Sambaza....

George Lwandamina ni moja ya jina kubwa barani Afrika kwa sasa, huwezi kukwepa ukweli kuwa George Lwandamina aliwahi kufanya vizuri kwenye michuano ya vilabu barani Afrika akiwa na Zesco United ya Zambia.

Inawezekana kabisa hii ilikuwa moja ya sababu ambayo iliwashawishi Yanga wamchukue George Lwandamina ili wafikie mafanikio makubwa kwenye michuano hii ya vilabu barani Afrika.

Mafanikio ambayo yalianza kuonekana yanawezekana chini ya kocha Hans Van Pluijm baada ya Yanga kufika katika hatua ya makundi ya kombe la shirikisho.

Walitaka mtu wa kuwavusha pale, hapana shaka jicho lao lilidondokea kwa Mzambia George Lwandamina, hapana shaka jicho lao lilikuwa sahihi kwa asilimia kubwa kwa sababu George Lwandamina ndiyo alikuwa anatoka kuifikisha Zesco United katika hatua ya nusu fainali ya kombe la klabu bingwa barani Afrika.

Lazima ushawishike tu kuwa huyu aliyekuwa anakuja alikuwa ni kocha mzuri kulingana na mazingira ya sasa ya mpira wa sasa, kufika hatua ya nusu fainali kwa nyakati hizi ambazo kuna timu nyingi bora zilizowekeza ndani na nje ya uwanja lilikuwa jambo kubwa sana.

Swali kubwa lilibaki, anaweza akafanya makubwa kama aliyoyafanya Zesco United akiwa Yanga? Wengi hatukuwa na jibu la swali hili zaidi ya matumaini ambayo yalikuwa yamevaa mioyo yetu.

Subira ndicho kitu tulichokuwa tunakihitaji na tuliamua kuwa nacho kwa kipindi hicho. Mtihani wake wa kwanza ambao niliuona ni kwenye usajili wake wa kwanza kumsajili Emmanuel Martin.

Emmanuel Martin ndiye alikuwa mchezaji wa kwanza kusajiliwa na George Lwandamina, swali moja ambalo nilibaki nalo kichwani mwangu ni ƙmoja tu, ni kipi kakiona George Lwandamina kwa mchezaji ambaye kamuona kwenye mechi moja ya kirafiki?, au magoli mawili aliyowafunga Yanga kwenye mechi hiyo ya kirafiki ndiyo yalimpa nafasi Emmanuel Martin kwenye moyo wa George Lwandamina?

Sikutaka kabisa kuja na hitimisho la usajili huu, moyo wangu uliniambia Kiyumbi kuwa na subira yape macho yako kumtazama Emmanuel Martin.

Niliusikiliza na kuuelewa moyo wangu, nilijipa nafasi ya kumtazama Emmanuel Martin hatimaye nilipata sababu ya kwanini George Lwandamina aliamua kumsajili Emmanuel Martin kama usajili wake wa kwanza baada ya kuja Yanga.

Emmanuel Martin ni mchezaji ambaye siyo wa kiwango cha juu kama alivyokuwa Simon Msuva, hatishi sana na wala haogopeshi sana ila yeye ni mtumwa.

Hufanya kwa kujituma kila anachokuwa ameambiwa na kocha wake kukifanya. Hakuwa mchezaji wa kipaji cha juu ila alikuwa mchezaji ambaye kocha fulani huwa anaamua kuwa naye kwa ajili ya matumizi yake binafsi anayoyaona yanafaa kwake yeye kiufundi.

Ni aina ya wachezaji ambao kocha fulani hupenda kuwa nao kwa sababu fulani ambayo kocha huyo ameiona kwa mchezaji huyo, sababu ambayo itakuwa na faida kwenye mfumo wa kocha husika kwa wakati huo.

Tatizo huja pale kipindi huyo kocha anapoondoka katika timu hiyo, wachezaji wa aina hii huonekana kama wachezaji mzigo na hawana faida kwenye timu kwa sababu kocha ambaye alikuwa anajua kuwatumia wachezaji hawa anakuwa hayupo tena na timu.

Na ndiyo maana wengi wetu tulikuwa tunaiona Yanga ikitoa ushindani na kufanya vizuri tofauti na kikosi kikosi hiki walicho nacho kwa sasa, kwa sababu George Lwandamina alikuwa na wachezaji ambao alikuwa anajua kuwatumia ili afanye vizuri.

Kabla ya George Lwandamina kuondoka, Yanga walikuwa wanalingana alama na Simba katika msimamo wa Ligi kuu, lakini baada ya kuondoka michezo saba mpaka sasa hawajashinda na Yanga imeshapoteza ubingwa ambao awali walionekana wana matumaini ya kuutetea.

George Lwandamina aliwapa matumaini Yanga ya kubakiza kombe lao chini ya kikosi hiki hiki ambacho kinaonekana kina wachezaji wa kawaida, kikosi ambacho mpaka sasa hivi hakijapata ushindi wa aina yoyote tangu aondoke George Lwandamina.

Inawezekana Yanga ina matatizo ya kiuchumi lakini moja ya tatizo ambalo wengi hawalioni ni George Lwandamina kufanya usajili ambao yeye alikuwa na uwezo wa kuuishi na timu ikafanya vizuri chini ya matatizo hayo ya kiuchumi.

Matatizo ya kiuchumi kwa Yanga hayakuanza siku ya mechi ya Rayon sports, ila yalianza kipindi ambacho George Lwandamina yupo kama kocha mkuu.

Kilichokuwa kinambeba George Lwandamina ni yeye kuwa na wachezaji ambao alikuwa anajua kuwatumia yeye kama yeye.

Alijua kumtumia Yusuph Mhilu na akaonekana anaweza kuwa mchezaji bora kwa baadaye lakini baada ya kuondoka George Lwandamina , Yusuph Mhilu amekuwa siyo mchezaji wa kiwango kile kama alipokuwa chini yaa George Lwandamina.

Alijua kupata matokeo chini ya Emmanuel Martin, na aliweza kabisa kupata alama tatu muhimu kipindi alipomfanya Pato Ngonyani kama beki wa kati.

Hata Pius Buswita kwenye mikono ya George Lwandamina alifinyangwa vizuri akaonekana ni mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Yanga lakini alipoondoka George Lwandamina, Pius Buswita hana kiwango kama alichobahatika kuwa nacho chini ya Mzambia huyo.

Hii yote inatoa tafasri moja, George Lwandamina alikuwa na wachezaji ambao aliwaamini na alijua kuwatumia kupata matokeo mazuri licha ya sisi kuwaona kama ni wachezaji wa kawaida.

Ukawaida wa wachezaji hawa upo kwenye mikono ya makocha hawa waliobaki Yanga lakini ukawaida huu haukuwepo kwenye mikono ya George Lwandamina kwa sababu timu ilikuwa inapata matokeo chanya.

Ndipo hapo ninapozidi kuamini kuwa George Lwandamina alikuwa anajitengeneza yeye pembeni ya Yanga. Hakuweza kuitengeneza Yanga iliyosimama yenyewe , Yanga ambayo kocha yoyote angeweza kwenda nayo vizuri, usajili wa George Lwandamina ulikuwa ni kwa ajili ya afya yake na siyo kwa ajili ya afya ijayo ya Yanga.

Sambaza....