Blog

Kichuya umeenda MISRI ukiwa umenenepa sana.

Sambaza....

Mtaani kuna picha yako inasambaa sana. Picha ambayo ulipiga kipindi ambacho ndiyo unatua Simba. Kipindi ambacho dunia ya mpira wa miguu ilikufahamu vizuri. Kipindi ambacho kila jicho lilijivunia sana kukuona wewe, hakuna ambaye alikuwa hana furaha kila alipouona mguu wako wa kushoto ukigusa mpira.

Kuna wakati hata mashabiki wa Yanga walikuwa wanakukubali kimoyo moyo. Hili limejionesha baada ya wewe kuondoka Simba. Mashabiki wa Yanga wamefurahi sana , unajua kwanini ? Kwa sababu wewe ulikuwa mhimili mkubwa wa Simba kwa misimu ya hivi karibuni. Wewe ndiye ulikuwa muuaji mkuu wa Yanga katika mechi dhidi yao. Kuna usemi unasema kuwa “ukiona mtu anakuogopa basi jua anakukubali”.

Bila ubishi wewe ulikubalika sana mpaka kwa mashabiki wa Yanga, kwa sababu tu walikuwa wanakuogopa sana. Hata kuondoka kwako kumekuwa ni furaha kubwa sana kwao. Utaachaje kufurahia kipindi ambacho unaona mchezaji bora kutoka timu ya wapinzani wako anaondoka?. Mchezaji ambaye msimu jana alikuwa mchezaji bora wa klabu. Mchezaji ambaye msimu jana nusu ya magoli ya Emmanuel Okwi yalitengenezwa na mguu wake?

Mchezaji ambaye anaondoka akiwa na wastani wa kufunga magoli 10 kwa msimu mmoja?. Mchezaji ambaye alikuwa anatengeneza nafasi nyingi za magoli ? Mchezaji ambaye alikuwa hachoki akiwa ndani ya uwanja. Alikuwa anapigana sana tena kwa moyo wote. Lilikuwa ni jambo la kawaida sana kwa Shiza Kichuya kuonekana kila sehemu ya uwanja. Wakati timu inapokuwa inashambulia alikuwa anahusika na mashambulizi.

Kipindi ambacho timu ilikuwa haina mpira Shiza Kichuya alikuwa anaonekana kupambana kukaba kwa kushuka chini ya uwanja. Kwa kifupi Shiza Kichuya ni mchezaji mwenye ” work rate” kubwa ndani ya uwanja. Na aina hii ya wachezaji ni aina ya wachezaji wa kisasa. Makocha wengi watapenda kumtumia mchezaji wa aina hii katika mbinu zake ndani ya uwanja. Kwa mfano, dunia ya sasa makocha wengi wanapenda timu zao kufanya “pressing”.

Iwe ” high pressing” kukabia juu. Ambapo wanatakiwa aina ya wachezaji ambao wana kasi pia wawe na “work rate” kubwa. Sifa hizi Shiza Kichuya anazo kabisa. Pia kuna wakati mwingine makocha wengi wa kisasa wanatumia “hard pressing”. Mfano, Jurgen Klopp kocha wa Liverpool hutaka timu yake ifanye ” hard pressing ” ikiwa haina mpira ili kutowapa nafasi wapinzani kujipanga na mashambulizi.

Mbinu hii huitaji pia aina ya wachezaji ambao wana “work rate” kubwa ndani ya uwanja. Kitu ambacho Shiza Kichuya anacho. Kwa kifupi Shiza Kichuya ni mchezaji wa kisasa, ni mchezaji wa mpira wa kisasa. Ni mchezaji ambaye makocha wengi watatamani kuwa naye. Lakini sifa zote hizi alikuwa nazo msimu jana kurudi nyuma. Misimu ambayo alikuwa na njaa. Msimu ambao shibe ilikuwa haijakaribia tumbo lake.

Alikuwa anapigana sana bila kuchoka kwa kuamini alichokuwa anakitafuta. Hakuwa ameridhika kabisa. Moyo wake , mwili wake pia ulikuwa haujanenepa kabisa kama ambavyo alivyo sasa hivi. Moyo wake , nafsi yake na mwili wake umenenepa sana.

Hana njaa tena!, hapigani tena kama kipindi kile alipokuwa na njaa. Ile “work rate” ndani ya uwanja imepungua sana. Hata umakini umepungua sana hasa hasa akiwa na mpira na akiwa hana mpira. Siyo kama kipindi cha nyuma ambapo kila alipokuwa na mpira alikuwa anafanya maamuzi ambayo yalikuwa yanainufaisha timu yake.

Kitu hiki kimepungua sana Shiza Kichuya. Najua anauwezo wa kukirudisha kabisa. Muda anao , bado hajachelewa. Na kizuri zaidi anaenda Misri. Sehemu ambayo anatakiwa awe na njaa kali kama njaa aliyokuwa nayo kipindi cha nyuma wakati anatua Simba, ili tu afanikiwe kufika sehemu ambayo mwanzoni alikuwa anaiota.

Nafahamu ni ndoto ya kila mchezaji kucheza sehemu ambayo ina manufaa makubwa kwake. Misri ni sehemu nzuri kwake yeye kujiuza. Asiruhusu tena nafsi yake, moyo wake na mwili wake uzidi kunenepeana kama ambavyo alivyokuwa ameanza kunenepa wakati yupo Simba.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x