Sambaza....

Klabu ya soka ya Azam imefikia maamuzi ya kumsafirisha beki wao Abdallah Kheri kuelekea nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa kina baada ya kuumia goti lake wakati akifanya mazoezi na timu ya vijana.

Afisa Habari wa Azam Jaffary Idd Maganga amesema maamuzi hayo yamefikiwa baada ya kutambua kuwa jeraha alilopata ni kubwa na linahitaji uchunguzi mkubwa ili kupata tiba yake.

“Jana tumemsafirisha beki wetu Abdallah Kheri kuelekea Afrika Kusini kwa ajili ya uchunguzi wa goti lake aliloumia wakati akiwa anaitumika timu ya vijana, jeraha lake ni kubwa na ndio maana tumefikia uamuzi huo kabla ya kurejea tena kwenye soka la ushindani,” Maganga amesema.

Kheri ambaye ni mchezaji wa timu ya Taifa, na mwenye umri wa miaka 22 alijiunga na Azam akitokea Zimamoto ya Zanzibar, lakini amekuwa hapati namba mara kwa mara kwenye kikosi cha kwanza cha Azam licha ya kuonekana kuwa na kiwango bora.

Sambaza....