Ligi Kuu

DANTE ni UCHOCHORO kwenye mechi ya SIMBA na YANGA

Sambaza kwa marafiki....

Kesho imekaribia kufika ili Tanzania ishuhudie sikukuu ya mpira wa miguu. Sikukuu ambayo kila Mtanzania hutamani kuishuhudia kwa sababu tu Simba na Yanga zimebeba mashabiki wengi Tanzania.

Kuelekea mechi hii leo hii tutaanza kuangalia sehemu ambazo zina udhaifu mkubwa ndani ya vikosi vyote, leo hii tunaanza na Yanga na tunaanza na beki wa Yanga Andrew Vincent “Dante”. Kwanini nasema ” Dante” ni moja ya madhaifu ambayo Yanga wako nayo?

Sababu kubwa ambayo Andrew Vincent “Dante” inampotezea sifa nyingi za kuwa beki wa kati ni ile tabia yake ya yeye kutokuwepo katika eneo lake muda mwingi.

Andrew Vincent “Dante” huwa anakuwa na tabia ya yeye kusogea mpaka katikati ya uwanja na kusababisha eneo la nyuma kuwa na uwazi.

Hapa ndipo uchochoro unapoanzia. Kwanini nasema hivo ?, mpira wa siku hizi ni mpira wa kutengeneza uwazi na kuutumia uwazi husika.

Inapotokea beki analazimika kutengeneza uwazi (spaces) katika eneo lake la nyuma basi huwa inakuwa kuna madhara makubwa sana kwa timu yake.

Andrew Vincent “Dante” mara nyingi huwa anakuwa juu sana “HIGH” kitu ambacho hupelekea eneo la nyuma kwa Yanga kuwa na uwazi sana.

Sasa ni kwa namna gani Simba wanaweza kutumia madhaifu haya ya Andrew Vincent “Dante” kuwaadhibu Yanga kwenye mechi ya Kesho.

Kama Andrew Vincent “Dante” ataamua kutumia muda mwingi mwa mchezo kuwa chini(kwenye eneo lake la nyuma) na kuachana na tabia yake ya kusogea juu, basi Simba wanatakiwa kufanya kitu kimoja.

Mshambuliaji wa kati wa Simba anatakiwa kumlazimisha Andrew Vincent “Dante ” kutengeneza uwazi katika eneo lake la nyuma.

Kivipi ?, kama mshambuliaji huyo wa kati ambaye kwa asilimia kubwa atacheza John Bocco, kama atakuwa na tabia ya kuwa ana shuka chini katikati kufuata mpira basi hii itakuwa na faida kubwa sana kwa Simba na hasara kwa Yanga.

Kwanini nasema hivo ?, kama John Bocco atakuwa na tabia ya yeye kushuka chini katikati kuchukua mipira, basi atamtamanisha Andrew Vincent “Dante” kupanda.

Kuna asilimia kubwa ya Andrew Vincent “Dante” kuwa anapanda kumfuata John Bocco kila anaposhuka chini katikati.

Na kila Andrew Vincent “Dante” atakapokuwa anapanda juu kumfuata John Bocco basi atakuwa anatengeneza uwazi katika eneo lake la nyuma.

Na akitengeneza uwazi kwenye eneo lake la nyuma basi wachezaji wa Simba watakuwa na nafasi ya kuutumia uwazi huo wa nyuma kwa ajili ya kuwaadhibu Yanga.

Sasa kipi wakifanye Yanga?. Kuna vitu viwili ambavyo Yanga wanatakiwa kuvifanya. Cha kwanza ni hiki hapa, Yanga wanatakiwa kukataa kulazimishwa kutengeneza uwazi katika eneo lao.

Wacheze mpira ambao uwazi kutokea katika uwanja uwe kwa nadra sana. Kama John Bocco atakuwa na tabia ya kushuka chini kuchukua mipira basi Yanga wasitamani kupanda naye.

Njia ya pili ni yule ambaye atapewa jukumu la kucheza eneo la kiungo cha kuzuia apewe jukumu la kutembea na John Bocco kila anapokuwa anashuka chini katikati kuchukua mipira.

Kuwepo kwa Andrew Vincent “Dante” kwenye mechi kama hii dhidi ya timu yenye safu imara ya ushambuliaji kama Simba ni hatari kubwa sana kwa Yanga, hivo wanatakiwa kabisa kutoruhusu uwazi kutengenezeka katika eneo lao.

Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.