Sambaza....

Aliyekua meneja wa klabu ya Chelsea Antonio Conte, anatajwa kuwa katika orodha ya makocha wanaopewa nafasi ya kuajiriwa na uongozi wa mabingwa wa soka barani Ulaya Real Madrid.

Jina la meneja huyo limechukua nafasi ya juu kwenye orodha hiyo, kufuatia joto la kufukuzwa kwa mkuu wa benchi la ufundi klabuni hapo Julen Lopetegui kuendelea kupanda siku hadi siku.

Kwa mujibu wa gazeti la The Mirror, uongozi wa Real Madrid kwa asilimia kubwa unaamini endapo utampata Conte, kutakua na uwezekano mkubwa wa kikosi chao kuwa na mabadiliko ya kiushindani katika ligi pamoja na ligi ya mabingwa barani Ulaya.

Kwa sasa Conte hana kazi, bada ya kuondoka Chelsea mwezi Julai mwaka huu, huku nafasi yake ikichukuliwa na Maurizio Sarri, ambaye kwa sasa anaendelea kuifanya kazi yake kwa ufasaha katika milki ya Stamford Bridge.

Wengine wanaotajwa katika orodha ya mameneja wanaowaniwa na Real Madrid ni Santiago Solari, Laurent Blanc, Michael Laudrup, Guti pamoja na Jose Mourinho, ambaye aliwahi kuwa mkuu wa benchi la ufundi klabuni hapo kuanzia mwaka 2010-13.

Harakati za kumsaka mbadala wa Lopetegui ziliongeza kasi mwishoni mwa juma lililopita, baada ya kikosi cha Real Madrid kupoteza mchezo wa ligi kwa kufungwa mabao mawili kwa moja nyumbani dhidi ya Levante.

Kufuatia matokeo hayo, Real Madrid kwa sasa inakamata nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi ya Hispania (La Liga), huku mwishoni mwa juma hili wakitarajia kusafiri hadi mjini Barcelona kucheza mpambano wa El Clasico dhidi ya mabingwa watetezi FC Barcelona.

Kabla ya mchezo huo wa ligi, Real Madrid leo jumanne wataendelea kutetea ubingwa wa Ulaya kwa kupambana na mabingwa wa soka wa Jamuhuri ya Czech Viktoria Plzen, na tetesi zinaeleza kuwa endapo watapoteza ama kutoka sare, uwezekano wa kutimiliwa kwa Lopetegui utaongezeka maradufu.

Sambaza....