Ligi Kuu

Macho yangu yanatamani kumuona Lwandamina

Sambaza....

Mvua ilikata ghafla, manyunyu yakabaki katika anga la klabu Yanga. Dalili ya kwamba mvua ya neema ilikuwa inapotea na kiangazi kukaribia zilianza kuonekana baada ya mwenyekiti wa timu hiyo Ndugu. Yusuph Manji kujiweka pembeni na klabu hii.

Hali ilianza kubadilika taratibu kwa sababu Ndugu. Yusuph Manji ndiye alikuwa kiungo muhimu sana hasa hasa kwenye suala la uchumi.

Ilikuwa ngumu kusikia malalamiko kutoka kwa wachezaji kuwa hawajalipwa mshahara wao kwa miezi kadhaa mfululizo.

Njaa ilikuwa mbali sana, visima vya maji vilikuwa vinapatikana kwa wingi pale Jangwani, lakini alipoondoka Yusuph Manji ukame halisia wa jangawani tulianza kuushuhudia.

Dirisha la usajili lilidhihirisha yote haya, Yanga ilishindwa kufanya usajili nyota kama kipindi cha nyuma walivyokuwa wanafanya

Sajili za wachezaji vijana kutoka serengeti boys kama Ramadhani Kabwili, Yohana Nkomola, Said Musa na wengine ilidhihirisha Yanga hii inapitia nyakati ngumu kwa muda huo (simaanishi kuwasajili hawa vijana Yanga walikosea , hapana ila najaribu kuonesha utamaduni ambao awali hawakuwa nao kipindi walipokuwa na pesa za usajili)

Kocha George Lwandamina alikuwa na kikosi cha kawaida kilichokuwa kimejaa wachezaji wengi wa kawaida katika klabu isiyo kuwa ya kawaida.

Hofu ilijaa ndani ya mioyo ya wana Yanga, wengi waliona ni ngumu kwa Yanga kufanya vizuri kwa sababu ya kikosi walichokuwa nacho.

Kikosi ambacho kilionekana hakina ushindani mkubwa ukilinganisha na vikosi vilivyopita, ilikuwa ngumu kuamini George Lwandamina kama atatumia kikosi hiki kupambana kwa ajili ya ubingwa.

Mzimu wa majeruhi ukauvaa tena, matatizo yakawa yanarundikana baada ya tatizo. Hali ya uchumi ndani ya klabu ikaungana na hali ya majeruhi ya wachezaji nyota ndani ya timu

Timu ikawakosa wachezaji nyota ambao walikuwa mhimili mkubwa ndani ya misimu kadhaa waliyobeba ubingwa

Kila mtu ndani ya Yanga alitembea akiwa ameinamisha kichwa, swali kubwa ni namna gani Yanga inaweza kukimbia bila ya wachezaji wake nyota.

George Lwandamina hakuamini kama huo ni mzigo mzito kwake, aliamini kila mchezaji ndani ya kikosi cha Yanga alisajiliwa kwa ajili ya kuwapa matokeo chanya Yanga.

Akaingiza sumu kali ndani ya wachezaji wa Yanga, wakapigana bila kuwa na hofu kuwa wachezaji nyota wa kikosi hicho hawapo

Wakaitumia nafasi hiyo kuonesha kiwango chao , kiwango ambacho ƙkiliwasaidia kwa kiasi kikubwa kupata alama ambazo zilikuwa na msaada kwao.

Hata katika mechi za kimataifa walijitengenezea mazingira mazuri ya wao kufuzu kwenda katika hatua ya makundi ya kombe la shirikisho barani Afrika.

Pamoja na matatizo mengi ndani ya timu, Lwandamina hakuonekana kutetereka, leo hii hayupo na timu

Leo hii kaiacha Yanga katika kipindi cha muhimu sana, kipindi ambacho Yanga inamwihitaji yeye kwa kiasi kikubwa

Kipindi ambacho Yanga inahitaji kutetea kombe lao la ligi kuu na kufika mbali katika michuano ya kimataifa.

Hawana kiongozi tena, uwepo wake ulikuwa muhimu sana ndiyo maana tuliona katika michuano ya kombe la mapinduzi Yanga wachezaji walikuwa wapweke sana , timu haikuwa na morali kwa sababu baba wa timu hakuwepo kwenye benchi la ufundi.

George Lwandamina alikuwa zaidi ya baba pale Yanga, kuna wakati alitoa pesa zake mfukoni kuwahudumia wachezaji wake

Wachezaji walimsikiliza yeye na kupigana kutokana na maagizo yake , leo hii hayupo tena.

Wasiwasi unanikamata ninapofikiria Yanga watakavyoenda kucheza katika mechi za kimataifa. Morali ya kupigana itakuwepo ndani yao kipindi hiki ambacho hali ya uchumi ni mbaya ndani ya klabu?

Nani atawaambia wapigane kwa matumaini ya kupata kesho? Nani atawapoza kwa kidogo chake kipindi hiki ili wapigane na njaa??

Hapa ndipo huruma inaponivaa, Yanga imeachwa kipindi ambacho ilikuwa inamwihitaji sana George Lwandamina, kipindi ambacho ilitakiwa ifuzu kwenye hatua ya makundi ya kombe la shirikisho na kutetea ubingwa

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x