Blog

Unataka kuanzisha klabu? ipande Ligi Kuu? Tazama hii..

Sambaza....

Kandanda ilitua katika bara la Afrika katika karne ya 19 na watu kutoka Ulaya, na mchezo wa kwanza ukichezwa katika bara hili mwaka 1862, kwa mujibu wa taarifa za kihistoria kuhusu kandanda barani Afrika. Mwanahistoria Peter Alegi aliwahi kusema “Ulisambaa haraka sana kupitia shule za kimisionari, majeshi na kupitia mashirika ya usafiri wa reli”. Na kwa kumbukumbu hata hapa Tanzania (Tanganyika) vilabu vingi vinatokea au vilitokea katika maeneo hayo.

Timu kama Savages FC na Gezira SC  ndizo kongwe zaidi barani humu ambazo hadi leo zipo, zikianzia harakati zao kwenye miaka 1882. Achilia mbali kuhusisha kandanda barani Afrika na mambo ya kiuchawi, na sahau kuhusu kwanza mapenzi ambayo Kandanda letu barani Afrika lilivyo na mapenzi ya dhati na Siasa na Jamii inayoizunguka. Mtandao wa Kandanda umeangazia nini muhimu cha kuangalia kama unataka kuanzisha au kuongoza kilabu cha mpira wa miguu, yaani Kandanda.

Tulifunga safari hadi visiwani Zanzibar, katika Chuo Kikuu cha Kwanza Visiwani Zanzibar, Zanzibar University (ZU) kukutana na shabiki na Mtafiti Dizo Moja (Zomboko, Frank Eric) ambaye ni Mhadhiri akisomesha Masomo ya Biashara (Business Studies). Kikubwa kwanza tulitaka kujua katika upande wa masuala ya fedha, timu inawezaje kujiendesha, hapa tukitumia mfano wa timu ambayo ipo katika Ligi Kuu Tanzania Bara bajeti yake inaandaliwa vipi.

“Kwanza kabisa, kitu cha msingi lazima tujue kama tunataka kuandaa bajeti ya timu ni lazima kuangalia kwanza makadirio au makisio yetu ya mwezi mmoja.” Dizo moja alianza kwa hivi kwa kuuambia mtandao huu.

Vilabu vingi vimekuwa vikipata changamoto kubwa sana katika jinsi ya kujiendesha kwake hasa inapokuja katika swala katika masuala ya fedha. Wakati wote matumizi ya Kampuni, Taasisi yoyote au mtu mweredi wakati wote huangalia nini amepata, yaani mapato yake. Hivyo hivyo na klabu inatakiwa kuangalia nini itapata kabla ya kupanga bajeti ya matumizi yake.

Hivi karibuni Rais wa TFF (Shirikisho la Kandanda Tanzania), alinukuriwa kuwa wapo mbioni kuangalia jinsi ya kuleta usawa wa matumizi ya vilabu kulingana na mapato yao. Hili tuliache kwanza.

Dizo Moja

Hivyo basi kwa upande wa klabu kama tulivyosema hapo juu matumizi yako unatakiwa kuandaa nini unataka kufanya katika mwezi wako wa kwanza husika:

Mishahara: Wachezaji, Maofisa wote husika na Viongozi. Lazima ujue kikosi chako kitakuwa na wachezaji wangapi kwa uhitaji, benchi la ufundi bila kusahau viongozi waandamizi na klabu. Hapa ndipo watu wa rasmali watu wanaingia.

Kambi, Wachezaji na timu nzima inaweza kukaa kambini au kutokea nyumbani, lakini si muda wote wachezaji watatokea majumbani kwao. Gharama za kambi zinatakiwa kujumuisha Matibabu, Chakula na malazi

Timu ikiwa na mdhamini katika usafiri, inapunguza gharama.

Usafiri: Kwa kuzingatia mechi za nyumbani na ugenini, hapo maanake unatakiwa kuangalia nauli ya kwenda na kurudi, kwenda tena na kurudi, kutokana na ligi ilivyo. Ukishindwa kupanga hili unaweza jikuta unafika kituo cha mchezo asubuhi, jioni unaingia uwanjani na kufungwa vile vile. “Hapa inamaana wachezaji hawakuwa na utimamu wa kimchezo” Ticha Tigana, East Africa Radio, alituambia.

Viwanja vya mazoezi ugenini na nyumbani, Vinywaji: haya ni mahitaji muhimu kwaajili ya utimamu wa mwili wakati wa mazoezi na mechi pia. Vilabu kama Simba SC na Azam FC tayari vimeshamalizana kuhusu suala la viwanja vya mazoezi wakati timu ikiwa nyumbani. Vilabu vingi hulipia ili kupata huduma hiyo.

Mawasiliano, hii ikiangalia gharama za kuwasiliana na timu kama itakuwa nje ya kituo chake. Vilabu sasa vipo kidigitali zaidi, vinahitaji kupata taarifa na kuwasiliana katika kupanga mikakati yao.

Hapo ndipo pia vilabu vingi hugonga mwamba sana, na kupelekea kusuasua katika mashindano husika. “Matumizi haya ambayo ni muhimu sana kwa timu ndiyo yanatupekekea katika hatua ya pili ya kujua mapato yetu yanatakiwa kuwa vipi” Anaongeza Dizo Moja.

