Mataifa Afrika U17

Sababu zilizosababisha Serengeti Boys itolewe.

Sambaza kwa marafiki....

Serengeti Boys ilitolewa kwenye michuano ya vijana waliochini ya umri wa miaka 17 ya Afrika, hivo kama mwenyeji aliaga rasmi kwenye michuano hii. Je ni sababu zipi ambazo zimesababisha timu itolewe ?

SAFU MBOVU YA IDARA YA KIUNGO

Hapa ndipo palikuwa kiini pa tatizo kubwa kwa timu ya Serengeti Boys. Idara ya kiungo ilikuwa mbovu katika maeneo mawili.

Eneo la kwanza , idara hii ya kiungo ilikuwa haina uwezo mkubwa wa kuilinda idara ya ulinzi ya timu ya Serengeti Boys.

Ndiyo maana ilikuwa inapokea mashambulizi mengi sana. Pili, Idara ya kiungo ya Serengeti Boys ilikuwa dhaifu katika kuzalisha au kutengeneza nafasi ndani ya uwanja.

Kina Edmund John na Kelvin John muda mwingi walikuwa hawatengenezewi nafasi nyingi za kufunga. Pia walikuwa hawapati usaidizi mkubwa wakati timu inashambulia kutoka katika safu ya kiungo.

TIMU KUTOKABIA JUU.

Ulikuwa unawatazama Kelvin John na Edmund John wakati wanapoteza mpira kule mbele?. Walikuwa hawajishughulishi kukaba.

Na hata mabeki wa timu pinzani walipokuwa wanamiliki mpira wao walikuwa hawashughuliki kwenda kuwakaba, hivo kuwaacha mabeki wawe huru kuanzisha mashambulizi bila bughudha yoyote.

IDARA YA ULINZI

Huku ndiko kulikuwa na makosa mengi binafsi ambayo yalikuwa yanasababisha golikipa kukutana na washambuliaji wa timu pinzani.

Mabeki wa pembeni walikuwa dhaifu. Magoli ya Uganda Jana yalitokea pembeni mwa uwanja. Mabeki wetu wa pembeni walikuwa wanacheza sana juu na kuacha uwazi katika eneo nyuma.

AHADI NA MATEGEMEO MAKUBWA KWA WATOTO.

Tulitegemea mkubwa sana kwa hawa vijana na ahadi tulizitoa nyingi kwa hawa watoto. Kitu ambacho kilichangia kwa kiasi fulani wachezaji kubebeshwa jukumu kubwa ambalo hawakustahili.

Jukumu ambalo liliwafanya wawe na presha kubwa ya kuyafikia matamanio yetu kitu ambacho kiliwaondolea umakini mkubwa.

Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.