Blog

Kibabage ameenda, Chilunda amerudi

Sambaza kwa marafiki....

HIVI karibuni mastaa wetu wawili wamepishana Uwanja wa Ndege Mw. Nyerere. Nickson Kibabage ameondoka nchini kwenda Morocco, Shaban Chilunda amerudi nchini akitokea Hispania.

Hawajapishana sana umri wao. Kibabage yuko chini ya miaka 20. Chilunda yuko chini ya miaka 25. Ni vijana wadogo sana. Lakini mimi nikakaa nao nasimama kama kaka. Ni wadogo zangu.

Shaban Idd akiwasikiliza kwa makini wachezaji wa zamani wa Stars walioipeleka Tanzania Afcon mwaka 1980

Katika miaka 23 ya Chilunda usingetegemea kuona anarudi nchini kiurahisi kama alivyorudi. Angeendelea kupambana na Wazungu, lakini ameamua kurudi katika umri ambayo Jay Jay Okocha aliondoka Nigeria kwenda Ujerumani kwa rafiki yake. Tofauti yetu na wao inaanzia hapa.

Swali la kujiuliza kama Chilunda amerudi nyumbani na miaka yake 23, lini atakwenda tena? Ni swali gumu nililolikosea majibu yake. Chilunda alipaswa kukomaa huko aliko. Lakini kurudi nyumbani katika umri huu, amejirudisha nyuma bila kujijua. Atakuja kujua akianza kuzomewa Uwanja Taifa. Uamuzi huu atakuja kuujutia.

Kuna mastaa wengi nafsi zao zinawasuta hivi sasa. Walipata fursa ya kwenda nje, lakini walichokifanya wanakijua wenyewe. Leo hii wamebaki kuumia kimoyo moyo. Wanaona haya kutoka hadharani kukiri ujinga waliowahi kuufanya. Sijui kama Chilunda amelitazama hili.

Kibabage

Nilitamani kumuona Chilunda akikomaa nje akizurura sehemu moja hadi nyingine, mwisho wa siku akirudi nchini kwa maana ya kushindwa sehemu zote, hapo tutakusanyika kwenda kumpokea kwa Mw. Nyerere.

Tutamuona kama shujaa aliyetaka kufika sehemu fulani, lakini imeshindikana. Lakini amerudi nyumbani katika muda ambao Watanzania wengi tunataka kuona wachezaji wetu wakienda nje.

Shida kubwa inaanzia kwa marafiki wa wachezaji. Marafiki hawafanyi vyema kazi yao katika ushauri. Kibaya zaidi wachezaji wanawapenda mno marafiki wao kuliko washauri wa mambo mazuri.

Rafiki anayekuja na mtazamo wa kimaendeleo na ushauri anaonekana mshamba aliyepitwa na wakati. Stori nyingi za wachezaji na marafiki zao ni kuponda starehe. Nje ya nchi hakuna maisha haya ya uchawa. Mastaa wetu wakikumbuka starehe zao za Magomeni wenyewe wanatamani kurudi nchini. Akili zao zimeishia hapo.

Chilunda wakati akitambulishwa katika timu ya Zamani

Kuwa star mkubwa kama alivyo Mbwana Samatta si kazi ndogo. Mbwana amekubali kuacha vitu vingi na kuvichukua vichache vinavyomsaidia. Ni kama nyani mkongwe aliyekwepa mishale mingi, leo hii tunamuona kama mtu wa ajabu. Hana maajabu yoyote, lakini ameamua kujitambua tu.

Mastaa wetu wengi hawajaiamua hatima yao. Wamekuwa mastaa ni kutokana na Mungu kuwabariki vipaji, lakini katika maamuzi kichwani wanabaki ‘weupe’ kama sanda inayosubiri maiti.

Mwisho wa yote namkaribishaa Chilunda nyumbani. Karibu kaka. Karibu sana. Sihitaji kukwambia kuhusu Dar es Salaam ilivyo. Najua unaijua sana. Naombaa nirudie tena karibu. Katika muda huu ambao Kibabage amepishana na Chilunda, vipi nae tumwambie cha kufanya?

Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.