Sambaza....

Ndiyo usajili wa gharama msimu huu na ndiyo usajili ambao kila kona ulikuwa gumzo.

Kila mtu alishangaa kwanini Cristiano Ronaldo anaenda Italy, nchi ambayo kwa miaka ya hivi karibuni ushindani umekuwa finyu.

Juventus ameitawala ligi hii, hakuna ambaye ameweza kumzuia. Kila asubuhi pakikucha anawaza ashinde magoli mangapi.

Hali ambayo imemfanya aoneshe kuwa Seria A kuwa ni ligi ya timu moja. Kitu ambacho hakikuwepo awali.

Awali Seria A ilikuwa ligi ambayo kulikuwa na ushindani mkubwa. Hakukuwepo na timu moja tu ambayo ilikuwa imetawala hii ligi.

Kila msimu kulikuwa na ushindani kwa sababu timu nyingi zilizokuwa zinaonekana kubwa zilikuwa na uwezo mkubwa wa kumiliki wachezaji wakubwa wenye kuleta ushindani.

Lilikuwa jambo la kawaida kuiona Juventus kuwa na Paul Nedved, Del Piero, Fabio Cannavaro, Zlatan Ibrahimovich, huku Ac Milan ikiwa na kina Paul Maldini, Philipo Inzaghi, Nesta.

Wachezaji hawa walifanya hata michezo ya Derbies (wapinzani wa jadi) iwe inavutia kwa kiasi kikubwa.

Hata kama ingekuwa usiku wa saa sita , watu wengi walisubiri kushuhudia kipi ambacho kingetokea katika uwanja San Siro.

Mechi kati ya Ac Milan na Intermilan ilikuwa zaidi ya mechi, ilikuwa mechi ambayo mpira ulichezwa kwa hisia zote.

Kwa kifupi ilikuwa mechi ambayo Wataliano walifanikiwa kutuuzia mpira mzuri na wenye ushindani pamoja na hisia.

Tulizinunua bidhaa zao kwa sababu zilikuwa zenye ushindani mkubwa. Tulijivunia bidhaa zao kwa sababu zilikuwa zinatupa furaha.

Kwa kifupi ligi ya Seria A ilikuwa inavutia tofauti na kipindi hiki. Kipindi ambacho usingetegemea kumuona Cristiano Ronaldo anaenda sehemu ambayo haina ushindani kwa sababu yeye kazaliwa kwa ajili ya kushindana.

Hapendi kukaa sehemu ya kujifariji, sehemu ambayo inaushindani hafifu, sehemu ambayo inaonekana kuna mterezo kwa sababu maisha yake ameshayaweka katika daraja la ushindani.

Ndiyo maana alishindana England akawa mshindi, akaenda Hispania akashindana kisha akawa mshindi.

Mshindi ambaye aliweka alama nyingi katika klabu ya Realmadrid.Alama ambazo zilimfanya aoenekane ni mchezaji bora kuwahi kutokea katika nyasi za Santiago Bernabeua.

Hapana shaka aliweka Ufalme pale, hili siyo jambo la kuuliza. Ufalme ambao uliwaficha watu wengi.

Ufalme ambao ulifanya baadhi ya wachezaji kutumikia falme ya Ronaldo na kuacha kutumikia falme zao.

Siyo jambo la kushangaza kwa Karim Benzema msimu uliopita kuzomewa na kutukanwa na mashabiki wa Realmadrid kwa sababu hakufanya chochote kikubwa kujenga Ufalme wake.

Muda wote alikuwa kijakazi cha Cristiano Ronaldo, aliiingia uwanjani kwa kumtumikia Cristiano Ronaldo.

Ndiyo maana mashabiki wengi waliona hana msaada mkubwa kwenye kikosi cha Realmadrid na kumtaka aondoke.

Hawakutaka kumuona, pengine walikuwa sahihi lakini walisahau kitu kimoja tu, je Karim Benzema alikuwa anacheza sehemu ambayo anastahili kucheza?

Muda mwingi Karim Benzema alikuwa anatoka katika eneo la ushambuliaji wa kati ili kumpisha Cristiano Ronaldo.

Hii ilikuwa ni lazima afanye hivo , sawa lilikuwa eneo lake lakini lilikuwa eneo ambalo Cristiano Ronaldo alikuwa analipenda zaidi.

Hutakiwi kumnyima, ukimnyima ananuna, na akinuna mnagombana.

Karim Benzema hakutaka ugomvi na mtu aliamua kujitoa sadaka kwa ajili ya Cristiano Ronaldo.

Sadaka ambayo haikuonekana kwa mashabiki wengi wa Realmadrid. Hawakuona hata kidogo kitu ambacho Karim Benzema alikuwa anakufanya, kwao wao walitaka kumuona Karim Benzema akitengeza Ufalme.

Leo hii Cristiano Ronaldo hayupo tena. Karim Benzema yuko peke yake, yuko huru.

Anajenga Ufalme wake , hajengi Ufalme wa mtu tena na anacheza sehemu ambayo alizaliwa ili acheze.

Na anachokifanya hakuna shabiki wa Realmadrid atakayedhubutu kusema Karim Benzema aondoke kwa sababu Ufalme wake unaonekana na nguvu kwenye timu nzima.

Sambaza....