Blog

Kwenye Giza la Kaseja hatukuwa Mishumaa yake

Sambaza....

Miaka mingi iliyopita, miaka ambayo Wafalme ndiyo walikuwa na sauti kubwa sana kwenye nchi za Afrika, hawa ndiyo walikuwa kila kitu. Waliheshimiwa sana, waliabudiwa sana na walikuwa MIUNGU ya duniani kwa wakati huo. Kila kitu kilikuwa kinaendeshwa kwa mdomo wao, ambayo ilikuwa Katiba na kila neno lililokuwa linatoka kinywani mwao ndiyo lilikuwa sharia.

Hakuna mtu yoyote ambaye alitakiwa kuendana kinyume na ndimi za wafalme hao. Ndimi zao zilikuwa za moto, zilikuwa zimetengenezwa na upanga wa nchi Kali, kilikuwa kitu cha kawaida mtu wa kawaida kutolewa Shingo yake kwa ulimi wa moto wa Mfalme. Hawa ndiyo walikuwa na hatimiliki ya kumiliki vitu vyote vizuri. Hakuna mwanachi wa kawaida aliyekuwa na uwezo wa kumiliki kitu chochote kizuri , iwe mwanamke mzuri, mifugo na vitu vyote vizuri.

Hii ndiyo ilikuwa maana halisi ya utawala wa kifalme. Kutawala vyote vizuri. Wananchi walijua Hilo ndiyo maana kuna Mfalme mmoja aliwahi kumiliki ndege wawili pekee ambao walikuwa wazuri kuzidi wote. Aliwaweka sehemu mbili tofauti , sehemu ya kwanza ilikuwa kwenye mti mzuri wenye matawi mazuri. Hili ndilo eneo la kwanza ambalo ndege huyo alikaaa. Eneo la pili ni kwenye ardhi. Ndege wa pili alitumia eneo hili kukaa chini kila ikifika usiku lakini kila jua lililopokuwa linachomoza alikuwa anaruka juu angani na kwenda kutafuta chakula. Hii ilikuwa tofauti sana na kwa ndege wa pili ambaye muda wote alikuwa amekaa kwenye tawi la mti, hakuwa na uwezo wa kuruka juu kwenda kujitafutia chakula. Kila uchwao akuwa anadhoofika afya yake kwa kukosa malisho mazuri tofauti na yule ndege ambaye alikuwa anaruka kila siku kwenda kujitafutia majani.

Ndipo hapo Mfalme alipohangaika kutafuta wataalamu wa mifugo na ndege kumtazama yule ndege kama alikuwa na tatizo. Madaktari wote wa mifugo walishindwa kabisa. Ndipo mkulima mmoja alidai anayo dawa. Na mfalme aliahidi kumpa zawadi kubwa kama akimwezesha huyo ndege kuruka juu na kwenda kujitafutia chakula. Asubuhi ya siku iliyofuata Mfalme alipoamka alimkuta ndege akiwa amesharuka tayari. Yule mfalme alimuuliza mkulima yule dawa ipi ambayo ilimponesha yule ndege?

Mkulima yule alisema alikata tawi ambalo yule ndege alikuwa amekalia muda wote. Ndipo hapo Mfalme alishangaa. Ndege akawa na uwezo wa kupaa tena. Tawi lilikuwa linamwaharibu yule ndege , tawi aliona ni eneo salama kwake kwa wakati huo (Comfort Zone) wakati alikuwa na uwezo wa kupaa mbali.

Na wakati yule ndege alipokuwa amekaa pale na kudumaaa kwa kukosa chakula watu wote walijua siku zake za mwisho zilikuwa zimekaribia. Walijua muda wowote ule angekufa mpaka alipokuja yule mkulima kumuokoa na kwa kukata tawi ambalo ndege yule aliona ni sehemu sahihi ingawa lilikuwa linamfanya adumae kwa kukosa malisho sahihi.

Hapana shaka Juma Kaseja alikuwa ameshakubali kufukiwa kwenye kaburi ambalo tulikuwa tayari tumemfukia wote. Alitumia muda mwingi sana kuwa gizani.Na kibaya zaidi tulimpaka oil nyeusi ili tu asionekane , hatukutosha na yeye kuwa gizani. Kwa sababu hatukutaka kumuona tena tulimpaka oil.

Na kibaya zaidi hatukutaka hata kumpa mshumaa kwenye giza lake. Ndiyo maana aliamua kukaa kwenye tawi ambalo aliona kwake yeye ni eneo zuri (Comfort Zone ) bila kujali alikuwa amedumaa.

Ni mkulima Ettiene Ndaragije aliyekata hilo tawi na kumwezesha Juma Kaseja kuruka kwa ajili ya kutafuta malisho ambayo Leo kanawiri kila mtu anamtamani wakati wa giza lake hatukutaka kuwa mishumaa kwake


Sambaza....
Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.