Blog

Siku Gagarino alimpomsikitisha Morgan

Sambaza kwa marafiki....

Katikati ya miaka ya themanini, michuano ya Kombe la ilifanyika Visiwani Zanzibar. Nafikiri kama siyo Novemba mwaka 1985 basi ni Novemba mwaka 1986. Katika pambano moja muhimu sana, timu ya Tanzania Bara, ilikuwa inapambana na timu ya Taifa ya Uganda. The Uganda Cranes. Zamoyoni Mogella na Hamisi Thobias Gaga, katika michuano hiyo walitengeneza pacha moja ya hatari sana.

Katika mchezo huo, Zamoyoni Mogella kuna wakati alimpa Hamisi Thobias Gaga pasi moja maridadi sana, watoto wa mjini wanaita ” Bonge moja la Pande maridadi” na Gaga akiwa katika nafasi nzuri alikosa bao la wazi ambalo pengine huenda lingekuwa bao la ushindi na kuifanya Bara iende nusu fainali. Pambano hilo liisha kwa sare tasa ya bila kufungana kama kumbukumbu zangu ziko sawa. Kwa sare ile timu ya Bara ikawa imetolewa katika hatua ya makundi.

Gazeti la kila wiki la Mfanyakazi likaandika: “SIKU GAGARINO ALIPOMSIKITISHA MORGAN!” Pambano hilo lilitangazwa moja kwa moja na Charles Hilary, wa Radio Tanzania Dar es salaam ambaye siku hizi tupo Azam Media. Charles Hilary ni mzaliwa wa Zanzibar. Nami nililisikiliza pambano lile nikiwa kijijini kwetu Ndyonga, Tukuyu, kupitia Redio ya Bibi yangu Marehemu Bibi Tunsume Mungasulwa Kilasa Mwamafupa Mwaipaja “Gwamumpata, ” Gwammasoko”.

Jumapili iliyopita nilikuwepo uwanja mkuu wa Taifa katika pambano la wachezaji wanaocheza ligi za ndani kwa ajili ya michuano ya CHAN, kati ya timu yetu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars na timu ya Taifa ya Taifa ya Kenya, Harambee Stars. Sitaki kuongea mengi kuhusiana na pambano hilo la uwanja wa Taifa. Mimi siku Zote ni muumini wa timu zinazofanya mafunzo na mazoezi ya muda mrefu. Kwa timu yetu hii siwezi kulaumu kwa sababu Mwalimu ni mpya, wachezaji hawajakaa kwa pamoja kwa muda mrefu.

 

Kama kawaida Watanzania huwa hatunaga mipango ya muda mrefu tunataka leo leo tufanikiwe. Tunataka leo leo mambo yawe mazuri. Hatuna subira ya kusubiri kesho, keshokutwa. Hatuna utamaduni wa kusubiri kwa muda mchache kidogo ili kufanikiwa. Tunataka mambo leo leo. Hatuwezi kusubiri na kujiandaa na kuwa na utayari wa angalau miaka michache. Hatuwezi. Hicho kitu katika dunia ya soka hakipo.

Lakini ninachotaka kukisema hapa pamoja na mechi yenyewe ambayo kama nilivyosema sitaki kuizungumzia kwa kirefu, ni namna watanzania walivyo wajanja kila sekta kila sehemu. Nataka kusema kuhusu namna watanzania wanavyoweza kuhujumu kila sekta kwa kila nafasi wanayoipata. Mheshimiwa Rais wetu ana kazi kubwa sana.
Wahuni wamejaa kila sehemu kila kona kila sekta.

Jumapili iliyopita mapato ya uwanjani yamehujumiwa kwa kiasi kikubwa sana. Kwa nilichokiona Jumapili ni kuwa mapato yatakayotangazwa hayatakuwa halali. Hayatakuwa Halisi kwa sababu wizi mkubwa sana wa tiketi ulifanyika siku ya Jumapili na pesa nyingi kuingia mifukoni mwa watu wajanja wachache. Pesa nyingi zimeingia mifukoni mwa wajanja na bila shaka baadhi ya watu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini Tanzania kwa maana ya TFF wanashirikiana na baadhi ya watu pale milangoni kuhujumu mapato.

Nilifika uwanjani saa kumi kasoro dakika kumi. Lakini sehemu zote za kuuzia tiketi zikawa ama hazipo ama tiketi ni chache na tiketi nyingi hasa za elfu tatu tatu nyingi zikiwa mikononi mwa watu wakiziuza kwa shilingi elfu nne nne badala ya elfu tatu tatu Nje kulikuwa na misongamano ya kugombea tiketi kana kwamba uwanja umefurika lakini ndani ya uwanja, uwanja ulikuwa mweupe kabisa lakini vurugu yake mle magetini unaweza sema ndani sitapata siti.


Sisi tiketi ilimbidi tumtume mtu keko, akafika Hadi kariakoo akazipatia karume.” Manyanya Jr, Shabiki wa Azam Fc na Taifa Stars.


