Blog

Inashangaza sana!

Sambaza....

“TFF tumechanganyikiwa, yaani ni sawa na kuwa msibani halafu kuna mtu anakuja kukupora hata jamvi lile ulilolikalia” ni kauli ya Rais wa shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) alipoulizwa kuhusiana na kuchukuliwa kwa magari manne ya TFF na Mamlaka ya Mapato, (TRA)! Niseme tu bayana kauli hii ya Rais wetu wa TFF Ndugu Jamal Emily Malinzi ni moja ya kauli zilizoupasua moyo wangu usiku wa tarehe 31/3 kuamkia tarehe 1/4/2016.

Nimejiuliza maswali mengi sana bila ya majibu, nimekaa na kutafakari usiku wote sijaelewa hadi sasa, kama nilichokisikia kilikuwa ni sahihi kutoka kwa Rais Malinzi, mimi nafikiri ifike pahala sasa tujitafakari kabla ya kuchukua hatua za dhati kabisa kuomba ridhaa ya kupata Uongozi mahala popote pale, iwe kwenye serikali ya mtaa hata kwenye mashirikisho yenye kupata viongozi kwa njia ya chaguzi, Ndio nasema tujitafakari kwa maana ya kujiuliza kama tunatosha kwenye hivyo vyeo.

Kadhia kubwa iliyolikumba shirikisho la mpira wa miguu nchini mwetu la kutolipa kodi sio suala la jana wala la juzi, leo nataka kuliongelea kitaalamu baada ya kumsikia Mtaalamu wa Elimu ya Mlipa kodi wa TRA akizungumzia suala hili, kwa kusema TFF imeshindwa kuwasilisha malipo ya Kodi za Kodi ya ongezeko la thamani (VAT), Makato ya kodi yatokanayo na mshahara Pay As You Earn (PAYE) na mapato yakusanywayo kuendeleza Mafunzo ya Ufundi Skills and Development Levy (SDL) ukiangalia aina zote za Kodi hizo TFF hailipi yenyewe moja kwa moja kwa maana ya kulipa kutoka kwenye vyanzo vyao vya mapato la hasha bali ni Kodi ambazo wanatakiwa kuzikata/ kuzipokea kutoka kwa mlaji wa mwisho na kuziwasilisha kwa TRA wenyewe wakiwa kama Mawakala wa Kodi wa TRA, hapa unaweza kusema TFF wanapaswa kulipa asilimia tano tu (SDL 5%) ya mishahara yote wanayowalipa watumishi wake.

Baada ya kupitia vifungu vyote vya sheria za kodi na kujiridhisha juu ya makato yote na marejesho yote waliyotakiwa kuyafanya TFF nikajiuliza wapi kuna tatizo? Nikawauliza wahusika Je, TFF ina mtaalamu wa kodi kwa maana ya Tax Expert/ Consultant/ ama Officer? Nikauliza tena kama TFF ina Mhasibu/ Accountant ama Mkaguzi wa ndani wa hesabu? Nikauliza kama TFF ina Meneja wa Fedha/ Finance manager? Nikaambiwa TFF ina Director of Finance ambae ni CPA (T) holder, niliulizia hawa watu ili nijue kama TFF ina wataalamu hawa ili nipate kuwauliza Je, hawafahamu deadline ya Ku-file SDL & PAYE ni tarehe 7 ya kila mwezi…… hawajui tarehe ya Ku-file VAT ni mwisho wa mwezi wa kila mwezi wa pili? Kwa mfano VAT ya March tuna file mwisho wa mwezi wa April? Nilipoambiwa yupo DoF mwenye CPA nikajiuliza kwanini sasa Rais wa Shirikisho aseme wamechanganyikiwa? Hivi Rais anajua majukumu ya waajiriwa wake? Je, Rais ameshapata hata wasaa wa kukutana na watu wake kuwapa Dhima na Dira yake au Dhima na Dira ya taasisi anayoiongoza? Je hawa watumishi walioajiriwa TFF wana sifa stahiki kuwapo mahala pale? Je wanaifanya kazi yao kwa kufuata weledi?

Unajiuliza Rais anachanganyikiwaje kwa suala lililopaswa kufanywa na watu walioajiriwa kutokana na sifa zao, Rais unachanganyikiwa vipi na kitu ambacho kinaweza kufanywa kwa ufasaha kabisa hata na mwanafunzi aliyepo kwenye mafunzo ya Vitendo (field work) kwenye taasisi yoyote ile?

TFF kama shirikisho kazi yao kubwa (core business) ni kusimamia maendeleo ya mpira na masuala yote yahusuyo mpira wa miguu kuanzia ngazi ya chini kabisa soka la vijana hadi ya juu kabisaTimu ya Taifa, masuala ya kulipa Kodi, Masoko, wadhamini na mengineyo ambayo kwao ni (Non-core) wanatakiwa kuajiri watu wawe kama watumishi wao ama kuchukua kampuni kutoka nje ya TFF kuwafanyia hizo kazi na kuwalipa (Outsource), kama Rais wa Shirikisho angesema wamechanganyikiwa kwa kukosa kushiriki ama kuelekea kutoshiriki kwa fainali zijazo za AFCON nchini Gabon mwaka 2017 kwa mwaka wa 36 sasa, hapa ningemuelewa sana ila kwa hili naona Rais wangu hajui wapi pa kuanzia!

