Sambaza....

Young Africans wameanza vizuri sana msimu huu mpya wa mashindano, mechi za mwanzo wamepata matokeo mazuri kitu ambacho ni kizuri kwa kocha mkuu kuangalia namna ambavyo wachezaji wanatekeleza kile anachowapa mazoezini.

Timu imeanza vizuri sana ijapo kuna wachezaji kadhaa pia ambao bado hatujaona wakipata dakika nyingi ndani ya uwanja! Na mfano mzuri ni Skudu Makudubela ambaye watu wengi wanasubiri kuona miguu yake itaongeza kitu gani kwenye kikosi cha Miguel Gamondi.

 

Jezi yake ndio ilipigiwa “Promotion” kubwa wakati wa usajili jezi namba 6 kuliko wachezaji wengine wote, hivyo watu wanasubiri kuona anapeleka kitu gani kwenye eneo la mwisho la Young Africans! Uwezo wa kuchezea mpira anao, kutengeneza nafasi, kasi nzuri na uwezo wake wa kupiga mbali pia ni mkubwa sana.

Max Nzengeli, Pacome Zouzoua, Nickson Kibabage, Yao Kouassi, Jonas Mkude na Hafidh Konkoni tayari wamecheza mechi za ushindani na tumeona dakika walizocheza kuna kitu wametoa kikosini!. Gift Fred bado hajapata dakika nyingi kama ambavyo ipo kwa Skudu Makudubela ambaye pia watu wanataka kumuona uwanjani.

Pacome Zouzoua.

Vizuri! Jezi namba 6 ilichukuliwa tofauti sana kabla hajatambulishwa hivyo lazima miguu yake iwape watu kile ambacho walitarajia kutokana na “Promo” ya jezi yake, miguu yake inahitaji kuongeza kitu ndani ya kikosi na sio kazi ndogo kupata dakika za kutosha sababu kuna watu ambao tayari wanacheza vizuri.

Young Africans kuna wachezaji wengi wazuri hali inayopelekea ushindani wa namba ndani ya uwanja kuwa mkubwa, hivyo ni lazima upeleke kitu cha ziada kwenye uwanja wa mazoezi ili kuwapa changamoto wenzio na kulishawishi benchi la ufundi likupe dakika nyingi za kucheza uwanjani.

Skudu Makudubela.

Skudu Makudubela kazi ni kwake kuyafanya matarajio ya Wananchi juu yake yakaishi na kuonekana kwenye miguu na ubongo wake ndani ya uwanja! NBC Premier League imeanza ukiunganisha na CAF CL ambayo tayari wenzake wamecheza mechi mfululizo.

Sambaza....