Baada ya kutafuta sehemu ziuzwapo tiketi na kuona watu wa selcom ni wachache na hawamo kwenye uzio kama kawaida yao, nikalazimika kununua tiketi kwa jamaa mmoja aliyekuwa na tiketi kibao za elfu tatu tatu akiziuza kwa elfu nne nne. Jamaa akaniuzia tiketi lakini nikamuuliza ndugu yangu tiketi hii ni halali kweli maana usije kuwa unaniuzia tiketi “fake” maana niliwahi kulizwa siku ya mechi na Uganda. Akasema kama hutaki acha yaani watu wote hawa wanunue tiketi hizi halafu wewe useme “fake”? Na kweli alikuwa nazo nyingi sana. Na watu wakawa wamemzonga ile mbaya wakinunua tiketi hizo.alipoulizwa na jamaa mmoja kama anazo tiketi za elfu tano tano akasema hana yeye alikuwa anauza za elfu tatu tatu tu. Nikanunua tiketi yangu na kwa vile foleni ya kuingia ndani haikuwa kubwa nikasema nikifika kwa mkaguzi wa selcom ikigoma kusoma narudi kumdaka! Maana nilikuwa nimemkariri sura na alikuwa na tiketi nyingi hivyo isingekuws rahisi kuondoka sehemu ile kwa wakati ule.

-Shabiki akiingia uwanjani kwenye moja ya mechi uwanja wa taifa.

Nikiwa ndani kwenye foleni karibu na mashine ya selcom nilimuona yule jamaa wa tiketi kaingia ndani kakaa pembeni karibu na mtu anayehakiki tiketi, akiwa anapeana ishara na mtu aliye ndani kabisa baada ya mkaguzi wa selcom. Nikajisemea moyoni “ikibuma” “namdaka” hapahapa! Kweli bwana nilipofika kwa mkaguzi wa selcom tiketi ikakataa kusoma. Mkaguzi akanigeukia akasema tiketi yako haisomi! Nikamwambia usinitanie aliyeniuzia ni huyo hapo mnayetaka kumpa tiketi nyingine maana zile mlizompa na kutuuzia kwa elfu nne ne amemaliza na huyo hapo anataka nyingine. Akaniambia kwa ukali haya bwana pita sasa unasimama nini? Mie nikapita nikawa ndani ya uzio. Nikajaribu kumfuata polisi mmoja mwenye nyota mabegani lakini jamaa mmoja akaniambia kuwa huwezi kusikilizwa kwa sababu hao wapo pamoja na polisi na wanajua nini kinachofanyika. Basi nikaamua kwenda zangu uwanjani.

Patrick Mwasomola, mwandishi wa makala hii akiwa uwanjani siku ya Tanzania vs Kenya

Walichokuwa wanakifanya hawa jamaa ni pale mtu wa kukagua tiketi wa selcom kuchukua tiketi na kupitisha kwenye mashine ikisoma wewe unapita na yeye anachukua zile tiketi zikiwa nyingi anampa mtu aliye ndani kwenye uzio naye anachana chache tu kisha zingine anampa yule jamaa aliyeniuzia mimi anaenda nje anaziuza upya yaani zinauzwa mara mbili. Je katika mageti yote ya kuingilia uwanjani watu kama hawa wapo wangapi? Wanahujumu mapato kiasi gani?
Pale milangoni walikuwa wanaziacha tiketi za VIP tu ndizo walikuwa hawazikusanyi.


Yaani jana (siku ya mechi) niliumia sana taifa!..yaani mkata tiketi anaulizwa tiketi za elfu3 anasema zimeisha halafu ukimpa elfu5 anakuprintia ya elfu3!..yaani nilishindwa cha kufanya hasira nilizokuwa nazo!..hivi tunawezeje kuyapata ktk mambo yetu ikiwa sisi wenyewe tunachapana kiasi!..nikajiuliza huyu mtu akipiga tiketi mia ana laki2!..kwa masaa yasiyozidi ma4!..tunawezaje kwenda namna hii!..wapo watu watauliza ili lina connection na kuangukaanguka kwa boko!..niwaambie tu ipo!..kubwa sana ipo!?” Ismail Mohamed , Shabiki wa Yanga na Taifa Stars. #KandandaChat


Nchi hii inapigwa kila sehemu, kila mahala. Nchi hii inapigwa kutoka kila sekta. Katika suala la tiketi pale milangoni bila shaka kuna watu walio nyuma ya hii kitu. Na bila shaka yoyote kama nilivyokwishakusema hapo juu ni baadhi ya watu wasio waaminifu kutoka Shirikisho la mpira wakishirikiana kwa ukaribu na wahudumu wa Selcom.

Electronic tickets kwa soka la Bongo it is nonsense!

Siku hizi Taifa Stars ikicheza huwa nnawafikiria jamaa zangu wale wawili, Pierre Liquid na Bongo Zozo na fujo zao zisizoumiza! Naamini hawa huwa wanaumia sana kuliko sisi wote.
Siku chache zijazo tutakwenda kurudiana na mashemeji pale Moi Kasarani. Je tutatoka? Je siku hiyo “GAGARINO ATAMFURAHISHA MORGAN” AU ATANSIKITISHA TENA KAMA ALIVYOMSIKITISHA SIKU ILE PALE UWANJA WA SHEIKH ABEID AMAN KARUME MJINI ZANZIBAR?
Let us wait and see as always anything can happen in the football match.


-Maka Patrick Mwasomola, Majohe,
Bwera Kwa Mchika, Gongolamboto, Dar es salaam Tanzania.


 

Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.