Blog

Nani chaguo sahihi kiufundi: Tshabalala/Gadiel? Sehemu ya Pili

Sambaza....

Karibu tena katika sehemu ya pili ya muendelezo wa makala ya kiuchambuzi juu ya matumizi sahihi ya mabeki Gadiel Michael na Mohamedi Husseni katika klabu ya Simba hata timu ya taifa.

Katika sehemu tutaangazia sifa za kiujumla za beki yeyote yule, tutaangazia jukumu la msingi la mchezaji katika nafasi ya ulinzi na jinsi anavyotimiza majukumu yake kama mlinzi na wakati mwingine kama mshambuliaji.

Katika kuweka Mambo sawa, acha tuangazie kiufundi juu ya sifa za wachezaji hawa wawili na ni wapi anapaswa kutumika nani? Na kwa wakati gani? Kumbuka uchambuzi unazingatia vitu vikuu vitatu, ambavyo ni sifa ya mchezaji husika, Mbinu za Mwalimu na aina ya mechi.

Jukumu la msingi kwa beki yeyote yule ni kulinda, ndio maana huitwa Mlinzi na wakiungana pamoja huitwa safu ya ulinzi. Majina hudhihirisha kuwa jukumu mama la Gadiel na Tshabalala ni kulinda.

Katika hili nitaangazia Mambo mbalimbali ambayo kiufundi ni majukumu ya kiulinzi katika timu. Mambo haya ndio yanayomtofautisha mlinzi na mshambuliaji katika ufanisi wao.

1. kuingilia mchezo (interception)

Katika hili Tshalala na Gadiel wote hawako vizuri, kwa maana hakuna mwenye rekodi nzuri katika hili. Sababu kuu ni aina ya soka wanalocheza, yaani hakuna hata mmoja mwenye tabia ya kuingia katikati na kuwa kama kiungo wa ulinzi.

Ni nadra sana kumuona Tshabalala akizuia pasi mpenyezo, ni nadra sana kumuona Gadiel akizuia shambulizi lililokuwa linafikia ukomo kuandika goli.

Ni rahisi sana kwa beki wa pembeni kufanya interceptions kama atachezeza kama false full back, kwa maana timu inapopokonywa mpira katika nusu ya eneo la mpinzani yeye awe kiungo wa kati, akiiacha safu ya ulinzi ikiwa na mabeki watatu.

Hivi ndivyo Mu Ukraini Oleksandr Zinchenko anavyotumiwa na Pep Guardiola pale Man City. Zinchenko huwa kiungo wa ulinzi kuungana na Fernandinho wakati timu pinzani inapoanza kusafiri na mpira  kuelekea kwa man City, kisha hurudi kwenye nafasi haraka Man City inaposhambuliwa kwa kasi, hii Humsaidia kuzuia mashambulizi mengi kuelekea langoni mwake.

2. Tackling.

Tafsiri nyepesi ya msamiati huu ni kumpokonya mpira mchezaji wa timu pinzani hasa kipindi cha kushambulia.

Kanuni kuu inayoongoza tendo hili uwanjani ni kuanza kuupata mpira kwanza kabla ya kumgusa mchezaji, tackle huhesabika kama faulo endapo mchezaji ataonyesha nia ya kumzuia mchezaji na sio mpira.

Ni wachezaji wachache sana wenye uwezo wa kucheza tackle zenye mafanikio. Katika hili Mohamedi Husseni ni mzuri zaidi, kwa maana kati ya tackle 5 atakazocheza mbili huwa ni sahihi, tatu huwa ni madhambi tofauti na Gadiel. Bila shaka wachezaji hawa sio wazuri kucheza tackling.kwanza ni sababu ya vimo vyao. Tshabalala na Gadiel wote ni wafupi kwa maani hiyo ni vigumu sana kwa wao kuwa na makadilio sasa ya kufanya tackling hasa slide tackling. Lakini katika hili Tshablala ana afadhali kuliko Gadiel.

3. Kumiliki Mpira  bila kupokonywa.

Katika hili wachezaji wote wako vizuri lakini Tshabalala amemzidi Gadiel. Sababu zinazombeba Tshabalala ni uwezo wake wa kumuhadaa mchezaji kwa kupiga chenga na hata kupiga pasi.

Katika mpira ni vigumu sana kumpokonya mpira mchezaji mwenye uwezo wa kuitikisa vyema miguu yake.

Kutokana na umbo lako ni rahisi pia kupokonywa mpira akikabwa kwa nguvu na wachezaji wawili au mmoja lakini sharti amkabe hali ya kuwa hajui kama atakabwa kwa lugha ya kitaalamu huitwa ‘Blind side defending’.

