Sambaza....

Klabu ya Soka ya Alliance ya Jijini Mwanza, Jumatatu hii imemtambulisha kocha wa Zamani wa Ruvu Shooting na Ndanda, Malale Hamis Keya kuwa kocha mkuu akichukua nafasi ya Mbwana Makata aliyetimuliwa wakati timu ikijiandaa na mchezo wa ligi dhidi ya Simba SC.

Akizungumza mbele ya vyombo vya habari, mwenyekiti wa mashindano wa klabu ya Alliance Yusuph Budodi amesema Malale ameingia mkataba wa miaka miwili na moja ya vipengele vya mkataba huo vikimtaka kumaliza ligi katika nafasi 10 za juu.

“Ni kweli leo tunatangaza benchi jipya la ufundi na Malale Hamsin atakuwa kocha mkuu, mnajua kuwa katika mechi zilizopita tulikuwa na kocha Gilbert Dady ambaye atabaki kuwa kocha msaidizi, lakini Malale amekuja na kocha wa makipa ambaye ni Wilbert Mweta William,”

“Tumempa mkataba wa miaka miwili lakini tumemtaka ahakikishe kwa msimu huu timu inamaliza katika nafasi 10 za juu, na tunamuahidi hatutamuingilia katika upangaji wa kikosi na ndio maana tumemuwachia nafasi ya kuendelea kusajili wachezaji anaowataka yeye,” Budodi alisema.

Kwa upande wake kocha Malale ameushukuru uongozi wa Alliance kwa kumuamini na kumpatia kibarua hicho na kuahidi kuendeleza falsafa ya soka la timu hiyo la pasi fupi fupi na haraka.

“Katika timu zote ambazo nimekuwa nikifundisha zimekuwa zikicheza soka la pasi fupi fupi na za haraka, naamini aina hiyo kwa hapa itakuwa bora zaidi, nawaamini wachezaji niliowakuta na kama kuongeza sitaongeza wengi ni sehemu chache chache tu kwa sasa, ila nawashukuru sana uongozi wa Alliance kwa kunichagua mimi kwani mbali na Tanzania kuwa na makocha wengi wenge sifa lakini wameniona mimi,” amesema.

Kuhusu hali iliyojengeka ya watu kuiona Alliance kama timu ya wanafunzi ambayo haiwezi kuleta ushindani kwenye ligi, Malale amesema, “Nimetoka kuzungumza na wachezaji kabla ya kuja hapa, nimewasisitiza hilo, nimewaambia wapo ligi kuu, wasijione kama wao ni vijana wanatakiwa kupambana kama wachezaji wengine kwenye ligi,”.

Wilbert Mweta William ambaye ni kocha wa makipa, yeye amemuahidi Malale ushirikiano mzuri katika kufanikisha timu ya Alliance inafikia malengo ambayo wamejiwekea msimu huu.

“Malale ni kocha ambaye amenifundisha, lakini pia ndiye kocha wa kwanza kufanya kazi naye, niliposikia anakuja huku nilifurahi na nikamuomba kuambatana naye akakubali, tunamuahidi ushirikiano ili kufikia malengo tuliyojiwekea msimu huu,” Mwita amesema.

Alliance inayoshika nafasi ya 17 wakiwa na alama 13, kwa sasa inajiandaa na mchezo wa ligi utakaopigwa Disemba 2, 2018 katika uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba watakapokaribishwa na Wanankurukumbi Kagera Sugar.

Sambaza....