Blog

Simba isomeni hii barua ya Juventus.

Sambaza....

Ni barua ambayo imesambaa sana duniani kote !, siyo kwa nia mbaya, ni kwa nia nzuri. Nia ambayo ni chanya, nia ambayo inatakiwa kuishi muda mrefu.

Tuko kwenye ulimwengu ambao moyo wa mwanadamu uko karibu sana na neno kukata tamaa!. Ndiyo dunia tuliyo nayo.

Dunia ambayo imebeba watu ambao hukata tamaa mapema. Dunia ambayo imebeba watu wenye matamanio mengi kuliko malengo.

Ndiyo maana hukata tamaa hata kabla ya pambano lolote, kwa sababu tu hawana malengo na wamejaa matamanio tu kuliko malengo.

Huu ndiyo mstari mkubwa unaomtenganisha mshindi na mtu anayejaribu katika mbio za kutafuta mafanikio.

Siku zote bingwa huwa na malengo, ila mtu anayejaribu kuwa bingwa huwa na matamanio tu. Matamanio ambayo humfanya asiwe na uelekeo sahihi.

Mbio zake zinaweza zikawa zenye kasi lakini zikakosa uelekeo sahihi. Akabaki mtu wa kuendeshwa tu bila kujua ni wapi mahali sahihi anapotakiwa kwenda.

Malengo hujaa kwenye kitabu cha bingwa, imani ya ubingwa huvaa moyo wa bingwa siku zote. Hakati tamaa hata siku moja.

Yeye anaamini kila sekunde ina nafasi kubwa sana katika maisha yake hapa duniani. Ndiyo maana Juventus wakaamua kuandika barua hii.

Barua ambayo ilianza kuandikwa katika nchi ya Hispania. Nchi ambayo kwa miaka ya hivi karibuni imetawala sana soka la ulaya.

Katika fainali kumi zilizopita za ligi ya mabingwa barani ulaya, timu za Hispania zimeingiza timu saba katika fainali kumi zilizopita.

Na zimefanikiwa kushinda fainali tano, nne zikienda na Realmadrid na moja ikaenda na Barcelona katika hizo fainali kumi zilizopita.

Huu ndiyo Ufalme wa hatari ambao ulikuwa umewekwa na timu za Hispania. Ufalme ambao uliwafanya kuingiza timu tatu kwenye robo fainali kwa mara ya sita mfululizo, ni msimu huu tu pekee wameingiza timu moja robo fainali tangu msimu wa 20012/2013.

Juventus waliondoka katika ardhi ya Hispania wakiwa nyuma ya magoli 2 dhidi ya timu ambayo inatoka nchi ambayo ndani ya misimu sita mfululizo imeingiza timu 3 robo fainali.

Hapa ndipo ugumu wa kwanza ulipoanzia. Kitabu chao kilianza na kurasa za kuogofya kweli. Kurasa ambazo zilipambwa na sifa za Diego Simione.

Kocha ambaye alizaliwa kwa akili ya kulinda tu. Yeye yuko tayari kulinda ndani ya msimu mzima bila tatizo lolote, ndivo alivyo na hii kazi ameifanikiwa sana.

Hata kabla ya kwenda Turin, Diego Simione alikuwa amepata cleansheets katika michezo mitano iliyopita, huku akiwa amefungwa magoli 8 pekee msimu huu.

Kikosi cha Simba kikiwa mazoezini.

Umeona kitu hapo ?, jaribu kufikiria unaenda kucheza na timu ya aina hii tena ikiwa na mtaji wa magoli 2 kwenye mikono yake na wewe unatakiwa kushinda zaidi ya magoli 2 ili kupita.

Hapa ndipo moyo wa kuwa bingwa ulihitajika, moyo wa kuwa na malengo kuliko matamanio ndiyo ulihitajika ili kumshinda adui imara kama huyu.

Sitaki kuzungumzia ubora wa Cristiano Ronaldo kwa sababu haitakuwa sawa kuwapa mfano huu Simba ilihali hawana mchezaji wa kariba yake.

Sitaki pia kuzungumzia ubora wa mbinu za kocha Maxi Allegri kwa sababu Patrick Assumes tutampa mzigo mzito kumfananisha naye.

Ila nataka nizungumzie vitu viwili ambavyo Simba wanaweza kuvichukua kwenye barua ya Juventus na wao wakavitumia vizuri.

Uliwaona mashabiki wa Juventus walivyokuwa kwenye uwanja wa Allianz Stadium?, walivyokuwa wanaaamini kupitia miguu ya vijana wao ?

Walivyokuwa wanawapa nguvu ya kupigana wachezaji wao ?. Muda mwingi walikuwa wanawapa nguvu na kuwaaminisha kuwa wanaweza kuvuka kikwazo hiki.

Hiki ndicho kitu cha kwanza ambacho nataka kuwaonesha Simba, mashabiki wa Simba wana nguvu sana kuwapa nguvu wachezaji wa Simba katika mechi ya As Vita.

Kitu cha pili ni mapokeo ambayo wachezaji wa Juventus walikuwa wanayapokea kutoka kwa mashabiki wa Juventus.

Walikuwa wanapigana zaidi kila walipokuwa wanasikia sauti za mashabiki kutoka jukwaani. Kwa hiyo kulikuwa na muunganiko mzuri kati ya mashabiki wa Juventus na wachezaji wa Juventus.

Pamoja na wachezaji wa Simba kupewa nguvu na mashabiki wao, wanatakiwa kutowaangusha mashabiki wao kwa wao kujituma zaidi ndani ya uwanja.

Shabiki ni mchezaji wa 12. Shabiki ndiye kiungo anayetengeneza nafasi ya ushindi, na wachezaji ndiyo washambuliaji wanaofunga magoli baada ya shabiki kutengeneza nafasi ya magoli.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x