4. Kuondoa mipira ya hatari.

Huku mtaani kwetu tunaita kuhanua, kuondoa au kusafisha. Kwa kimombo huitwa ‘Clearance’ kwa maana kuuondoa mpira katika eneo la hatari na kuupeleka eneo lenye usalama zaidi. Mara nyingi wanaofanya hivi huwa ni mabeki wa mwisho.

Katika hili, Gadiel amemzidi Tshabalala kutokana na ukweli kuwa Gadiel sio mtu wa mambo mengi sana uwanjani. Sifa kuu ya Gadiel ana sifa nyingi za ulinzi kuliko ushambuliaji hivyo hata maamuzi ya kubutua mpira kwenda mbele ni rahisi kumjia kuliko hata Tshabalala.

Tshabalala naye ni mzuri akiwa anatokea pembeni kuingia katikati. Tshabalala hutumia mbinu hii pindi beki wa kulia anapokuwa amepitwa na mpira huku mabeki wa kati wakiwa wamebanwa, Tshabalala huwa ndie beki pekee kuuondoa mpira katika eneo la hatari. Kinachombeba katika hili ni uwezo wake wa kurudi kwa haraka katika eneo lake la ulinzi pindi timu in aposhambuliwa hasa katika beki ya kulia.

Ukiachana na Sifa hizi kuu, mabeki wa pembeni kote duniani husifika kwa kushambulia pia. Yaani nikikwambia unitajie mabeki bora wa kulia na kushoto, hutomuacha Marcelo, Dani Alves, Kyle Walker, Danny Rose, endelea kuwataja hapo chini…

Mabeki wote hao hujengwa na sifa ya kushambulia kupitia pembeni yaani ‘Overlapping’, na kwa lugha ya kitaalamu mabeki hawa huitwa ‘WingBacks’.

Katika hili Tshabalala ana sifa zifuatazo, kwanza ana kasi, pili ana uwezo mkubwa wa kukokota mpira, anajua kupiga vyenga pia ni mzuri kuelekea katikati na pembeni ili kupiga krosi. Ili kurejea vizuri ni goli alilolifunga dhidi ya AS Club Vita klabu bingwa Afrika.

 Udhaifu wa Tshabalala katika hili ni upigaji wa Mashuti na kufunga, laiti angekuwa anajua kufunga basi angekuwa mchezaji tishio zaidi. Kwanini Marcelo ni beki bora wa kushoto katika kikosi cha dunia? ni sifa hizi alizokuwa nazo Tshabalala, lakini tatizo linakuja suala la kucheka na nyavu.

Kwa upande wa Gadiel naye ana sifa zifuatazo kwanza ana kasi ya kukimbia bila mpira, pili anajua kupiga mashuti na akafunga, kumbuka goli dhidi ya Azam na hata lile dhidi ya mbao, tatu ana nguvu za miguuni na mwili. Hivi vyote humsaidia katika jukumu la ulinzi na kushambulia pia. Udhaifu mkubwa kwake ni kupifa krosi, yaani krosi zake huwa hazina macho ni mara chache sana kumuona anapiga krosi nzuri.

Pili mpira wake sio wa burudani yaani kazi kazi, tofauti na Tshabalala anayecheza ‘Sexy Football’.

Hawa jamaa wawili wanasifa nyingi za kuwafanya waitwe wachezaji bora, lakini twende kwenye swali la msingi je ni nani na anapaswa kutumika wapi?

Kwa mujibu wa Sifa zao nilizokutajia hapo awali ni dhahiri kuwa, Tshabalala anapaswa kutumika katika mechi ambazo timu inasaka ushindi, kwa maana timu inatarajia huduma ya kushambulia na kulinda kutoka kwake.

Sifa kubwa inayombeba ni uwezo wake wa kutoka na mpira kuanzia eneo lake la ulinzi hadi kwenye yadi 18 za mpinzani. Tshabalala ni mzuri kwa ‘One-two’ za kwenda mbele kwahiyo anafaa zaidi kuanza mechi ambazo Simba inahitaji ushindi.

Gadiel ni kinyume chake, kwa sababu yeye ni mtu wa kazi na ana sifa nyingi za kiulinzi kuliko ushambuliaji basi aanze kwenye mechi ambazo Simba haihitaji sana kupata matokeo kupitia pembeni. Kwa maana katika michezo hiyo yeye atapanda katika vipindi maalumu vitakavyomruhusu kupanda lakini muda mwingi atabaki katika eneo lake na kumuacha Shomari Kapombe ashambulie kupitia kulia.

Kwa upande wangu acha niishia hapa, niandikie hapo chini niambie Kati ya Gadiel Michael na Mohamedi Husseini yupi unamkubali zaidi?

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x