Blog

Kutoka Mjini Magharibi hadi Azam kisha Simba: Historia fupi ya Jeba hii hapa.

Sambaza....

Kifo cha Mchezaji wa zamani wa Azam, Simba na Mtibwa za Tanzania Bara Ibrahim Rajabu Juma ‘Jeba’ zimewashtusha wengi, wakiwemo wadau wa soka nchini na viongozi wa nyadhifa za juu wa mpira na hata wa kiserikali.

kwa upande wake Rais wa shirikisho la Soka Tanzania-TFF Wallace Karia ametuma salamu za rambirambi kwa Shirikisho la Mpoira wa miguu Zanzibar -ZFF na familia ya mchezaji huyo aliyefariki jana jioni katika hospitali kuu ya Mnazi Mmoja.

Katika salamu zake Rais wa TFF amesema amepokea kwa masikitiko taarifa za msiba wa Jeba.

Mohammed Seif King ni miongoni mwa aliyekuwa kocha na wakala wa Jeba enzi ya uchezaji wake. Huyu ndiye aliyempeleka Jeba Azam Fc, anaelezea safari yake na Jeba hadi pale umauti ulipomkuta.

“Cha kwanza ni kumshukuru Mwenyezi Mungu, kutokana na kazi yake lakini ni pigo kubwa sana katika tasnia ya mchezo wa mpira wa miguu. Ibrahim ni moja ya mafundi wachache kuwahi kutokea katika miaka ya hivi karibuni.

Kwa mara ya kwanza nilimuona Ibrahim kwenye uwanja wa Uhuru, zamani ukiitwa Taifa katika fainali ya Copa CocaCola kati ya Mjini Magharibi na Tabora.

Nilimuona pale na alicheza vizuri sana, nilimfuata na kuongea naye kwa sababu Azam FC muda huo walikuwa na mpango wa kuanzisha timu ya vijana, bahati nzuri tulikubaliana mimi na yeye na nikaanza kumuandalia safari nikampeleka AzamFC.

Mwaka 2009 alirudi nyumbani baada kutokuwa na maelewano na klabu hiyo, nikatumwa tena nimfate, nilimfuata nikazungumza naye na akakubali kurudi na kuendelea kucheza Azam chini ya Mbrazil Itamar Amorim, huyu ndiye kocha wa kwanza kumpandisha Jeba ‘senior team’.

Nilidumu naye hadi mwaka 2011 pale nilipoachana na masuala ya ukocha na mpira kiujumla na kuendelea na kazi zangu zingine, kwahiyo sikufuatilia tena masuala yao

Kabla sijakuwa naye na mpaka namuona katika timu ya Mjini Magharibi, Jeba ni mchezaji ambaye ana kiwango kinachostahili kusifiwa, ana mapungufu kama walivyo wachezaji wengine lakini ni mmoja kati ya wachezaji ambao tutawakumbuka sana katika tasnia hii.” Mohammed King alimaliza kwa namna.

kwa upande wake Rais wa ZFF, Seif Kombo (Seif Boss) amethibitisha kutokea kwa msiba huo, huku akionyesha kusikitishwa na msiba huo akisema kuwa Jeba alikuwa ni miongoni mwa wachezaji wenye vitu vingi mguuni vilivyohitajika kwa kizazi kijacho.

“Tumekosa kuona baadhi ya vitu… tuna masikitiko makubwa sana..” alisema Rais huyo.

Mwili wa Jeba utasafirishwa kutoka Magomeni Mjini majira ya saa nne asubuhi kuelekea kijijini kwake Ndigane kwa ajili ya mazishi.

Hadi Jeba anafariki alikuwa ni mchezaji wa timu ya Chuoni inayoshiriki ligi kuu visiwani Zanzibar, pia amewahi kuvichezea vilabu vya Azam, Simba na Mtibwa za Tanzania bara kwa vipindi tofauti tofauti.

Mtandano wa Kandanda umepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha fundi huyu wa soka. Rehema na Amani za Mwenyezi Mungu zimfikie huko aliko, Ameen!


Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x