Blog

Juma Mgunda ni Pitso Mosimane wa Tanzania

Sambaza....

Kifupi nawapongeza sana Simba kwa uamuzi wao wa kumchukua na kumtumia kocha mzawa Juma Mgunda kuwa kocha wa muda kipindi hiki wakiwa katika mchakato wa kutafuta kocha mwingine baada ya kuachana na Zolan Maki.

Nimeona watu wengi sana wakikebehi na kutukana matusi kwa uamuzi huo, nimeshangazwa zaidi hata baadhi ya wanaojiita wachambuzi wa soka hapa Tanzania nao wakiwa kwenye kundi hilo la kukosoa uteuzi wa Mgunda pale Simba.

Watanzania tubadilike, watanzania tuanze kuviheshimu na kuvipa thamani vya kwetu. Ni aibu kuona makocha wote wa timu kubwa ni raia wa kigeni. Hao akina Pitso Mosimane kama wasingepewa nafasi ya kufundisha timu kubwa nchini mwao leo wasingekuwa na thamani. Walithaminiwa kwao na ndio maana leo hii wako kama tunavyowaona.

Huyu Juma Mgunda anapaswa kupongezwa, ndio anapaswa kupongozwa na kutiwa moyo ili kesho afikie sifa za akina Mosimane. Bila kuoewa nafasi kama hizi mnadhani Tanzania itawatoa wapi akina Mosimane wake? Kama Mgunda na Simba wanabezwa, wanatukanwa na kutolewa lugha mbaya mitandaoni mnadhani watafanikiwa?

Juma Mgunda (mwenye koti la bluu) akizungumza na wachezaji wake wa Coastal Union

Binafsi nikiwa shabiki wa Simba SC Tanzania natamani huyu Juma Mgunda apewe kazi hiyo moja kwa moja hata bila kujali matokeo atakayoyapa Malawi dhidi ya Nyasa Big Bullets. Naunga mkono utanzania kwanza. Naamini Mgunda akipewa kila atakacho ndani ya Simba anaweza shangaza Afrika na Dunia. Mgunda au Pep Guardiola mnene kwa jina la utani anaweza kuwa zaidi ya Pitso.

Tanzania kwanza, utanzania mbele. Mgunda ni Pitso Mosimane wa Tanzania.

Mungu ibariki Simba, Mungu mbariki Juma Mgunda. Ipo siku Tanzania itanielewa na Dunia itashangaa.

Sady A. Mwang’onda

Sambaza....