Sambaza....

Klabu ya soka ya Ruvu Shooting ya Mlandizi Mkoani Pwani, imelitaka shirikisho la soka nchini ‘TFF’, kuwapatia vibali wachezaji wanane wa timu hiyo ili waweze kucheza mechi za ligi Kuu baada ya kukosa leseni kutokana na matatizo ya kimtandao kati ya TFF na shirikisho la soka ulimwenguni ‘FIFA’.

Msemaji wa Klabu hiyo Masau Bwire amesema wanakutana na madhira mengi kutokana na hilo wakati ambapo ligi kuu soka Tanzania Bara inashika kasi huku sababu kubwa ya hilo kutokea ikiwa ni matatizo ya mfumo wa TFF-FIFA Connect.

“Unajua tunakutana na matatizo makubwa kutokana na kuwakosa wachezaji hawa, tulienda Mbeya na wachezaji 18, tumefanya mazoezi na kujiandaa na mchezo dhidi ya wachezaji 8 wakazuiwa eti kwamba usajili wao haujakamilika, tumeingia uwanjani tukiwa na wachezaji 10 uwanjani hakuna mchezaji hata mmoja wa akiba, ambaye ni kipa Bidii Hussein sasa fikiria katika mazingira hayo unaweza kupambana na kupataje matokeo!?” Masau akahoji.

Amesema hata Bidii Hussein hapo awali aliambiwa kuwa hakuwa na Leseni lakini dakika chache kabla ya mchezo kuanza walifanikiwa kupata leseni yake ambayo ilitumwa kutoka Dar es Salaam ikabidi awekwe benchi na kipa aliyekuwa anaumwa akaanza na mchezo huo kuisha kwa sare ya 2-2 dhidi ya Tanzania Prisons.

“Sasa kwa kuwa suala hili limechukua muda mrefu na sio kosa letu sisi Ruvu Shooting wala la wale wachezaji ambao ni wa kikosi cha kwanza , ila ni kosa la kimtandao tunawaomba TFF waangalie namna nyingine ya kufanya ili na sisi tunufaike na wachezaji hawa wakati ambapo tunasubiri mtandao ukae sawa, kwa sababu tumewasajili ili waitumikie klabu yetu,” Masau amesema.

Mbali na changamoto hizo, kikosi hicho kitashuka dimbani kucheza dhidi ya African Lyon Alhamisi hii katika uwanja wake wa Mabatini uliopo Mlandizi mkoani Pwani ikiwa ni mechi ya muendelezo kwenye ligi kuu soka Tanzania Bara msimu wa 2018/2019.

Ruvu Shooting inashika nafasi ya 18 katika msimamo wa timu 20 za ligi kuu kwa kujikusanyia alama mbili katika michezo mitano iliyocheza mpaka hivi sasa.

Sambaza....