Sambaza....

Baridi limevaa ngozi yangu hii imekuwa kawaida sana siku hizi asubuhi kuwa na baridi kutokana na mvua, mvua ambayo imetusahaurisha kuhusu joto la Dar es Salaam

Joto ambalo limekuwa likitutesa kwa muda mrefu sana, mateso haya huwa ya nyakati fulani yenye majira ya joto.

Ndipo hapa huwa napenda kusema kila nyakati zina majira yake, nyakati zote hazina majira yanayofanana hata siku moja

Ndiyo maana pale Manchester United kulikuwa na nyakati za Sir. Alex Ferguson. Nyakati ambazo zilikuwa na majira ya mvua kwa kipindi kirefu.

Mvua ambazo zilileta neema kwenye mavuno ya Manchester United, tangu mwaka 1986-2013 ghala la Manchester United lilikuwa limejaa mazao mengi sana waliyovuna viziri.

Vikombe 38 chini ya Sir Alex Ferguson, kitu ambacho kiliifanya Manchester United ilijivunia nacho, kila shabiki wa Manchester United akawa amezoea raha.

Hakutaka kabisa shida ipite katika maisha yake kwa sababu furaha ndiyo nguzo ambayo ilijengwa na Sir Alex Ferguson

Nguzo hii ilisambaa mpaka kwa wachezaji wa Manchester United, kwao wao walijiona ni wachezaji ambao wamezaliwa kushinda.

Neno kushindwa lilikuwa mbali sana kwenye ubongo wao, kila mboni zao za macho zilipokuwa zinatizama mbele ziliona mafanikio makubwa ndani yao.

Walitaka vikombe, walikuwa na njaa ya mafanikio kiasi kwamba neno kukata tamaa halikuwepo ndani yao hata kidogo.

Ndiyo maana wengi wetu tulijua pale Camp Nou mwaka 1999 Bayern Munich anabeba kombe la ligi ya mabingwa barani ulaya.

Tuliona dakika zinaelekea ukingoni na Bayern Munich alikuwa anakaribia kwenda kulibeba kombe hili, lakini Sir. Alex Ferguson alituonesha namna ya kutumia kwa usahihi kila sekunde unayoipata kwenye maisha yako.

Dakika tatu (3) za nyongeza zilitosha kabisa kumhakikishia ubingwa tena akiwa na timu yenye morali kubwa ya ushindi kwenye mishipa ya damu yao.

Hawakukata tamaa, mechi kwao ilikuwa haijaisha na walikuwa wanasubiri dakika ya mwisho ili kuhakikisha mechi imeisha, kuwa kwao nyuma ya goli 1 mpaka dakika za nyongeza hakukuwavunja moyo kupigania ushindi , mwisho wa siku ikashinda kwa magoli 2-1 magoli mawili ambayo yalipatika dakika tatu za nyongeza

 

Dakika chache sana kwenye macho ya nyama lakini ni dakika nyingi sana kwenye mpira ndiyo maana jumamosi iliyopita Jose Mourinho alihitaji dakika tatu za magoli mawili ya Paul Pogba ili kuirudisha timu yake mchezoni.

Mashabiki wa Manchester City walikuwa wameshavua jezi zao na kubaki kifua wazi ili wazipeperushe kwa furaha ya kutwaa ubingwa.

Unatwaa ubingwa mbele ya mpinzani wako mkubwa? Hapana shaka ilikuwa furaha ya ajabu sana lakini ilikuja kuwa furaha ya muda

Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilitawaliwa na furaha kubwa ndani yao lakini dakika 45 za kipindi cha pili zilitawaliwa na huzuni kubwa sana.

 

Manchester United waliwaonesha mechi haiwezi kuisha kabla haijaisha, walicheza kwa kujiamini na kupigana ndani yao. Hawakuhofia tena kuwa mbele yao walikuwa wanacheza na timu bora

Ushindi ndicho kitu ambacho kilikuwa kinazunguka kwenye fikra zao, hatimaye roho ya Manchester United ya kipindi cha Sir Alex Ferguson ilirudi kwao na kufanikiwa kuzuia ndoto za wapinzani wao Manchester City

Hawakutaka kupata aibu ambayo ingedumu kwenye vizazi vingi , ndiyo maana kila walipokuwa wanamwangalia Sir Alex Ferguson jukwaani roho ya kupigana ilizidi kuwa kubwa ndani yao.

Sambaza....