Sambaza....

Kabla ya ligi kuanza kulikuwa na vitu vingi sana vya kuvutia. Vitu ambavyo vilitufanye tuanze kuisubiri ligi kwa hamu.

Kuna wengi waliangalia vitu vingi kulingana na wao wanavyopenda. Wapo ambao walizitazama Simba na Yanga kwa jicho la shauku.

Hapana shaka shauku ya kuzitazama Simba na Yanga huanzia kwenye aina ya usajili ambao timu hizi hufanya.

Usajili ambao timu hizi hufanya ndiyo huwa unasababisha watu wengi kusubiri ligi kwa hamu na ikizingatia na magazeti yetu huchombeza sana.

Siyo kitu cha kushangaza kukutana na kichwa cha habari ambacho kimejaza sifa kibao za mchezaji ambaye amesajiliwa na timu hizi za kariakoo.

Hawa ndiyo wazee wa mpira wetu, kwa kufupi mpira wetu umeshikiliwa na timu hizi mbili kwa sababu ya idadi kubwa ya mashabiki walionao.

Ndizo timu pekee ambazo zimefanikiwa kujikusanyia mashabiki wengi na hii ni kwa sababu ya ukongwe wao.

Ndiyo maana siyo jambo la kushangaza kuona shabiki wa timu husika kati ya hizi mbili akisubiri kwa hamu kwa ligi kuanza ili kushuhudia mchezaji ambaye alikuwa ananadiwa kwa mbwembwe.

Ndiyo maisha ya mashabiki wa hivi vilabu viwili. Wana mapenzi yale ya dhati, mapenzi yaliyopitiliza. Kwa bahati mbaya walianza kuvipenda hivi vilabu kwanza kabla ya mpira.

Ukiachana na Simba pamoja na Yanga, klabu nyingine yenye mashabiki ambao wanaupendo wa dhati. Mashabiki ambao hawako mara mbili basi ni Coastal Union.

Wamiliki halali wa mahaba kwenye ligi kuu na ina mashabiki ni wa kweli na siyo mashabiki wa ambao huwa timu mbili kwa wakati mmoja (yani timu husika na timu ya Simba au Yanga).

Hii ni moja ya timu ambayo iliwafanya watu wengi kusubiri kwa hamu ligi kuu Tanzania, unajua kwanini ? , hii ni kwa sababu walimsajili mwanamuziki nyota hapa nchini Ally Kiba.

Mwanamuziki ambaye ana mashabiki wengi sana. Lilikuwa jambo la kushangaza sana kwa sababu mara nyingi tumezoea kumuona Ally Kiba akiwa kwenye muziki.

Hatukuwahi kumuona akiwekea mkazo kwenye suala la mpira wa miguu, na kama alikuwa anacheza basi alikuwa anacheza kwa ajili ya kujifurahisha tu.

Lakini masikio yetu yalipewa taarifa kuwa atakuwa mchezaji wa ligi kuu Tanzania akiwa na timu ya Coastal Union.

Tulimsubiri kwa hamu sana, matamanio yetu wengi yalikuwa kumuona akianza katika kikosi cha kwanza ili kuona uwezo wake kama unaweza ukawa mkubwa kama ambavyo alivyo kwenye muziki.

Baada ya muda mrefu, jana ikawa ndiyo mechi yake ya kwanza kuanza rasmi kwenye kikosi cha kwanza. Ukawa wakati sahihi wa kuona kitu kilichomo ndani ya miguu ya Ally Kiba.

Baada ya mchezo kuisha Ally Kiba alifanya mahojiano na Azam Sport HD, kuna kitu kimoja ambacho kiliongelewa kwenye mahojiano hayo.

Kitu ambacho kinaweza kuonekana ni kidogo lakini ni kikubwa sana na kinafaa kufanyika kwenye dunia hii ya sasa.

Ally Kiba alikuja na gari lake binafsi, hakuja na gari la timu kwa sababu haishi kambi. Kwa maana hiyo Ally Kiba huwa anaenda mazoezini akitokea nyumbani tena akiwa na gari yake ya gharama.

Tayari Ally Kiba ameanza kuishi kama anavyoishi Eden Hazard ndani ya ardhi hii ya Tanzania. Anakuja mazoezini akiwa na gari Kali tena akitokea nyumbani.

Haya ndiyo maisha ambayo wachezaji wa ligi yetu wanatakiwa kuishi. Wanatakiwa kuishi neno “Ligi yetu ni professionalism”.

Wawe na mikataba mizuri kuanzia kwenye timu na makampuni binafsi ili tu waweze kupata pesa za wao kuwa na gari kali, na siyo kuwa na gari kali tu pia wawe wanatokea nyumbani na gari zao.

Yani kwenye uwanja wa mazoezi zitapakae gari nyingi na wakimaliza mazoezi kila mtu awashe gari yake na kurudi nyumbani.

Hii ndiyo dunia ambayo tunatakiwa kuishi Leo, hatutakiwi kuishi jana, mchezaji kutokea kambini hiyo ni dunia ya jana.

Dunia ambayo wazee wetu waliishi, hatuko huko tuko leo mwaka 2018 wakati ambao wachezaji wanatokea majumbani kwao wakiwa na magari yenye gharama.

Sambaza....