Blog

Namsubiri DIAMOND alete WCB kwenye MPIRA

Sambaza....

Usingizi umeshavunja urafiki na mboni zangu za macho. Mboni ambazo zimekataa kabisa kuvaa hili vazi la usingizi, macho yangu ni mepesi sana kila uchwao.

Viungo vyangu vyote vya mwili vinatoa ushirikiano kwenye macho yangu, tamaa ya usingizi haijafanikiwa kuuvaa mwili wangu. Niko macho kabisa , na sijabahatika kutamani kulala hata siku moja!.

Akili yangu inaniambia ni mapema sana kwangu Mimi kulala, nimekubaliana na akili yangu nimeamua kuipa ushirikiano na rasmi nimeamua kuisubiri dunia yetu ikamilike.

Hiii si timu ya Wasafi FC, Bali nitimu ya watangazaji wa Wasafi Sports Arena, vipi iwe ndiyo timu ya ligi kuu?

Dunia ambayo wakandarasi wetu hawajawahi kubahatika hata siku moja kumaliza kuijenga, ndiyo dunia ambayo wakandarasi walitumia tope kusimamishia nguzo za hekalu la Mbeya City.

Hekalu ambalo ramani yake ilikuwa yakuvutia na ilikuwa na ushawishi mkubwa sana ndani yake, kiasi kwamba asilimia kubwa ya watu walivutika na uzuri wa mchoro wa hekalu la Mbeya City.

Akili zetu zikatekwa , akili zikaamua kutoa ruhusa rasmi kwa mioyo yetu kuifutalia Mbeya City , kuipenda Mbeya na hata kuiunga kwa kiasi kikubwa sana Mbeya City.

Ikabatizwa timu ya kizazi kipya , kizazi ambacho kilisubiriwa kwa ajili ya kung’oa utawala wa masultan wawili , tuliamini hawa masultan wamekosa mvuto , haukuwa wakati wao kutawala , wengi tukashiriki mageuzi ya kuubeba utawala kutoka karikaoo kuupeleka Mbeya.

Tulitumia nguvu mno, Mbeya City ikawa inajaza mashabiki , wadhamini wakavutika kuwekeza kwenye timu ya kizazi kipya , bahati nzuri hata uwanjani walishinda mechi zao.

Mbeya City ile yenye makali

Nguvu zetu zilikuja kuangushwa na ujenzi ujenzi wa hekalu Lao , hekalu ambalo awali lilikuwa bora na zuri sana kwenye ramani lakini walipoanza kujenga walitumia tope kwa ajili ya kusimika nguzo za kubeba hekalu hilo.

Hata alipokuja Singida United naye aliichukua ramani ile ya Mbeya City kama ilivyo na kibaya zaidi aliamua kubeba na utaalamu wa ujenzi wa Mbeya City na yeye akaamua kutumia tope kusimikia nguzo za hekalu yao.

Wote wawili hakuna aliyefanikiwa kutufikisha sehemu ambayo tulikuwa tunatamani , sehemu ambayo ndiko ilipo dunia yetu , sehemu ambayo mpaka sasa mboni za macho yangu zimeshindwa kupata usingizi mpaka dunia hii itokee.

Sehemu ambayo hata Azam FC wameshindwa kutufikisha licha ya kuwa na vifaa bora vya ujenzi wa dunia hii lakini bado hawajaamua kupata wakandarasi bora.Muda unaenda , tutamsubiri mpaka lini Azam FC aamue kuwa na wakandarasi bora wa kujenga hekalu ambalo litakuwa dunia yetu ya kujivunia ?

Dunia ambayo itakuwa daraja la kusafirisha nje bidhaa wachezaji kwa ajili ya kwenda kucheza ligi shindani ?, dunia ambayo itatufanya Siku moja tushuhudie klabu moja hapa ikibeba kombe la CAF.

Dunia ambayo itatengeneza kikosi bora cha timu ya Taifa , unaikumbuka Hispania iliyoshinda kombe la dunia la mwaka 2010?, nusu ya wachezaji wa timu ya taifa ya Hispania kwenye mechi ya fainali walitoka Barcelona.

Unajiuliza kwanini ?, Barcelona waliamua kujenga dunia , dunia ambayo ilikuwa daraja la mafanikio mpaka kwenye timu ya taifa. Hapa ndipo ugumu wangu wa kupata usingizi unapoanzia.

Nawaza sana , lini tutapata mtu wa kutujengea dunia yetu ?, au tumsubiri Nassib Abdul aje kutujengea dunia yetu kama alivyofanikiwa kujenga dunia imara kwenye music ?

Leo hii Diamond kafanikiwa kubadilisha jina la bongo fleva na kuwa Wasafi Fleva. Amejenga timu imara kwenye music wake , timu ambayo Kila uchwao inabadilishana anga kwenda kuiwakilisha Tanzania.

Alifanikiwa kupingana na mawazo ya kuwa music haulipi yeye akaufanya biashara , leo hii ni mfanyabiashara bora wa music .

Tusubiri labda kesho atakuja na WCB kwenye mpira, augeuze mpira biashara , azalishe bidhaa nyingi ambazo ataziuza nje na kuja kutusaidia sisi.

Aweze kuwatengeneza wachezaji wetu kibiashara wawe na mvuto wa kibiashara mpaka makampuni mbalimbali yavutike kuwekeza kwenye majina Yao.

Bado niko macho , bado nasubiri namna ambavyo atakavyoweza kuwa na mtandao mkubwa wa mawakala kwenye mpira kama alivyofanikiwa kuwa na mtandao mkubwa kwenye music.


Sambaza....
Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.