Ligi Kuu

Kisiga anaishi kijamaa katika dunia ya kibepari

Sambaza....

Shaban Kisiga Malone. Mchezaji mmoja na nusu. Dead ball specialist. King of assist. Ball player. Ally Kamwe aliwahi kuniambia anachoweza kukifanya Said Juma Makapu kwa dakika moja, Kisiga anakifanya kwa sekunde mbili. Huyu ndiyo Kisiga aliyeamua kuukacha mpira na kukaa zake Vingunguti.

Jumamosi asubuhi nilikuwa nikifuatilia mahojiane yake na kaka yangu kitaaluma Bin Zubeiry kwenye kipindi cha Sports AM kinachorushwa na Azam Tv. Kisiga na Bin Zubeiry walizungumza mengi, lakini kubwa Kisiga alisema haonekani uwanjani hivi sasa kutokana na kutolipwa fedha zake na Ruvu Shooting.

Bin Zubeiry alimsihi atafute utaratibu wa kupata pesa zake, lakini Kisiga mwenyewe ni kama hajaonyesha kujali zaidi alisema anamuachia Mungu.

Maisha ya Mtanzania wa kileo anayeishi chini ya Dola Moja, Kisiga anadai vipi pesa zake kisha anasema anamuachia Mungu bila kujali ugumu wa maisha? Hapa aliniachia maswali.

Ina maana ana pesa nyingi zinazompa kibuli mpaka azipuuze pesa zake Ruvu Shooting? Ina maana amesusa? Ina maana hajui ugumu wa maisha? Ina maana amejikatia tamaa na umri wake wa miaka 31? Miaka hii bado ana nguvu za kutosha na kucheza katika kiwango bora tena kwa miaka mitano mbele.

Shaban Kisiga (Kushoto)

Binafsi nimehuzunika kuona fundi kama yeye akiondoka uwanjani mapema tena kwa sababu ya masilahi. Anyway anaondoka uwanjani nyuma akituachia kumbukumbu nzuri isiyoelezeka kwa siku moja, mbili wala tatu.

Nilitaraji kumuona akiondoka uwanjani kwa sababu za kimajeraha au umri wake kusogea, lakini sababu inayomtoa ni dhaifu mno. Katika miaka yake 31, anaondokaje kirahisi uwanjani kama alivyozungumza siku ile, huku sura yake ikijaa bashasha kama kazungumza kitu kizuri? Ameuponda sana moyo wangu.

Tofauti ya wachezaji wa Kitanzania na wachezaji wa mataifa mengine inaonekana katika hali kama hii. Namkumbuka Mmalawi Wisdom Ndlovu, Wakenya Joseph Shikokoti, Donald Musoti, walizikamua fedha za Simba, Yanga walipokwenda FIFA kupeleka madai yao. Kesi ilichukua muda, lakini zilisikilizwa na mwisho walishinda na walilipwa mamilioni yao.

Kando ya tofauti ya ubora wa wachezaji wetu na wachezaji wa mataifa mengine, tofauti nyingine ni hapo kwenye madai. Kina Musoti wamepata haki zao, Kisiga ameamua kurudi zake Vingunguti, nyuma akituachia ujumbe wa kumuachia Mungu madai yake. Hii ni moja ya tofauti ya wao na sisi.

Mpira wa miguu ni mchezo wa wanaume 22 wanaoingia uwanjani kuminyana vikali. Kuna wachezaji wamewahi kupoteza maisha yao uwanjani. Sijazungumza na watu wa Shooting kwa ajili ya kupata balance ya andiko hili, lakini timu zinapaswa kulitazama hili kwa macho matatu juu ya madai ya wachezaji.

FOS

Kama Kisiga anaondoka uwanjani kichwa chini namna hii, vipi rafiki zangu Said Ndemla, Kelvin Sabato, Ibrahim Ajib na Jonas Mkude wao wataondoka uwanjani kwa style gani?

Nilitaraji kuiona sura ya pili ya Kisiga katika kuidai haki yake. Sura yake ya kwanza ndani ya uwanja ninayo kwenye kiganja changu, muda wowote naitazama, lakini kitendo cha kusema anamuachia Mungu, ametunyima fursa ya kumtazama Kisiga wa sura ya pili.

Kwa kilichomtokea Kisiga, tumetengeneza picha gani, siku ambayo atakuwa babu na atakuwa kazungukwa na wajukuu zake na kuwahadithia yaliyompata katika mchezo wa soka? Unadhani wajukuu zake wataupenda tena mpira? Zaidi watauenezea sifa mbaya. Tuko tayari kwa mchezo wetu pendwa kupewa sifa mbaya?

Kupanga ni kuchagua. Kisiga ni sehemu ya wachezaji wengine wengi wa Kitanzania waliodhulumiwa pesa zao na wakaamua kukaa kimya bila kuchukua hatua yoyote ile. Kwa hili la Kisiga ni kama ameamua kuishi kijamaa katika dunia ya kibepari. Mzaramo kanena Zuwa Diswa.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x