Sambaza....

Mlinda mlango wa majogoo wa jiji la Liverpool, Simon Mignolet ameondolewa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Ubeligiji ambacho kitapambana katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Scotland kisha mpambano wa ligi ya mataifa ya Ulaya (UEFA Nations League) dhidi ya Iceland.

Mignolet alikua miongoni mwa wachezaji walioitwa na kocha mkuu Roberto Martinez, kwa ajili ya mchezo wa kesho Ijumaa dhidi ya Scotland, lakini amelazimika kuondoka kambini kufuatia kuumia mkono akiwa mazoezini.

Mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 30, anatarajiwa kuwa fit baada ya juma moja, na huenda akawa miongoni mwa wachezaji wataosafiri kuifuata Tottenham Hotspurs Septemba 15, katika ligi ya England.

Mignolet kwa sasa ni mlinda mlango chaguo la pili katika kikosi cha Liverpool, baada ya kusajiliwa kwa Alisson Becker akitokea AS Roma na kuondoka kwa Loris Karius alieuzwa kwa mkopo Besiktas.

Endapo atashindwa kuwa sehemu ya kikosi cha Liverpool kitakachosafiri hadi jijini London mwishoni mwa juma lijalo, huenda meneja wa majogoo hao Jurgen Klopp akawachukua kikosini makipa vijana Kamil Grabara na Caoimhin Kelleher.

Wawili hao wenye umri wa miaka 19, walitumika wakati wa michezo ya kujiandaa na msimu wa 2018/19, na hawajawahi kucheza mchezo wowote wa ligi ya England.

Sambaza....