Blog

Eti mechi ya Stars, ‘Ball Boys’ walikuwa Warundi.

Sambaza....

Ilikuwa ni dakika ya 79, Divock Origi anaiandikia Liverpool goli la 4 na kuifanya Liverpool kuongoza goli 4-0 dhidi ya wababe Barcelona katika mchezo wa nusu fainali ligi ya mabingwa Barani ulaya.

Goli hilo liliifanya Barcelona kutolewa nje ya mashindano hayo kwa jumla ya goli 4-3. Yalikuwa ni matokeo ya kibabe kwa Barcelona msimu uliopita, hadi leo kuna baadhi ya watu hawakubali kilichotokea na sasa wanaamini kuwa Liverpool ndio timu yenye maajabu yake katika ulimwengu wa soka, kumbuka Instanbul Miracle mwaka 2005.

Kwa msimu uliopita Liverpool walitawazwa kuwa mabingwa wa Ulaya. Wengi waliwapa ubingwa mapema tu baada ya kuwatoa Barcelona, licha ya kukutana na Tottenham katika mchezo wa fainali lakini watu walijua Liver ndiye mshindi wa mchezo huo.

Katika goli la Origi, la dakika ya 74 dhidi ya Barcelona, wengi walimpa kongole nyingi sana beki wa kulia wa Liverpool, Muingereza Trent Alexander Arnold aliyetishia kuuacha mpira kisha kupiga kona iliyomkuta Origi akiwa pekee yake bila kukabwa na yoyote na kuweka kambani goli la nne.

Kitu ambacho wengi hawakijui ni kwamba katika goli kama lile mtu wa kwanza kumsifia sio Origi wala Alexander bali ni “Ball Boy”.

Ball Boys na Ball Girls ni watu muhimu sana katika mechi. Katika mechi ya Liverpool, Muokota Mipira aliwahi kuuweka mpira eneo la kona kabla hata ya Alexander kufika katika eneo hilo na kutishia kuuacha kisha kupiga haraka.

Kwanini Muokota mipira aliuwahisha mpira eneo husika? Kwa sababu  anajua Liverpool kwa wakati ule ilikuwa ikihitaji nini. Ball Boy naye alikuwa mchezoni, na alihakikisha Liverpool inapata matokeo katika mchezo huo.

Kote duniani, Ball Boys na Girls hutumika katika michezo mbalimbali lengo ikiwa ni kuharakisha matumizi ya mpira,  ili kudhibiti upotevu wa muda wa mchezo.

Waokota mipira wengi wana wastani wa miaka 15. Katika nchi zilizoendelea Ball boys hupewa mafunzo ya muda maalumu lengo ni kuwafanya kujua hasa ni nini wanatakiwa kufanya katika mazingira gani.

Mfano katika ligi ya Marekani NFL, Waokota mipira humilikiwa na vilabu husika na hulipwa vizuri kwa kazi hiyo.

Acha niiangazie Tanzania hasa katika mchezo wa hivi karibuni, Ambapo Stars iliikaribisha Burundi, INTAMBA M’URUGAMBA katika uwanja wa Taifa kwa Mkapa ikiwa ni mchezo wa marudiano wa kufuzu kombe la dunia nchini Qatar mwaka 2022.

Katika mchezo ule wa nyumbani Stars ilihitaji matokeo, ndio maana kuanzia kipindi cha pili, wachezaji wa Stars walikuwa haraka hasa katika mipira ya kurusha na hata ya faulo huku Burundi wakieendelea kujiangusha hovyo.

Uharaka huu ulimaanisha kuwa, stars inahitaji goli, lakini kitu pekee kilichonishangaza ni mipira kuchelewa kuingia uwanjani baada ya kutoka na hata ilipoingia iliingia zaidi ya mmoja.

Yaani Ball boys wa siku hiyo walirusha mipira uwanjani bila kuangalia kama kuna mpira mwingine umeshaanzishwa, matokeo yake refa alipiga filimbi ili kuutoa mpira mmoja, hii ilipoteza Muda.

Bila kujua, au Makusudi matukio ya aina hii yalijitokeza zaidi ya mara moja. Kujirudia huku kulinifanya niamini kuwa, katika mchezo huo, ‘Ball Boys’ walitoka Burundi.

Kwa maana ukiwa na Muokota Mipira ambaye hujamfunza vizuri akajua  jukumu lake katika mechi husika, humlipi vizuri au humlipi kabisa, umemuokota tu mtaani hata sheria za kumuongoza hazijui, hajui thamani ya sekunde mbili katika mchezo, sio Mzalendo, ujue kabisa huyo alikuwa Mrundi.

Hapa naongea na Shirikisho, pia naongea na wewe Muokota mipira, Stars imeshafuzu hatua ya makundi, hatua hii ni ngumu kuliko kawaida. Tukiongoza kundi katika hatua hii tutaenda katika mechi mbili za mtoano.

Kutakuwa na makundi 10, kundi letu litakuwa na timu nne, tutacheza mechi 6, tatu ugenini na tatu nyumbani. Mechi hizi zinahitaji mbinu za uwanjani na hata nje ya uwanja. Waokota mipira ni sehemu ya mashambulizi na ulinzi wa Stars.

Ni muda sasa wa kuwafundisha Ball Boys wetu, wawe wazalendo, wawe katika mchezo, wawe na uwezo wa kujua Stars kwa sasa inahitaji nini na wao wanatakiwa wafanye nini. Yakijitokeza ya Burundi tutaishia kunawa tu, kula watakula wengine.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x