Shirikisho Afrika

Hivi ndivyo KMC walivyoingia kwenye mtego wa AS Kigali.

Sambaza....

Klabu ya KMC imekubali kichapo cha goli 2-1 katika mchezo wa shirikisho Afrika dhidi ya AS Kigali ya Rwanda, mchezo uliochezwa katika uwanja wa taifa Dar Es Salaam.

Magoli ya AS Kigali yaliwekwa kimyani na Rashidi Kalisa dakika ya 29 na Erick Nsabimana dakika ya 64 kabla ya Ndikumana kufunga goli la kufutia machozi dakika ya 85 kwa mkwaju wa penati.

Huu hapa ni uchambuzi wa timu zote mbili, hapa utapata kubaini mbinu za makocha wote wawili, game plan na wapi kulikuwa na mafanikio na wapi kulikuwa na makosa ya kiufundi kwa klabu zote mbili.

Kocha wa KMC, Jackson Mayanja aliingia na mfumo wa 4-3-3, akiwategemea Hassani Kabunda, salimu Aiyee na James Msuva kushambulia kwa kasi. Watatu hawa walijitahidi Muda wote kuwa katika eneo la hatari la AS Kigali.

Kabunda aliyekuwa akitokea kushoto aliungana na Amos Charles Kadikilo kuhakikisha wanalishambulia kwa kasi eneo hilo huku upande wa kulia, James Msuva ndiye aliyekuwa akitawala.

Kwa aina hii ya uchezaji inamaanisha kuwa, Mayanja aliingia na game plan ya kushambulia muda wote kwa kupitia krosi za ma wing backs hasa kwa upande wa kushoto.

AS Kigali walikubali kushambuliwa, kwani katika dakika zote tisini, AS Kigali walikubali kuchezea nyuma ya Yadi 30 kutoka golini kwao. Kocha wa Kigali alihakikisha timu yake inakuwa salama katika nyakati zote za kiuchezaji. As Kigali walionekana kuwa hatari zaidi katika kipindi cha mpito kuelekea kushambulia.

Mbinu kuu waliokuwa wanaitumia ni kuufinya uwanja wanaposhambuliwa na ndio maana Amos Charles alipata nafasi ya kupiga krosi chongo, lakini Kigali walitanua uwanja haraka baada ya kuunasa mpira.

Hii ina maana kuwa, AS Kigali walikubali kushambuliwa, lakini pindi wanapopata mpira walikuwa haraka kukaa katika maeneo hatari zaidi ambayo wachezaji wa KMC Wasingeweza kuyafikia katika sekunde chache za kipindi cha mpito.

GOLI LA KWANZA.

Kama nilivyokwambia awali kuwa KMC Walikuwa wakishambulia kwa kasi kupitia upande wa kushoto. Mashambuli hayo yalikuwa yakifanywa na beki wa kushoto kwa ushirikiano na Kabunda.

Katika kipindi hicho cha kushambulia, safu ya ulinzi ya KMC ilisalia na mabeki watatu huku eneo la beki wa kulia likibaki wazi. AS Kigali walitumia eneo hilo lilopo wazi katika kipindi cha mpito yaani transition na kutengeneza nafasi ya goli.

Goli hili lilifungwa kwa mchango wa makosa ya beki wa kushoto na kiungo wa ulinzi. Kiungo huyu alishindwa kumfanyia ‘marking’ mfungaji. Goli hili pia ni matokea ya KMC Kukosa ‘compactability’ ya timu kwa maana hakukuwa na muunganiko wa kutosha katika kikosi cha Mayanja.

KMC ilikuwa ikigawanyika katika vipande viwili. Kipande cha kwanza ni cha mabeki watatu, yaani beki wa kulia, na wakati wawili, kipande cha pili ni cha beki wa kushoto aliyepanda kushambulia akiungana na viungo na washambuliaji watatu. KMC Waliacha gap katikati lililotumiwa vyema na AS Kigali na kuandika goli. Hii  kitaalamu linaitwa POSITIONAL DESCIPLINE.

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika KMC Walishindwa kutumia faida ya kushambulia kupitia pembeni hasa upande wa kushoto. Amos Charles alipiga krosi zisizokuwa na faida pia James Msuva naye alishindwa kabisa kuwalazimisha mabeki wafanye makosa kwa upande wa kulia.

Kipindi cha pili hakikuwa na mabadiliko makubwa kwa maana ya game plan. Mayanja alisalia na mbinu yake moja ya kushambulia kupitia pembeni. Licha ya kumtoa James Msuva lakini KMC iliendelea kucheza 4-3-3.

Mayanja alimua kumzuia Amos Charles beki wa kushoto kupanda kushambulia na badala yake, Beki wa kulia Boniphace Maganga ndiye aliyepewa jukumu la kwenda kupiga krosi.

Katika kipindi hicho chote, AS Kigali walikubali kuwakaribisha KMC Katika eneo lao, yaani yadi 30 kutoka golini. Katika hili walihakikisha wanakuwa haraka kuisafirisha mipira kwenda mbele baada ya kuwapokonya KMC.

KMC wanapata goli la pili ikiwa ni matokeo ya Counter Attack iliyochangiwa na Offside Trick. Mabeki wa KMC Walijua mfungaji ameotea.

KMC Waliendelea kushambulia kupitia kushoto kwa Kabunda na kulia kwa Maganga. Makosa ya Amos Charles katika upigaji wa Krosi yalijirudia kwa Maganga na kuwakosesha magoli KMC kupitia washambuliaji wake Salim Aiyee, Kabunda na Vitalis Mayanga.

Kama bahati, KMC wanapata penati na kuandika goli la kwanza. Nasema kama bahati kwa sababu upatikanaji wa penati yenyewe haukuwa wa ufundi au wa kimbinu  japo penati hiyo ilikuwa ni matokeo ya High Pressing ya KMC dakika za mwishini na kumlazimisha mlinzi kufanya makosa na kuunawa mpira.

Kiujumla, KMC walifungwa kutokana na makosa matano ya kiufundi yaliyojitokeza, kwanza ni kwa mabeki wa pembeni kushindwa kupiga krosi zenye macho, hii dalili kuwahawakuzifanyia mazoezi.

 Pili KMC Walikuwa hawana mfumo unaoeleweka wa ukabaji, haijulikani walikuwa wanakaba nafasi au watu yaani Zonal Marking au Man to Man Marking.

Tatu, Mwalimu Mayanga aling’ang’ania mfumo mmoja wa ushambuliaji bila kubadilisha licha ya mbinu hiyo kufeli, mwalimu mzuri ni yule anayebadilika kutokana na hali ya mchezo itakavyokuwa yaani Mayanga hakuwa flexible.

Nne, KMC walishindwa kutumia faida ya uwanja wa nyumbani kwa maana, AS Kigali ndio waliokuwa waamuzi wa mchezo na wala sio KMC.

Tano, KMC ilikosa Compactability, wachezaji wa KMC walishindwa kutembea sawa, yaani kuanzia safu ya ushambuliaji hadi mabeki ukimtoa golikipa.

Mwisho kabisa KMC waliangushwa na aina ya pasi walizokuwa wakipiga. Walikuwa wakipiga pasi mfuato na sio pasi mguuni hii iliwafanya AS Kigali kuwahi kufanya Marking na zonal Coverage mapema na hii ndio sababu ya KMC kushindwa kukaa na mpira kwa japo sekunde 30.

Hadi kufikia hapo sina la ziada, kumbuka uchambuzi huu haujagusa mbinu zote zilizotumika, unaweza ukaongezea zaidi hapo chini kwenye sanduku la maoni.


Sambaza....
Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.