Sambaza....

Mshambuliaji Zlatan Ibrahimovic 36, alitolewa nje kwa kadi nyekundu katika dakika ya 41 kwenye mchezo wa ligi nchini Marekani baada ya kamera kumnasa akimzaba kibao beki wa timu ya Montreal Impact, Michael Petrasso.

Zlatan ambaye anaichezea timu ya LA Galaxy alitolewa nje baada ya kuonekana kwenye video akimzaba beki Petrasso ambaye alimkanyaga mguuni bahati mbaya. Wachezaji wote wawili walikwenda chini wakijaribu kumshawishi mwamuzi ambaye ilimbidi kuangalia marudio ya picha za video (VAR) na kujiridhisha tukio lilivyotokea na hivyo kumpa kadi nyekundu Zlatan na Petrasso akaambulia kadi ya njano.

Tukio la kuchapwa kibao

Hata hivyo, Katika mchezo huo uliofanyika jumatatu kwenye uwanja Saputo ulishuhudia LA Galaxy wakipata ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Ola Kamara katika dakika ya 75.

Ibrahimovic ambaye ni mchezaji wa zamani wa Manchester United na PSG mpaka sasa amefunga mabao matatu katika mechi saba ambazo ameshacheza na kuisaidia timu yake kushika nafasi ya pili nyuma ya Sporting Kansas City kwenye msimamo wa ligi hiyo ukanda wa Magharibi.

Sambaza....