Blog

Hesri Said! Mkombozi sahihi wa Yanga anaehitajika na Wananchi.

Sambaza....

Neno bwanyenye kwa kiswahili lina maana ya mtu mwenye mali nyingi ambapo wingi wake huwa Mabwanyenye. Achana na hayo, kiswahili na maneno yake muendelee kujifunza kutoka kwa wajuzi wa Lugha hii yetu pendwa akiwemo mimi pamoja na nguli Oni Sigara.

Andiko hili leo ni kuhusu moja ya mabosi wa kampuni ya GSM mwenye mapenzi na Kandanda aliyeamua kuwekeza akili, nguvu na mipango yake mikubwa kunako klabu ya Yanga, si mwingine ni mhandisi Hersi Said.

Sina uhakika bali ninaimani kuwa huyu ndiye aliyeishawishi kampuni na mabosi wa GSM kwenye vikao vyao kuwekeza kunako klabu ya wananchi “Dar es Salaam Young African” soma hii kwa sauti ya Antonio Nugazi.

Mwaka 2016, klabu hii yenye makombe mengi kuliko klabu yoyote Tanzania ilikumbwa na ukata baada ya aliyekuwa bwanyenye ama tajiri wa chama hilo bwana Yusuph Manji kuamua kuachana na timu hii pendwa nchini Tanzania.

Aliekua Mwenyekiti wa Yanga, Yusuph Manji.

Kwakua soka la bongo limetawaliwa na utani wa jadi kati ya Yanga na majirani zao Simba basi mashabiki wa klabu hio hawakutaka kabisa kuamini wala kuonesha kuwa timu yao imetetereka kiuchumi bali walizidi kuipambania kwa hali na mali.

Daima hakuna mwanzo usio na mwisho, mashabiki, viongozi, wadau na wapenzi wa timu hiyo walijitoa kwa kila namna kulinda uchumi wa klabu hio ili kuitofautisha Yanga na Ngara Boys.

Ilifika mahali jitihada zote zikagonga ukuta na wingu kubwa jeusi lenye michirizi ya njaa, tabu na shida likatanda hewani pale mitaa ya Jangwani.

Manj (Katikati mwenye Fulana ya Njano) kwenye moja ya Mechi za Yanga

Ndipo jina la “Timu ya wananchi” likaibuka, likawafanya mashabiki wasahau kabisa habari za kusaidiwa na flani kisha kuamini kuwa timu ni yao na wao ndio wanapaswa kuirudisha kwenye ramani.

Kwa uwezo wao wananchi wa Yanga waliweza kupunguza baadhi ya madeni, shida na karaha zilizokuepo pale jangwani japo mziki ulikua bado mnene kama wasemavyo waswahili wa Efm.

Imani yao ikabaki kuwa Yanga ni timu kubwa hapa bongo na lolote linaweza kutokea, wakasali wakalala siku zikaenda. Asubuhi moja wakaamka na kukuta ofa kubwa kutoka kampuni ya GSM ikiwajuza kuwa wanataka kuwekeza kunako klabu hio.

Viongozi wa Yanga

Wengi wao hawakuamini kwani imani yao juu ya matajiri aliondoka nayo yule bwanyenye Manji, GSM wakatafuta mtu wa kuwaaminisha mashabiki hao dhamira hio chanya.

Bila kupepesa macho risasi, mabomu na silaha zote wakamkabidhi injinia Hersi Said, Naam!! mwamba akaanza kazi kwa ufasaha, mashabiki wakavuta pumzi ya matumaini.

Mipango ikaanzia kwenye jezi, Hersi kupitia GSM wakaachia uzi mmoja mtamu sana kwaajili ya Yanga na mashabiki zake kwa msimu wa soka 2019/2020, imani ikaanza kurejea.

Wachezaji wa Yanga ndani ya uzi mkali kutoka GSM.

Baadhi ya madeni yakalipwa, wachezaji wakaanza kupanda tena ndege kwenda kwenye mechi za mikoani.

Ubishi mjini ukaanza, Simba wakahofia kunyang’anywa ubingwa wao, presha ikawa juu huku wanayanga wakitamba mtaani kicheko meno therathini na mbili yote nje.

Hersi huyo huyo kupitia GSM na Yanga wakasajiri vifaa mara ghafla Benard Morisson akawachoma mkuki wa moyoni Simba kwenye mchezo wa ligi ngoma ikaisha 1-0, Yanga wakiondoka na ushindi wananchi wakajaza shangwe kila kona.

Mipango ikawa mingi, tupilia mbali habari za kushirikiana na Laliga, sahau kuhusu harakati za ujenzi wa viwanja viwili vya kisasa Kigamboni na jangwani ruka kila kitu hapo kati njoo hadi kwenye usajiri wa wachezaji kuelekea msimu mpya 2020/21.

Viongozi wa Yanga na GSM katika hafla ya utiaji saini ya uhusiano na Laligaga

Unaiona yanga yenye mikakati madhubuti, jana tu Hersi kala mwewe mpaka Congo, kawachukua “key players” wawili toka klabu ya AS Vita (Tuisila na Tunombe) kwa dau nono kweli.

Leo hapo pasi yake ya kusafiria  itakua inapigwa mhuri mwingine azame nchi nyingine kuchukua vifaa bora vya kazi pale Jagwani.

Nia kaionyesha, uwezo na mikakati ipo, nini tena mpewe Wananchi?.

Hii ni ishara kuwa Hersi na GSM wangekuepo Yanga toka mwanzo hata kabla ya matajiri wengine basi leo Jangwani kungekuwa na vikombe vingi vya klabu Bingwa Afrika, Ligi, na vingine vingi.

Mabadiliko lazima yafanyike, kuna watakaoumia pia watakaofurahia.


Sambaza....
Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.