Blog

Vipaji vingi sana vimepotea, na vinaendelea kupotea

Sambaza....

Wakati nakua pale Iringa, uwanja wa Mwembetogwa/Makorongoni ulikua uwanja maarufu zaidi kwa mechi za watoto! Ligi nyingi sana zilichezwa pale na watu wazima walifurahia burudani!

Ili timu ishiriki ligi, kiingilio ilikua TZS 200 na mshindi wa 1 angepata 1,000/. Kukata Rufaa ilikua 50 – 100.

Soka la mtaani (picha sio ya Iringa)

Marefa wa ligi zile wote walitoka kwenye familia ya Mzee Kibasila (Yusufu, Juma na Kibasila Abdallah). Hawa watu sidhani kama bado wanajihusisha na mpira, lakini kazi yao ilikua nzuri sana kwa wakati ule ambapo mpira ‘live’ ilikua mpaka twende kuchungulia mechi za Ulaya pale Paris Guest House au Stereo!

Leo nimemkumbuka mtu anayeitwa Agasele! Saidi Agasele! Moja ya watoto ambao mpaka sasa naamini, kwa akili zangu za umri huu, kwamba ni umasikini wetu Watanzania ulimfanya asiwe kama Okocha, Mark Viduka au Ben McCathy! Saidi angekua kama Eden Hazard, David Silva au Gareth Bale!

Jamaa alikua anaujua sana mpira! Ni kati ya watoto ambao ungependa uwe naye kwenye timu yako au ukae nje uangalie anavyocheza lakini si kupambana nae kwa sababu angekufanya ujione hujui kitu! Agasele alikua na ajili sana uwanjani, kasi na uwezo wa kufunga! Bahati mbaya hakuwa anaweza kucheza na viatu! Umasikini wetu ulimkuza akicheza peku na miguu yake ilizoea hivyo! Mpira kwake ulikua unakaa vizuri kama hana viatu miguuni na ikitokea mmempa viatu basi angeviua kati kati ya mchezo!

Agasele aliupamba uwanja wetu wa Mwembetogwa, akaifanya timu yetu ipendwe na akawafanya watoto wengi zaidi kutamani kuwa kama yeye! Umasikini wetu ukamnyima nafasi ya kukuzwa na kuendelezwa kipaji chake cha asili! Ukimuangalia Jordan Henderson Captain wa Liverpool) au Phil Jones wa Man Utd utaona namna ambavyo uwezo wa kiuchumi wa nchi yao (Uingereza) umewasaidia kuwa pale walipo! Lakini hakuna kipaji cha asili pale, siwezi kuwaweka level moja na Agasele fundi!

Leo hii nikiwa maskani huwa nakutana na Saidi Agasele maeneo ya Miyomboni, Akiba House pale akitafuta mkate wake! Kila nikimuuliza kuhusu mpira na mazoezi hua anacheka na kusema ‘Side, me siku hizi veteran, mazoezi kidogo sana nikipata nafasi! Lakini bado nawakimbiza.’ Tunaishia kuchrka halafu kila MTU anakula hamsini zake!!!!

Agasele, Muhsin, Richard na Yusuf Chediel, Frank Mkinga, Mwankusye Emmanuel, Faza Gian Adrian, Yahya Kibasila, Davy Geofrey na wengine wengi walitakiwa kuwa alama ya mpira wa Iringa na TZ kwa kizazi chetu! Lakini mpaka sasa mpira kwako umekua anasa kabisa!

Leo hii nikipita pale Mwembetogwa uwanjani basi nategemea kuona machinga wamepanga bidhaa zao au kuna jukwaa kubwa kwa ajili ya mkutano wa injili kama sio siasa au kiserikali.


Imeandaliwa na Fredirick Jailos, #KandandaChat (Picha zilizotumika sio za Iringa)


Sambaza....
Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.