Blog

Natamani kumuona HENRY akiwa kocha bora kama alivyokuwa MCHEZAJI.

Sambaza....

Dunia iliwahi kuwa sehemu kubwa ambayo vitu vingi vizuri viliwahi kuishi. Aliwahi kuishi Yesu kwenye dunia hii hii ambayo kila uchwao tunaamka na kukutana na jua.

Waliwahi kuishi WAFALME wengi sana, hata MFALME SULEIMAN Aliwahi kuishi kwenye dunia hii. Pamoja na kwamba tunapita ila nafsi yangu inajivunia na Mimi kuishi kwenye dunia hii.

Dunia ambayo iliwahi kumhifadhi Thierry Henry. Mshambuliaji bora kuwahi kutokea duniani. Huwezi kukosea kama ukisema Thierry Henry ni mmoja wa wachezaji bora kuwahi kutokea duniani.

Mchezaji ambaye aliweka rekodi nyingi sana kwenye kitabu cha kumbukumbu cha mpira wa miguu. Rekodi ambazo zinaishi na leo tunamkumbuka na kumheshimu kwa sababu ya rekodi hizo.

Tulimwelewa sana Thierry Henry, kwa sababu alibeba hatma ya kutufurahisha mioyo yetu. Alifanikiwa sana kwenye hilo. Alifunga magoli ambayo yalitufanya tuinuke na kushangilia sana.

Na kipindi kile anavuma wengine tulikuwa watoto wadogo sana, tulikuwa hatuna hata uwezo wa kujinunulia jezi. Na wazazi wetu hawakuwa na uwezo wa kutununulia hizo jezi.

Lakini fulana zetu tulizichakaza kwa kuziandika jina la Thierry Henry mgongoni mwetu. Kwa sababu tu alitokea kuwa kipenzi chetu.

Henry wakati akichezea Arsenal FC

Ndiyo huyu ambaye baadaye alikuja kuwa mfungaji bora wa Arsenal wa wakati wote. Anabaki kwenye kitabu cha Arsenal tena katika ukurasa wa mbele kabisa.

Ndiyo huyu ambaye mpaka sasa ndiye mfungaji bora wa wakati wote wa timu ya taifa ya Ufaransa. Anaendelea kubaki kwenye kumbukumbu za kitabu cha soka la Ufaransa.

Nchi ambayo iliwahi kuchukua kombe la dunia na kikosi ambacho Thierry Henry alikuwepo. Dunia inakumbuka sana hili tukio. Na dunia hii hii inawakumbuka wachezaji waliofanikiwa kutwaa taji hilo dunia.

Kwa kifupi Thierry Henry alifanikiwa kuwa “LEGEND WA MPIRA”. Mpira wa miguu unamkumbuka sana Thierry Henry kwa sababu aliwahi kuutendea haki sana huu mpira wa miguu wakati akiwa mchezaji.

Alionesha kila aina ya juhudi kipindi alipokuwa anaingia uwanjani. Alifunga sana kila alipopata nafasi ya kufanya hivo. Aliogopeka sana na mabeki wa timu pinzani.

John Terry , Beki wa kati wa zamani wa Chelsea aliwahi kusema kuwa kila alipokuwa anajua anaenda kukutana na Arsenal , usiku mmoja kabla ya mechi alikuwa anafikiria namna ya kumkaba Thierry Henry.

Aliwaza jinsi gani ambavyo angeweza kumzuia asiyelete madhara makubwa kwenye timu kwa sababu alizaliwa kwa ajili ya kufunga sana.

Na alikuwa anafunga sana, alichukiwa sana na magolikipa na ilifikia wakati hata magolikipa walipokuwa wanafungwa walikuwa wanatabasamu na kufurahia tu kwa sababu walikuwa wamefungwa na mchezaji bora kuwahi kutokea duniani.

Mchezaji ambaye aliwahi kubahatika kuwa chini ya makocha wawili wanaoheshimika sana na mpira wa miguu (Arsene Wenger & Pep Guardiola).

Hawa walimlea sana na inawezekana kuna mengi alijifunza sana kupitia kwa hawa wawili. Vitu hivi alivyojifunza ndivo ambavyo vimempelekea leo hii tukimuona sehemu ambayo ni tofauti.

Sehemu ambayo alizoea kumuona Arsene Wenger na Pep Guardiola akiwepo. Sehemu ambayo ni ngumu kwa sababu huwezi kuifananisha na sehemu ya ndani ya uwanja.

Unaweza kuwa mchezaji mkubwa ndani ya uwanjani lakini ukashindwa kuwa kocha bora kwenye benchi la ufundi. Hili eneo lilahitaji mambo mengi sana.

Pamoja na kwamba unatakiwa kuwa kocha wa kisasa, kocha ambaye anaendana na mbinu za kisasa lakini unatakiwa uwe na KIPAWA kikubwa cha uongozi.

Hapa unatakiwa uongoze kila aina ya wachezaji. Utakutana na wachezaji tofauti, ambao wametoka kwenye malezi tofauti. Malezi ambayo yamewajenga kuwa na tabia tofauti.

Tabia ambazo wewe kama kocha unatakiwa kusimama kama mzazi ili uweze kuishi nao na waweze kucheza kwa bidii na wafanikishe kuipatia timu matokeo chanya.

Hapa ndipo Thierry Henry unatakiwa kujitofautisha sana. Anatakiwa ajue ameingia kwenye daraja la ulezi. Daraja ambalo anatakiwa kuwa kiongozi mkubwa.

Kiongozi ambaye atasimama kama amri jeshi mkuu kwenye vita ili wapambane ipasavyo washinde vita. Natamani sana kumuona Henry kwenye hili eneo akifanikiwa. Ameanza vibaya, hii haifanyi kusema ameshindwa kwenye hili eneo. Tuusubiri muda , ndiyo utakuwa hakimu mkubwa wa eneo hili ambalo Henry kaamua kuwepo.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x