Sambaza....

Kikosi cha timu ya Vijana chini ya Umri wa miaka 17 (Serengeti Boys) kimeendelea na mapumziko kupisha sikukuu za Christmas na Mwaka mpya kabla ya kurejea tena kambini kuendelea na maandalizi kwa ajili ya michuano ya Afrika itakayofanyika mwakani hapa nchini.

Kocha wa Serengeti Boys Oscar Mirambo amesema baada ya mapumziko hayo ya majuma mawili wataendelea na mazoezi ambapo wataenda nchini Uturuki kushiriki mashindano ya timu 12 kutoka bara la Afrika na Ulaya.

Amesema mashindano hayo yatatumika kama sehemu ya kuendelea kufanya tathimini kwa kikosi walichonacho kabla ya mashindano ya Afrika ambayo yanatarajiwa kufanyika mwakani hapa nchini.

“Tunataka kuyatumia haya mashindano kama sehemu ya kuendelea kufanya tathimini ya kikosi chetu pia kuona kama kuna changamoto ambazo tunahitajika kuendelea kuzirekebisha kuelekea katika mashindano makubwa ambayo tutayafanya hapo baadae mwakani hapa nyumbani,” amesema.

Ikumbukwe wenyeji Serengeti Boys ambao ni Mabingwa wa CECAFA na COSAFA wapo kundi A pamoja na timu za Angola, Uganda na Nigeria huku kundi B likiundwa na Guinea, Morocco, Senegal na Cameroon.

Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Tanzania kuandaa mashindano makubwa ya soka kwa Afrika.

Sambaza....