Blog

Dani Ceballos nyongeza ya Ozil kwa Arsenal kutoka Madrid.

Sambaza....

Namfikiria yule Mesut Ozil wa pale Madrid mwaka 2010 hadi 2013 alivyokua mtu hatari nyuma ya Christiano Ronaldo mkono wangu wa kushoto unapata kigugumizi kumuandika vibaya mpiga pasi huyu wa Kituruki.

Tupilia mbali mbwembwe za mashabiki wa Arsenal sijui Lacanyavu,Auba,Xhaka boom, na wengine, hapo 2013 dunia ilizizima baada ya Mesut Ozil kutua rasmi kwa washika mtutu wa pale London.

Jezi ziliuzwa sana, tambo zilikua hazizuiliki mashabiki wa Arsenal walinenepa na wengine walikufa kwa furaha ya kumpata mnyumbulifu huyo wa dimba la kati.

Mali ikaanza kupigwa, Arsenal ikaanza mambo yake leo kicheko, kesho kilio “Ups and Downs” zikawa kibao sema mguu wa Ozil ulibaki kuwa nuru pale Arsenal japo haikuwa kwa viwango vile vya Madrid.

Miaka tisa baadae Arsenal wakarudi mezani kwa maboss wa Real Madrid wakawaambia wazee mnakumbuka tulifanya vyema biashara ya Ozil miaka ile?, Sasa kwanini msitupe kijana Dan Ceballos kwa mkopo aje akinukishe pale Emirates maana nyie hata hammtumii saana.

Madrista wakanyoosha roho, wakamkabidhi Daniel Ceballos Fernández kwa mabosi wa Arsenal kumbe Ceballos mwenyewe alikua na hasira zake na dimba la washika bunduki hao akilini akiamini kuwa inabidi alipe deni la Madrid wanalodaiwa pale juu ya uwezo wa Özil yule wa 2012.

Panga pangua za Arteta zikamfikia Ceballos akapewa dimba kazi ikaanza, akaanza kunesa box baada ya box “Box to box midfielder” Arsenal hao wakapita na kikombe cha FA mbele ya Chelsea ya Frank Lampard.

Nikakumbuka kuwa ‘Muungwana akipewa hushukuru’ kwa maana ya Mkwanja waliouvuna Madrid kwa Arsenal pindi wanamuuza Özil ulikua mkubwa kuliko alichoenda kukifanya Özil pale London, hivyo wakaona sio kesi wacha wawashukuru Arsenal kwa kuwapa kijana Ceballos kwa mkopo kama nyongeza ya biashara ya Ozil.

Sasa ni muda mwafaka wa Mabosi wa Arsenal kurudi mezani na kutaka saini ya jumla ya kiungo huyo mdogo muongo muongo wa kihispania mwenye umri wa miaka 23.

 


Sambaza....
Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.