Mdathir akishangilia bao lake, Azam FC.

Swali kuu hapa, ‘Tunapata Pesa kutoka wapi'”

Wadhamini ndiyo kimbilio la kwanza, Ukiangalia vilabu vingi vya Ligi Kuu sasa vinavaa jezi zenye majina au nembo katika jezi zao, hao bila shaka wanakuwa wamekuwa wameisaidia timu husika katika baadhi ya vitu katika ‘Matumizi’ au fedha taslimu. Huo ndio umuhimu wao, pesa yao inaweza kusaidia katika baadhi ya maeneo ambayo tumeyaanisha hapo nyuma, mfano Usafiri ndio maana Sportpesa wameipa Simba na Yanga mabasi nakadhalika.

Viingilio vywa uwanjani, Mashabiki wanapoingia kuanngalia mechi ya timu husika wanalipia viingilio ambavyo baada ya makato mengine ya waendesha Ligi kinachobaki ndicho kinaenda kwa timu husika. Utaratibu wa Ligi Kuu kwa sasa ni kuwa mwenyeji ndiye anapata mapato yote baada ya makato mengine yote. “Je kila mechi inaweza kuingiza mapato ambayo timu inaweza yatumia katika matumizi muhimu, mfano kila mechi wakaingia mashabiki 2,000 kila mmoja akalipa

Moja ya mikutano ambavyo timu inaweza kutangaza viingilio au utaratibu wa mapato yao. Pichani ni Haji Manara, Msemaji wa Simba SC.

Wahisani, hawa unaweza waita wapambe, wadau, Wafadhili au wakareketwa wa timu, Simba Sc kuna watu wanajiita Friends of Simba. Hawa wahisani nao wanaweza kutoa kiasi gani kwa timu. Na je kinaweza kukidhi mahitaji?. Mfano msimu uliopita wadau wa Lipuli FC waliichangia timu hiyo maji ya kunywa kwa mechi nyingi sana kutokana na michango ya wadau hao.

Michango ya wanachama, hii ndiyo sehemu muhimu zaidi kwa timu lakini si ya kuitegemea sana katika mfumo wetu wa uendeshaji timu. Vilabu huweka ada na viingilio vya wanachama katika vilabu, ambavyo jukumu lake ni kusaidia katika uendeshaji wa vilabu husika. Klabu inaweza uza kadi ambazo zimetengenezwa kwa kiwango fulani kutokana na vile bajeti ilivyo, au pia unaweza boresha na kadi hizo katika madaraja tofauti tofauti.

Usimamizi wa klabu katika masuala ya fedha unamambo mengi sana “Ukimaliza kuangalia Matumizi na Mapato katika klabu lazima unangalie gharama (Cost) zako zinangukia katika upande gani” Dizo Moja. Wataalamu wa masuala ya fedha kama vile Mjumbe wa Kamati ya Fedha wa Klabu ya Lipuli FC, Bw. Shabani Lushino anaelewa vizuri sana haya mambo, Wao wanaita Varible Cost na Fixed Cost.

Fixed Cost vs. Variable Cost – Difference and Comparison – Diffzi

Gharama zote ambazo hazibadiriki tunaziita Fixed Cost (Mfano Usafiri) na zile ambazo zinabadilika badilika tunaziita Variable Cost. Mfano wa Variable Cost ni kama pale unaposafiri na timu kwenda Mwanza ukijua kwa kila chumba utalipia 30,000 lakini unafika kule unakuta chumba ni 40,000/-

“Tukumbuke pia, baada ya kuangalia Fixed na Variable cost, lazima tuangalie tena Expenses ambazo kwa kile ambacho unaweza kuwa umekutana nacho unaweza kufanya adjsustments (marekebisho) ili kuendana na uhalisia wake”.Ikiwa gharama za timu zimezidi mapato, hivyo tunatakiwa kuangalia kwenye Variable Cost, hapo ndipo unapojikuta kuwa chumba cha kulala watu wawili, wanne watalala kwa chumba hicho kimoja. Kimehesabu, sehemu ambayo unaweza punguza ni Variable Costs tu ili Matumizi yaendane na Mapato ya klabu. Ukikwama hapo, maanake klabu inaweza kuwa na madeni kutoka kwa wachezaji hadi walinzi wa klabu.

Hatua hii ni muhimu katika kuandaa bajeti ya klabu yako, hapo ndipo unaweza kufanya ya miezi inayofuata na kuangalia kama klabu unayotaka kuianzisha inaweza kukutengenezea pesa au itakuwa kwaajili ya kuwafurahisha tu mashabiki.

Vijana wakisakata soka katika viwanja vya Gezaulole (Gezaulole United SC)

Kwaufupi safari yetu visiwani ambako ni chimbuko la viungo mahiri sana katika soka letu, tumejifunza kwa undani kabisa kuanzisha timu si tu kukusanya vijana, kuandaa katiba ya timu na kwenda kusajili BMT. Inakubidi ukae chini uandae mpango mkakati, sehemu gani timu itakuwa maskani kwake bila kusahau rangi zake na jina ambalo litawavutia mashabiki wako wapya. Ikumbukwe pia kuna timu zimewahi kupanda Ligi na kushuka, na zikapotea moja kwa moja.

Sambaza....