenyewe haonekani kujali
kwa maneno tuliyowahi kumkosoa nayo siku chache alivyotua uwanja wa Ndege wa Jiji la Manchester kuifundisha City.

Kabla sijapiga goti chini na kukabidhiwa mke wiki mbili zilizopita, ligi ya Uingereza ilisimama juma moja kupisha michezo ya timu za taifa.

Wakati ligi hiyo ikisimama, City walikuwa kileleni mwa ligi. Ligi ilivyorudi kila mmoja aliamini wakati wa City kudondosha pointi umewadia na timu za karibu yake kuisogelea. Lakini haikuwa hivi.

City walienda kuendelea pale walipoishia. Walienda ugenini kuwafunga Huddersfield Town, wakarudi nyumbani na kuzifunga Southampton, West Ham na jana wameifunga Manchester United ugenini. Timu ya ubingwa inakuwa na sifa hizi. Inashinda ugenini, inashinda nyumbani, bila kujali
inakutana na mpinzani wa namna gani.

Katika hili wanalolifanya City ni kama Pep anatuzaba kibao cha kelbu watu wengi tuliotumia kila ila kumkosoa na kujiaminisha kuwa hawezi kufanya kitu katika ligi ya Malkia. Masikini mawazo yangu.

City wako kwenye kilele cha ubora wao. Ukitazama timu yao inavyocheza ndiyo
utajua kwanini wapo pale walipo na timu nyingine ziko zilikokuwa. Ni kama
wameiteka ligi na wanafanya wanavyotaka.

Kuna timu ziko imara msimu huu. Chelsea na Manchester United ni timu zilizo imara, lakini
uimara wa City umetufanya tusizitazame United na Chelsea kama timu imara na tushajiaminisha ikitokea City wamekosa ubingwa itakuwa bahati mbaya.

Kwa mwenendo wa ligi unavyokwenda sasa, unadhani stori kubwa mwishoni mwa
msimu utakuwa City kupata ubingwa au kuukosa? Jibu ni kuukosa. Hivi sasa wanatuonyesha kila dalili ya kubeba taji.

Related image

Moja ya sifa ya kuwa bingwa ni kuzifunga timu unazogombania nazo ubingwa.
City wanalifanya jambo hili vizuri. Tayari wameshazifunga Liverpool,
Chelsea, Arsenal, United na wikiendi hii wanaenda kucheza na Tottenham Hotspurs.

Ni ngumu kushinda taji kama huzifungi timu unazogombania nazo taji lenyewe. Wakati huu City wanapitia njia sahihi ya kulishinda taji mwishoni mwa msimu japo ni mapema kubashiri wao ni mabingwa.

Gary Neville (Messi wa Uchambuzi Uingereza) aliwahi kusema kwa mbinu za Guardiola ni ngumu kufanikiwa Uingereza. Neville alikosoa mbinu hizo na kusema soka la Uingereza linahitaji wanaume wa shoka wa kupambana mechi ya kwanza mpaka ya mwisho.

Pep Guardiola na Gary Neville

Pep aliyasikia maneno haya na msimu huu amekuja tofauti. Ana kila aina ya mchezaji. Ana wachezaji wa kupambana, ana wachezaji wa kuulainisha mchezo ana wachezaji wa kumpa matokeo kwenye mechi ngumu na nyepesi. Aibu iliyoje Neville amegeuka bubu.

Pep amejenga timu isiyofikiriwa na wengi haswa ukizitazama rekodi zake huko
nyuma. Uwepo wa Mikael Aterta katika benchi la ufundi la City ni silaha muhimu kwa Pep. Aterta anaifahamu vyema ligi ya Uingereza na yeye ndiye anayechora ramani ya vita katika michezo ya City.

Image result for Pep Guardiola

Pep hakuwa mjinga kutaka kuwa na mtu aina ya Arteta katika benchi lake. Anafahamu uwepo wa Arteta utaifanya kazi yake ionekane nyepesi kama kuupaka mkate siagi kisha kuupeleka kinywani.

Muda huu Pep anapoamua kubadili mikao yake katika viti kadri anavyojisikia
tunapaswa kumuheshimu katika mabadiliko mapya ya soka lake. Awali alionekana kocha anayeweza kufundisha mpira laini pekee, lakini leo hii nae anakaba kama Jose Mourinho, lakini bado anakupa soka la burudani ndani yake.

Katika michezo 16 iliyochezwa na kila timu hivi sasa, City wamevuna pointi 46. Haijawahi kutokea katika historia yao tangu waanzishe timu. Tunaposema Pep na City yake wako kwenye kilele cha ubora tunamaanisha.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x