Sambaza....

Maafande wa JKT Tanzania wamejinasibu kuwa tayari kwa mchezpo wa mzunguuko wa 11 wa ligi kuu ya soka Tanzania bara ambao utawakutanisha na vinara wa msimamo wa ligi hiyo Azam FC, kwenye uwanja wa Meja Jenerari Isamuyo uliopo Mbweni JKT jijini Dar es salaam.

Afisa habari wa klabu ya JKT Tanzania Jamila Mutabazi hii leo amezungumza na waandishi wa habari na kueleza namna walivyojiandaa na mchezo huo wa kesho, huku akikiriwa akisema kuwa kikosi chao kinawaheshimu Azam FC kutokana na soka safi wanalocheza.

Hata hivyo Jamila amesema pamoja na kuwapa heshima hiyo Azam FC, bado dhamira yao kuelekea mchezo wa kesho inawaelekeza katika kusaka alama tatu muhimu na kuendeleza kasumba ya kutopoteza mchezo tangu walipoanza msimu huu wa ligi kuu.

“Niseme tu Azam Fc ni wazuri kama tunavyowaona kwa sasa wanaongoza ligi, tunawaheshimu, lakini hata sisi ni wazuri kwani hatujapoteza mchezo wowote mpaka sasa hivi sasa, kuhusu kikosi wachezaji wote wapo vizuri na hatuna majeruhi,” Jamila amesema.

Katika hatua nyingine Jamila akazungumzia mchezo wao dhidi ya Wekundu wa Msimbazi Simba utakaochezwa kwenye uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga mwezi ujao, baada ya bodi ya ligi kupitisha ombi lao la kuutumia uwanja huo kama uwanja wao wa nyumbani kwa michezo itakayowakutanisha dhidi ya Simba na Young Africans.

Wakati huo huo Jamila akawataka mashabiki wa JKT Tanzania kuiunga mkono klabu yao kwa kununua jezi halisi za klabu hiyo ambazo zimetengenezwa kwa ajili yao, kwa msimu huu wa ligi kuu ya soka Tanzania bara.

Michezo mingine ya mzunguuko wa 11 wa ligi kuu ya soka Tanzania bara itakayochezwa kesho jumatano, ni pamoja na Coastal Union watakua nyumbani CCM Mkwakwani wakiwakaribisha Kagera Sugar kutoka mkoani Kagera.

Simba watapambana na Alliance FC Uwanja wa taifa Dar es salaam, Maafande wa Tanzania Prisons watakua nyumbani jijini Mbeya kwenye uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine wakipapatuana na African Lyon kutoka jijini Dar es salaam na Ruvu Shooting watawakabili Singida Utd kwenye uwanja wa Mabatini mkoani Pwani.

Sambaza....