Sambaza....

Kuelekea mchezo wa pili wa Wekundu wa Msimbazi katika kundi D klabu bingwa barani Afrika dhidi ya Pomboo Weusi, AS Club Vita utaochezwa siku ya jumamosi kule Kinshasa nchini Congo, msemaji wa mabingwa hao, Haji Manara amewataka mashabiki na wadau wa soka nchini kuwaombea ili wapate alama zote tatu katika mchezo huo wa ugenini.
“Tunajua Club Vita ina historia kubwa katika michuano hii kushinda sisi lakini Inshaallah tutaibuka na ushindi”
“Tunahitaji dua za mashabiki kama wawakilishi wa nchi, lakini hata hivyo siwezi kujiwekea ushindi wa moja kwa moja, lakini kama klabu tuko vizuri” aliongeza msemaji huyo.
Kuhusu saikolojia ya wachezaji kuelekea mchezo huo, Manara amesema kuwa, saikolojia ya wachezaji ni nzuri kuelekea mchezo huo, wanajua majukumu yao na nini wafanye kwa mechi za ugenini dhidi ya timu kama hii.

Taarifa

Tarehe Muda Ligi Msimu Mwisho
19/01/2019 7:00 pm Klabu Bingwa Afrika Kundi D 2018-2019 90'


Kwa upande wake nahodha msaidizi, Mohamed Husseni, Zimbwe Juniour amesema kuwa, kama wachezaji wamejipanga kufanya vizuri katika mchezo huo.
“Tunajua umuhimu wa mechi hii, tunaijua timu tunayocheza nayo, ni kubwa, ipo nyumbani na kama tunavyojua mcheza kwao hutunzwa hasa na mashabiki”
“Kuna baadhi ya mashabiki watakuja kutuunga mkono kutoka nyumbani lakini watakaosalia huko dua zao ni muhimu, kwani kama wachezaji tupo tayari lakini tunahitaji hasa dua za Watanzania” aliongea Zimbwe.
Simba SC inaingia katika mchezo huo ikiwa inaongoza katika msimamo wa kundi D, ikiwa na alama 3 na magoli matatu kibindoni, ikifuatiwa na Al ahly ya Misri yenye alama 3 na magoli mawili. AS Club Vita inaingia katika mchezo huo ikiwa na hasira baada ya kujeruhiwa katika mchezo wake wa kwanza dhidi ya Al ahly baada ya kukubali kichapo cha goli 2-0 ugenini.

Sambaza....