Anaajiriwa Mkurugenzi wa Fedha huyu ni miongoni mwa (Decisions maker) kwenye kampuni na linapokuja suala la Fedha kwenye Taasisi yoyote anapewa Uhuru mkubwa wa kufanya kazi yake kutokana na unyeti wa kazi yenyewe, sitaki kuamini kuwa Mkurugenzi huyu wa Fedha hajui umuhimu wa kufanya Returns za VAT/ PAYE/ hata SDL kiasi kwamba asifanye hiyo kazi kwa kipindi cha miaka 6 sasa na yeye bado yupo kazini tu!

Rais anasema amerithi madeni kutoka utawala uliopita, swali langu la msingi Je, rais kama Rais alifanya jitihada gani kuhakikisha wanalipa ama kupata maelezo juu ya malipo ya hizo kodi kutoka kwa watangulizi wake? Baada ya hapo Je, Rais aliwaambia nini watumishi wa taasisi yake juu ya malipo ya Kodi tofauti kwa Mamlaka ya Mapato? Maana pamoja na kusema walirithi madeni hayo ya kodi toka uongozi uliopita lakini hata Uongozi wake hadi sasa umebakiza mwaka Mmoja tu kabla ya Uchaguzi ujao wa viongozi nao hawajalipa chochote? Kuja kulalamika kuwa wamechanganyikiwa kwenye vyombo vya habari hii sio sawa.

TRA hadi inapofikia hatua ya kujua kuchukua mali za wadaiwa sugu wa kodi, basi njia nyingine zote za kidiplomasia zinakuwa zimshindwa kufanya kazi, Rais wangu Malinzi sin i miezi kama miwili tu ama mitatu toka TRA izifungie akaunti zenu za pesa? Je toka kipindi hicho mlichukua hatua gani? Kulisema hili suala ni sawa na kuwa na msiba halafu akaja mtu kuwapora majamvi mliyokalia naweza kusema sio sahihi kabisa! Miezi miwili ama mitatu sasa mmekaa kimya bila kufanya jitihada za makusudi kutatua matatizo yenu ya Msingi? Mmmmh!

Rais nikwambie tu ilikupasa usiku mmoja tu baada ya TRA kuchukua Magari ya Taasisi unayoiongoza kwa wewe kuita Mkutano na wanahabari na kuliongelea suala lile kwa kina ukiwa na Taarifa sahihi kabisa na sikungoja wanahabari wakudake juu kwa juu ukiwa kwenye masuala mengine ya utendaji wako wa kaziwa kila siku, au hata ungeandaa basi press release, kukaa kimya na kudakwa juu kwa juu na wanahabari ambao walikupa maswali ya kukutingisha hakika haikuwa sawa, na katika kukudhihirishia kuwa haikuwa sawa majibu yako tu yalitosha kunifanya kufahamu kuwa Rais wangu umetindikiwa na Msongo wa mawazo, ulipoteza kujiamini kiasi kwamba ukaanza kuwatupia Lawama waandishi wa habari za michezo, watangulizi wako na hata TRA kwa ujumla wake kitu ambacho hakikuwa sawa, ilifikia hatua kupitia maneno yako ulionyesha kuwa umekosa pa kushika.

Mimi nafikiri umefika muda sasa Rais wangu uweze kutofautisha vyeo vya Kisiasa na vyeo vinavyotaka weledi (professions) kwa mfano Mkurugenzi wa Ufundi anapaswa technically kuwa ni Mwalimu wa Mpira wa miguu (Kocha) hali kadharika Afisa Masoko awe na Elimu hiyo, hata masuala ya Kodi yanahitaji watu wenye ufahamu nayo kama Wahasibu, Maafisa Kodi na wengineo wenye elimu ya kodi, lakini Rais wangu kuelekea kwenye Kadhia hii ya masuala ya Kodi ilikupasa upate hata elimu mbili tatu kutoka kwa wataalamu wako wa kodi kabla ya kujitokeza hadharani na kutoa majibu yaliyokuwa yamejaa hasira na ukosefu wa ufahamu juu ya Kodi na kile ulichoulizwa.

Rais wangu Malinzi nikwambie tu, usipoteze muda chukua hatua stahiki muda ndio huu naamini wewe ukiwa kama Rais wa TFF na Mwenyekiti wa kamati ya utendaji ya TFF, na waajiriwa wote wa TFF wako chini yako naomba uwawajibishe wote wanaohusika na Kadhia hii kubwa ambayo imechafua taswira nzima ya TFF, Imechafua taswira nzima ya Familia ya Soka, na pia Imekuchafua wewe mwenyewe kama Mkuu wa Familia hii ya Soka, ukishindwa Mkuu wangu kuchukua hatua kali juu ya Uzembe huu usiovumilika nikuombe tu kwa kutunza heshima yako na ya taasisi unayoiongoza na familia ya soka kwa ujumla wake ujiuzulu tu maana hakuna namna nyingine, kwani hao watumishi wa TFF wameajiriwa kwa kufuata vigezo vipi? Wana sifa zipi? Baba fukuza wote pale urudishe heshima ya TFF na Heshima yako.

Usichanganyikiwe kwa jambo ambalo umewaajiri watu unaowalipa mamilioni ya shilingi walifanye kwa weledi mkubwa na wewe uweze kufanya yanayoigusa soka letu moja kwa moja halafu wao wanashindwa kutimiza majukumu yao na kusababisha shirikisho kushindwa kupiga hatua mbele na kuliletea Taifa maendeleo.

-Eric Zomboko (Dizo Moja)

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x