Ibrahim Ajib Migomba
Blog

Kuna hela za kina AJIB zinachukuliwa na kina Diamond

Sambaza....

Ukikanyaga kwenye jukwaa la uwanja wa Taifa kutazama siku ambayo Simba au Yanga wanacheza utagundua kitu kimoja kikubwa , timu hizi zinapendwa sana tena kupitilizwa .

Mapenzi haya huwa hayaishii kwenye timu pekee , huwa yanaenda mbali mpaka kwa mchezaji mmoja mmoja. Mashabiki wengi wana mapenzi na hawa wachezaji wao .

Kichuya

Mapenzi ambayo mpaka sasa hivi hakuna mchezaji ambaye amefanikiwa kuyageuza kutoka kwenye mahaba mpaka kwenye pesa . Mahaba ya mashabiki hawa ni pesa ambayo haijawahi kuwanufaisha wachezaji.

Inawezekana wachezaji hawa wakawa wanapendwa sana na mashabiki wao lakini wao wakawa hawawapendi mashabiki wao. Au inawezekana mapenzi haya huishia kwenye uwanja wa taifa tu.

Mapenzi haya hayajawahi kutafutiwa njia nzuri ya kutoka uwanjani mpaka kwenye makampuni ya wafanyabiashara mbalimbali ambayo hutafuta kila namna ya kutafuta balozi wa biashara zao.

Leo hii tunashuhudia mafanikio ya Cristiano Ronaldo ndani ya uwanja , mafanikio ambayo yamemfanya apate mashabiki wengi sana nje  ya uwanja , mashabiki ambao wamemfanya yeye apate hela kutoka kwenye makampuni mbalimbali.

Leo hii Cristiano Ronaldo peke yake anaingiza dollar milioni 44 kwa mwaka kupitia matangazo ya Nike, Herbalife, TAG Heuer, American Tourister, Egyptian Steel, PanzerGlass, MEO, Toyota3 na mengine mengi kwa sababu ya umaarufu wake nje  ya uwanja.

Hapa ndipo alipofanikiwa , kuhamisha umaarufu wake wa ndani ya uwanja na kuupeleka nje ya uwanja , kwa sasa anafunga magoli ndani ya uwanja na anafunga akaunti zake za pesa nje  ya uwanja.

Hapa ndipo mstari unaowatofautisha wachezaji wetu na wachezaji wa nje.  Wachezaji wetu hawajataka kabisa kuwa maarufu nje  ya uwanja ndiyo maana makampuni mengi ya kibiashara yameshindwa kuwapa bidhaa za kutangaza.

Hakuna  mchezaji hapa nchini anayesimama kama nembo kubwa ya kibiashara na hii ni kwa sababu wachezaji wetu hapa nchini siyo chapa za kibiashara,  chapa ambayo ina ushawishi mkubwa kibiashara .

Tuko kwenye dunia ya kidigitali,  dunia ambayo vitu vingi hufanyika kidigitali. Dunia ambayo kwa sasa ili bidhaa iweze kumfikia mlaji kwa kiwango kikubwa lazima utumie njia za kidigitali zaidi .

Wachezaji wetu kwa sasa hata account zao za Instagram hazina ushawishi wa kubeba bidhaa ya kampuni moja kwa ajili ya kuitangaza na kuwafikia walaji kwa kiasi kikubwa.

Inauma kuona Diamond Platnumz anachukua tangazo la mchezo wa kubahatisha wakati Ibrahim Ajib yupo , mtu ambaye alitakiwa kwa kiasi kikubwa kufikiria kuwa mtu wa kwanza kuwa balozi wa kampuni la mchezo wa kubahatisha kwenye michezo.

Hizi pesa ambazo kina Diamond Platnumz wanazipata ilitakiwa ziwe pesa za kina Ibrahim Ajib,  Kelvin Yondani , John Bocco , Jonas Mkude ila kwa sababu hawazitaki ndiyo maana zinaenda sehemu nyingine .

Sehemu ambazo wamefanikiwa kutengeneza wafuasi wengi kwenye mitandao ya kijamii tofauti na wachezaji wetu ambao wametengeneza wafuasi wachache kwenye mitandao ya kijamii , wafuasi ambao hawawezi kuwabeba kuwa mabalozi wa bidhaa mbalimbali.

Sambaza....