Sambaza....

Mechi tatu alama tisa, huu ni mwanzo mzuri kwa timu ya wananchi ” Yanga” na hapana shaka ni mwanzo mzuri kwa kocha Mwinyi Zahera. Kocha kutoka DRC Congo, kocha ambaye ana vyeo viwili kwa sasa, cheo cha kwanza ni kocha msaidizi wa timu ya taifa ya DRC Congo na cheo cha pili ni kocha mkuu wa Yanga.

Cheo cha pili ndicho ambacho kinaangaliwa na Watanzania kwa sababu yupo kwenye timu ambayo inatazamwa na watu wengi. Timu ambayo ina mashabiki wengi sana hapa nchini. Na hapana shaka ndiyo timu ambayo neno mgogoro ni kitu cha kugusa.

Hapa ndipo neno mgogoro lilipoanzia. Hata kitu kidogo tu kinaweza kuleta mtafaruku mkubwa sana ndani ya klabu. Na hii inatokana na sababu nyingi, moja ya sababu kuu ni kuwa na viongozi ambao hawana maono.

Viongozi ambao hawafikirii kesho ya timu, ila wanafikiria kesho ya tumbo lao. Viongozi ambao wako kwa ajili ya kutazama leo, ndiyo maana mipango yao huwa siyo madhubuti. Huwa ni mipango ya kuwafurahisha mashabiki tu.

Ni mipango “perfume” mipango ambayo hupulizwa kwa ajili ya kuondoa kwa muda harufu ya uozo walioanzisha wao!. Ndiyo maana ni rahisi na siyo jambo la kushangaza kuona kiongozi akisajili mchezaji bila kujali mahitaji ya benchi la timu husika.

Hapa ndipo huwa mwanzo wa migogoro ndani ya timu. Mchezaji analetwa na kiongozi, kwa makubaliano ya asilimia kumi (10%). Makubaliano ambayo yatamfanya kiongozi atamani kuona mchezaji wake akipata nafasi kila mara ili adhihirishe kwa watu kuwa alikuwa sahihi kumleta mchezaji huyo.

Kila aina ya mbinu zitafanywa ili mradi tu mchezaji huyo acheze. Na kuna wakati mwingine kocha mkuu atashinikizwa kumwanzisha mchezaji huyo. Hapa ndipo huwa mwanzo wa kiburi cha wachezaji wetu. Utamafanya nini wakati nyuma yake kuna mtu anayemlinda?

Huwezi kumfanya kitu, atafanya chochote kwenye timu kana kwamba timu ni ya baba yake. Atachelewa mazoezi, utaenda kumsema kwa viongozi wa timu lakini kesho yake utamuona mazoezini tena akiwa amechelewa tena huku akiwa hana adhabu yoyote anayoitumikia.

Utaamua kumweka benchi katika mechi lakini utapokea vita ya maneno ya vitisho kutoka kwa kiongozi husika. Siyo jambo la kushangaza kocha kuambiwa kuwa mchezaji huyo ameshikiria kibarua chako.

Hapa ndipo huwa mwanzo kwa makocha wengi kufanya kazi kinyume na taratibu zao za ukocha. Kwa makocha wasiojifahamu!, wasiopenda kazi zao!, watafanya chochote kulingana na kitu ambacho wanaambiwa na viongozi wa timu husika.

Watampanga mchezaji ambaye hayupo kwenye mipango ya kiufundi. Atacheza , timu itapata matokeo hasi na siku za kocha kuishi kwenye timu huesabika kwa kasi.

PosTimuPWGDPts
138296293
238272986

Ni makocha wachache sana ambao husimamia weredi wa kazi zao. Mchezaji kupata namba kutokana na anachokifanya kwenye mazoezi.

Kusimamia nidhamu ya mchezaji. Wachezaji wengi wa Tanzania wamekosa nidhamu kwa kiasi kikubwa.

Kuchelewa mazoezi ni kitu cha kawaida kwao, na wakati mwingine kuacha kuhudhulia mazoezi siku nne ni kitu cha kawaida sana!.

Hata kutojali muda wa kula kwao wao ni huona ni kitu cha kawaida, hata sisi mashabiki na viongozi wa mpira huona ni kitu cha kawaida.

Ndiyo maana macho yetu huwa na mshangao mkubwa kipindi ambapo tunaposikia mchezaji fulani kaadhibiwa kwa kosa la kuchelewa kula.

Hii ni kwa sababu tunachukulia vitu vya msingi katika ukawaida usio wa kawaida. Ukawaida ambao makocha ambao wanajua kazi zao kwao wao haupo. Hawachukulii vitu kawaida hata kidogo!, kwao wao mpira ni kazi kitu ambacho kwetu sisi bado hatujaanza kukiwaza.

Kwao wao nidhamu ni msingi wa mafanikio katika kazi ya mpira wa miguu kitu ambacho kwetu sisi hata hatujabarikiwa kuwa nacho!.

Ndiyo maana huwa tunawachukia sana aina ya makocha hawa. Hatuwapendi sana, hatuwaelewi sana na huwa tunawaona siyo rafiki katika mpira wetu.

Utaanzaje kumwadhibu kwa kumweka benchi Kamusoko, mchezaji ambaye sisi tunamuona ni muhimu ndani ya timu afu tukakuelewa?

Ni ngumu sana, lakini cha kushangaza Mwinyi Zahera anatembea kwenye ugumu huo huo, anafanya vitu ambavyo hatuvipendi.

Anafanya vitu ambacho siyo utamaduni wetu!, lakini yeye anafanya tu bila kujali tunajisikiaje.

Ramadhani Kabwili kwetu sisi tunamuona ni hadhina ya taifa letu kwa baadaye, lakini kwa Mwinyi Zahera anachokitaka ni nidhamu.

Haogopi kumwadhibu Ramadhani Kabwili kwa kuwa ni hadhina yetu. Yeye anataka kuikuza hadhina yetu katika misingi ya nidhamu bora.

Masikio yake hayasikii chochote, anafanya kile ambacho anakiona ni sahihi kwa kazi yake. Ndiyo maana hata kusema Papy Kabamba Tshishimbi haitendei haki nafasi yake haogopi.

Anajua majukumu ya mchezaji husika, na anaona mchezaji akiwa uwanjani hatimizi majukumu yake ipasavyo. Huyu ndiye kocha ambaye wachache sana wanaweza kumwelewa lakini huyu hataeleweka na wengi sana kwenye mpira wetu.

Mpira wetu hauitaji ukweli unaouma ila unahitaji uongo mtamu. Hakuna ambaye anaoenda kuupokea ukweli unaouma hasa hasa wachezaji wetu.

Na huu ndiyo huwa mwanzo kwa wachezaji wengi kumfanyia visa kocha husika kwa chuki zao binafsi ambazo hazijengi ili tu aondoke.

Kwa kifupi Mwinyi Zahera ni aina ya makocha ambao mpira wetu unatakiwa kuwa nao lakini ni aina ya makocha ambao watu wa mpira hawawapendi.

Sambaza....